Showing posts with label Siasa na Jamii. Show all posts
Showing posts with label Siasa na Jamii. Show all posts

Sunday, 15 January 2012

ALIYEMPA MTEMA LESENI YA UDEREVA HAKUMTAKIA MEMA

Marehemu Mtema enzi za uhai wake.
Ni huzuni, majonzi na kwa wana familia ni pigo ambalo hawatalisahau milele. Ndio ameondoka, kwa sisi tunaoamini ‘kudra’ tunasema kwamba siku zimefika ama kwa imani ya marehemu tunaweza kusema ‘Bwana ametoa na Bwana ametwaa……”.
Naandika mistari hii ikiwa ni masaa kama 28 hivi yamepita tangu Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema) Regia Mtema afariki dunia jana pale karibu na Daraja la Ruvu barabara ya Morogoro, Mkoa wa Pwani kwa ajali ya gari.
Binafsi nimesikitika sana, nimesikitishwa na mambo mawili makubwa: 1. Mtema alikua bado kijana na alikua na matarajio mengi lakini Watanzania walikua na matarajio makubwa zaidi kutoka kwake. 2. Nimesikitishwa na taarifa kwamba marehemu alikua anaendesha gari mwenyewe.
Sote tunafahamu kwamba Mtema alikua mlemavu, hakua na mguu wa kulia ambao kwa magari ya auto ndio unaotumika kuendeshea.
Cha kushangaza ni kwamba pamoja na ulemavu huo bado Mtema alipewa leseni ya kuendesha gari na akawa anaendesha kwenye safari ndefu na kwenye barabara ambayo ina msongamano mkubwa kama hii ya Dar-Chalinze.
Nani kati yetu amewahi kujaribu kuendesha gari kwa mguu wa kushoto na akaona ugumu wake?, kwa kweli sio kitu rahisi hata kidogo.
Hata alipokua akitoa taarifa kwa waandishi wa habari jana, Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani mkoani Pwani, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Salehe Mbaga alieleza wazi kwamba kilichochangia kutokea kwa ajali ile ni ulimevu wa dereva akisema kwamba haikua rahisi kutumia mguu ule kufanya maamuzi ya haraka na sahihi.
Sasa tujiulize; nani alitoa leseni kwa marehemu? Taratibu gani za kisheria zilifuatwa mpaka akaonekana anastahiki? Bila shaka tumejifunza kitu kwa tukio hili la kusikitisha.
Kwahiyo wakati tunapita katika kipindi hiki cha majonzi na huzuni, tulitafakari na hili.

Tuesday, 3 January 2012

TAASISI ZANZIBAR ZATAKIWA KUSAIDIA UMMA

Na Iddi Haji Issa, Maelezo Zanzibar

Wito umetolewa kwa taasisi zote zisizo za kiserikali kubadilika kwa kutekeleza shughuli zilizo na manufaa kwa umma kuliko kwa mwanachama mmoja mmoja.

Wito huo umetolewa na Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Asaa Rashid wakati wa ufunguzi wa mradi wa kuongeza uelewa juu ya sera ya jumuiya zisizo za kiserikali (NGOs) Zanzibar katika ukumbi wa chuo cha elimu mbadala Rahaleo

Alisema kuwa jumuiya zisizo za kiserikali zinalