Wednesday, 30 November 2011

KATIBA MPYA: CUF NAO WAPIGA HODI IKULU, JK AWAKUBALIA.

 
Ofisi ya Rais, Ikulu, imepokea barua kutoka Chama cha Wananchi (CUF) kikiomba kukutana na kufanya mazungumzo na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete.

Mheshimiwa Rais amekubali ombi hilo la CUF na ameelekeza maandalizi ya mkutano huo yafanyike mara moja.

Imetolewa na:

Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.

30 Novemba, 2008

RAIS OBAMA AIPONGEZA TANZANIA KUFIKISHA MIAKA HAMSINI YA UHURU


Rais Obama
Rais wa Marekani Mheshimiwa Barak Obama ametuma salamu za pongezi na za kuitakia baraka Tanzania wakati inapoadhimisha miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara. Tanzania Bara inatimiza miaka 50 ya Uhuru Ijumaa ya wiki ijayo, Desemba 9, 2011.

Aidha, Rais Obama ameihakikishia Tanzania kuwa Marekani itaendelea kubakia rafiki na mshirika wa kuaminika katika jitihada za kuhakikisha kuwa Watanzania kujiletea maisha bora na kwa njia za amani.

Katika salamu zake kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, Rais huyo wa Marekani ametumia lugha ya Kiswahili kuitakia baraka Tanzania akimwandikia Mheshimiwa Kikwete, “Mungu awabariki” na kufuatiwa na tafsiri ya maneno hayo hayo katika lugha ya Kiingereza.

Katika salamu zake, Rais Obama ameongeza kuwa umbali mkubwa wa kijiografia kati ya Tanzania unazidi kupungua kwa sababu ya uhusiano wa karibu kati ya Wamarekani na Watanzania.

Amesisitiza Rais Obama, “Hali ya kuwa anuwai ya taifa lako, kama ilivyo ya kwetu, ni chimbuko na msingi wa nguvu zitakazoipitisha Tanzania katika mabadiliko mengi na changamoto nyingi zinazokabili nchi yenye demokrasia inayopanuka.”

Imetolewa na:

Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.

30 Novemba, 2001

JUSSA: CUF KUANZA KUZUNGUKA NCHI NZIMA DESEMBA KUZUNGUMZA NA WANANCHI

Naibu Katibu Mkuu wa CUF (Zanzibar), Ismail Jussa
"Programu ya viongozi wa Chama kuwafikia wananchi na wanachama wa CUF kwa Tanzania Bara na Zanzibar itaanza rasmi mwezi Desemba na kuendelea nchi nzima. Ajenda ni mwelekeo wa siasa za nchi na mjadala wa Katiba Mpya ambayo imekuwa ajeda ya CUF tokea kuasisiwa kwake, imekuwa katika ilani zake zote za uchaguzi na pia ilikuwa dai mojawapo kati ya madai matatu ya maandamano ya Januri 27, 2001".

RAIS KIKWETE ASAINI MUSWADA WA SHERIA YA MABADILIKO YA KATIBA YA MWAKA 2011

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete leo, Jumanne, Novemba 29, 2011, ametia saini Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya Mwaka 2011.

Hatua hiyo ya Mheshimiwa Rais kutia saini Muswada huo inakamilisha safari ya kutungwa kwa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya Mwaka 2011 baada ya Bunge kuwa limepitisha Muswada huo uliowasilishwa na Serikali katika kikao kilichopita cha Bunge.

Aidha, kutiwa saini kwa Muswada huo ili uwe Sheria ni hatua kubwa na muhimu katika safari ya kutungwa kwa Katiba mpya ya Tanzania kama ilivyoahidiwa na Mheshimiwa Rais Kikwete katika salamu zake za Mwaka Mpya kwa wananchi Desemba 31, mwaka jana, 2010.

Pamoja na kutiwa saini hiyo bado Serikali itaendelea kusikiliza maoni na mawazo ya wadau na wananchi mbalimbali kuhusu namna ya kuboresha sheria hiyo.

Hivyo, Mheshimiwa Rais Kikwete anatoa wito kwa mwananchi yoyote mwenye maoni ama mawazo ya namna ya kuboresha Sheria hiyo, ajisikie yuko huru kutoa maoni yake na Serikali itasilikiza na kuchukua hatua zipasazo.


Imetolewa na:



Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,

Ikulu,

DAR ES SALAAM.



29 Novemba, 2011


UZINDUZI WA PROGRAMU YA MIUNDO MBINU YA MASOMO UONGEZAJI THAMANI NA HUDUMA ZA KIFEDHA VIJIJINI-ZANZIBAR

Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar Balozi Seif Ali Idd akisalimiana na baadhi ya viongozi waliohudhuria katika uzinduzi wa Programu ya Miundo mbinu ya Masoko, Uongezaji Thamani na Huduma za Kifedha Vijijini katika hafla iliyofanyika Ukumbi wa Salama Hoteli ya Bwawani Mjini Zanzibar

Viongozi mbalimbali waliohudhuria katika Uzinduzi wa Programu ya Miundo mbinu ya Makomo, Uongezaji Thamani na Huduma za Kifedha Vijijini wakimsikiliza Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar Balozi Seif Ali Idd hayupo pichani katika hafla iliyofanyika Ukumbi wa Salama Hoteli ya Bwawani Mjini Zanzibar.

 
Na Hamad Hija –.Maelezo Zanzibar



Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd amesema kuwa utekelezaji wa Programu ya Miundo mbinu ya masoko, Uongezaji thamani na Huduma za kifedha vijijini utasaidia sana kusukuma mbele maendeleo ya wakulima wafugaji pamoja na wavuvi wanaoishi vijijini.



Balozi Seif ameyasema hayo huko katika ukumbi wa Salama Hall Bwawani mjini Zanzibar wakati akizindua programu ya miundombinu masoko na uongezaji thamani na huduma za kifedha Vijijini kwa upande wa Zanzibar.



Alisema kwamba mpango huo wa utelekelezaji wa mifumo ya masoko kwa upande wa Tanzania Bara umeweza kuwanufaisha walengwa na kuongeza bei ya mazao yao kwa wastani wa mara mbili zaidi ya kile ambacho wakulima walikuwa wakikipata hapo awali.



Aidha amekumbusha kuwa kutokana na mafanikio yaliyopatikana  kupitia mpango huo Serikali ikishirikiana na washirika wa maendeleo  kama vile IFAD,ADB na ACRA ilionelea kuwa ni vyema mafanikio hayo kuenezwa na kupelekwa kwa wananchi walio wengi kupitia mpango huo ikiwemo vijiji vya Zanzibar.



Amesema kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imekuwa ikichukuwa hatua mbali mbali katika kuimarisha miundo mbinu ya umwagiliaji maji,  kuongeza ruzuku  ya pembejeo  na utekelezaji wa programu mbali mbali za kuendeleza kilimo uvuvi na ufugaji kwa lengo la kupunguza umasikini na kuongeza kipato cha wakulima.



Balozi Seif Ali Idd amefahamisha kuwa sekta ya kilimo ni muhimu sana kwa vile imekuwa ikitowa ajira kwa zaidi ya asilimia 70 na kuchangia asilimia 50 ya chakula katika Nchi yetu.



Aidha Balozi amesema kuwa hatuwa ya kuzindua programu hii ni hatua moja wapo ya kupunguza umasikini na kujitosheleza kwa chakula ambapo hiyo ndio sera ya maendeleo inayolenga maendeleo endelevu na kuongeza kipato kupitia kazi za wajasiriamali nchini.



Naye Mratibu wa Programu hiyo Khalfan Masuod  Saleh amesma kuwa uzinduzi huo ambao umefanywa hivi leo  ni mpango ambao unagharamiwa kwa  pamoja na Serikali ya Muungano ya Tanzania  ambapo kwa upande wa Serikali ya Muungano imetoa Dola za kimarekani Milion 9.6, Mfuko wa kimataifa wa Maendeo ya Kilimo (IFAD) umetoa Dola Milion 90.6



Aidha Bank ya Kimaendeleo ya Afrika (ADB) imetoa Dola za kimarekani 62.9 ambapo kwa upande wa Taasisi ya Mapinduzi ya Kijani ya Afrika (ACRA) imechangia kwenye mfuko huo jumla ya dola za kimarekani 6.9



Akizungumzia mpango huo mratibu huyo amesema kuwa lengo kuu la mpango huo ni kwa ajili ya wanawake ambapo itajenga uwezo kwa wakulima na kuwaunganisha na masoko ili kuhakika suala lao la masoko nchini linapatiwa ufumbuzi.



Khalfan amesema kuwa Programu hiyo itawajengea uwezo wakulima ili wapate taarifa mbali mbali zinazohusiana na shughuli zao kwa kuwaunganisha na makampuni mbali mbali.



Ameongeza kuwa mpango huo unategemewa kuwa wa muda wa miaka sita kwa kuwa utaendeshwa Tanzania nzima na unategemewa kufikia kaya laki tano vijijini.  



Amesema lengo kuu la mpango huu ni kuongeza kipato cha uhakika wa chakula vijijini kwa njia endelevu hususani  kuboresha miundo mbinu ya masoko ili kuwajengea uwezo wananchi waishio vijijini



Programu hiyo pia itawawezesha wakulima kuyafikia masoko na kuongeza thamani ya mazao yao ya kilimo pamoja na kupanuwa wigo wa huduma za kifedha vijijini.




MAGARI YA JESHI KUTUMIKA KUSOMBA MAHINDI - WAZIRI MKUU

Pinda
WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amesema Serikali imefikia uamuzi wa kutumia majeshi yake ili kusomba mahindi yaliyolundikana katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini na kuyapeleka katika mikoa yenye upungufu mkubwa wa chakula.

Amesema uamuzi huo umechukuliwa baada ya kubaini kuwa kasi ya kusafirisha mahindi kwa njia ya reli peke yake ni ndogo na haikidhi mahitaji yaliyoko katika mikoa ya Shinyanga na maeneo mengine ya Kaskazini.

Ametoa kauli hiyo jana usiku (Jumatatu, Novemba 29, 2011) wakati akizungumza na wakazi wa mikoa ya Rukwa, Ruvuma na mkoa tarajiwa wa Katavi katika chakula cha jioni ambacho aliwaandalia kwenye makazi ya Waziri Mkuu, Oysterbay jijini Dar es Salaam.

Wakazi hao zaidi ya 100 walikuwa wamealikwa kuja jijini Dar es Salaam kushiriki tamasha la Utamaduni la mikoa ya Rukwa na mkoa tarajiwa wa Katavi ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara. Tamasha hilo lilifanyika Novemba 25-27, 2011, katika kijiji cha Makumbusho jijini Dar es Salaam.

“Tunatarajia ifikapo wiki ijayo tutakuwa tumemaliza kulipa madeni ya watu waliouza mazao yao… tunadaiwa kiasi cha sh. bilioni 13.6/-. Tukimaliza kulipa madeni, tumeamua tuwape jeshi kazi ya kusomba mahindi ili yaondoke haraka na yale waliyovuna wakulima yapate mahali pa kuhifadhiwa,” alisema.

Alisema Serikali imekwishapata mkopo sh. bilioni 20 kutoka kwenye mabenki na kwamba fedha hizo ndizo zitatumika kulipa madeni inayodaiwa na wakulima waliouza mahindi yanayohifadhiwa na Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) katika vituo vya Makambako, Songea na Sumbawanga.

Kati ya tani 114,117 za mahindi ambazo zimepokelewa katika vituo vya ununuzi, NFRA imeweza kulipia tani 80,615 tu na kushindwa kulipia tani 33,502 zilizopokelewa kutokana na ufinyu wa bajeti.

Alisema ili kukabiliana na tatizo la mlundikano wa mazao katika maghala ya kuhifadhia mazao, wamekubaliana na Rais Jakaya Kikwete kwamba mwakani Serikali itaruhusu mapema sekta binafsi inunue mazao kutoka kwa wakulima ili kuwe na soko la uhakika kwa wakulima.

“Tutaweka bei ya gunia iwe sh. 38,000/- na tani moja iuzwe kwa sh. 380,000/- … Bei inaweza kupanda lakini haipaswi kuwa chini ya hapo ili wanunuzi wasiwalalie wakulima. Tulichoamua ni kwamba wanunuzi waingie mkataba na Mkuu wa Mkoa ili kuwe na ufuatiliaji wa karibu,” alisema huku akishangiliwa.

Alisema utaratibu huo utaanza mapema ili tatizo la mlundikano wa mazao lililojitokeza mwaka huu lisiweze kujirudia. Alisema ameamua kutoa ujumbe huo kwao kwa vile wanaiwakilisha mikoa ya Rukwa, Ruvuma na mkoa tarajiwa wa Katavi lakini hali ni hiyo hiyo hata akienda Iringa au Mbeya.



IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 3021,
DAR ES SALAAM.
JUMANNE, NOVEMBA 29, 2011

WAZIRI MKUU ASISITIZA WAWEKEZAJI SIYO LAZIMA WATOKE NJE, ASEMA NA YEYE PIA NI MWEKEZAJI


Pinda
WAZIRI MKUU, Mizengo Pinda amesema suala la uwekezaji hapa nchini haliwalengi watu wa nje tu bali hata wa ndani wanaweza kuwekeza hata kama ni kwa kiwango kidogo.

Ametoa kauli hiyo jana usiku (Jumatatu, Novemba 29, 2011) wakati akizungumza na wakazi wa mikoa ya Rukwa, Ruvuma na mkoa tarajiwa wa Katavi katika chakula cha jioni ambacho aliwaandalia kwenye makazi ya Waziri Mkuu, Oysterbay jijini Dar es Salaam.

Wakazi hao zaidi ya 100 walikuwa wamealikwa kuja jijini Dar es Salaam kushiriki tamasha la Utamaduni la mikoa ya Rukwa na mkoa tarajiwa wa Katavi ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara. Tamasha hilo lilifanyika Novemba 25-27, 2011, katika kijiji cha Makumbusho jiini Dar es Salaam.

Akifafanua kuhusu uwekezaji Waziri Mkuu alisema yeye alipochukua mkopo waliopatiwa wabunge wa sh. milioni 90, hakuona haja ya kununua gari bali aliamua kuwekeza katika ujenzi wa nyumba ya kulala wageni kijijini kwao, Kibaoni wilayani Mpanda.

“Nilichukua mkopo mwingine benki ya NMB na kuamua kujenga vyumba 24 pale kijijini kwetu. Kama ningetaka ningechukua mafundi wazuri kutoka Kariakoo, (Dar es Salaam) lakini niliamua kutumia mafundi wa kijijini ili kutokana na zile fedha nao pia waweze kununua bati na kuezeka katika nyumba zao, jambo ambalo limewezekana,” alisema.

“Ujenzi wa vyumba 24 karibu unakamilika, … kiasi kingine cha fedha nililima shamba la mahindi na nikafanikiwa kuvuna magunia 380,” aliongeza.

Waziri Mkuu anasema aliamua kuuza magunia 300 kati ya hayo aliyovuna na kupata sh. milioni 11 ambazo aliziwekeza tena katika mradi wa ufugaji nyuki kijijini kwao na Dodoma.

“Nina mizinga 250 kule Dodoma na Kibaoni (kijijini kwao) nina mizinga 600, kila mzinga unauzwa sh. 50,000/- na kila mmoja una uwezo wa kutoa lita 10 za asali. Bei ya asali hapa mjini ni sh. 10,000/- kwa hiyo katika kila mzinga unaweza kupata sh. 100,000/-,” alisema.

Alisema suala la uwekezaji ni muhimu na haliepukiki na kumtaja Mbunge wa Mpanda Mjini, Bw. Said Arfi ambaye alikuwepo katika hafla hiyo kwamba ni miongoni mwa wawekezaji wadogo kwani ana ekari 200 za mahindi na Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga, Kanali Antonio Mzurikwao kuwa naye ana ekari 100 za mahindi. “Hawa nao ni wawekezaji lakini tunawaita wawekezaji wadogo,” alisema.

Akifafanua kuhusu uwekezaji, Waziri Mkuu alisema nchi zote zilizoendelea zilifaulu kufiki hatua hiyo kwa kupunguza idadi ya wakulima wadogo na kuongeza idadi wa wakulima wakubwa. “Mkiona wakulima wadogo ni wengi mjue kuwa bado hamjapunguza umaskini,” aliongeza.

Alisema Taifa bado linakabiliwa na changamoto ya kupunguza umaskini kwa kuhahakikisha kwamba kuna uzalishaji wa chakula cha kutosha ili watu kwanza washibe lakini pia akaongeza kusema kwamba inabidi uzalishaji uwe na tija ili wakulima wapate mazao mengi na kujiongezea kipato.

Akitoa shukrani katika hafla hiyo, Mbunge wa Mpanda Mjini, Bw. Said Arfi aliwashukuru wajumbe wa Kamati za maandalizi katika mikoa ya Dar es Salaam na Rukwa kwa maandalizi mazuri hadi wakafanikisha tamasha la utamaduni wa mikoa hiyo miwili.

Alisema utamaduni na lugha ni vitu vikubwa vinavyotambulisha utaifa wa watu na kwamba bila utamaduni hakuna Taifa. “Taifa lisilo na utamaduni ni Taifa lililokufa… tujihadhari kwani kumbukumbu zetu nyingi zimeanza kutoweka… wazo la kuanzisha hifadhi ya kumbukumbu kule nyumbani ni jema sana nami nitakuwa tayari kuwaunga mkono wakati wowote,” alisema huku akishangiliwa.

Aliwataka wana-Rukwa na mkoa tarajiwa wa Katavi wawe na umoja na kusisitiza kwamba siku zote wawe na mwamko mmoja wa kuleta maendeleo katika mikoa yao ya Rukwa na Katavi. “Tutumieni kila inapowekezekana sisi ambao tuko katika nafasi za uongozi ili tusaidie kuleta maendeleo kwa mikoa yetu,” alisema.


IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 3021,
DAR ES SALAAM.
JUMANNE, NOVEMBA 29, 2011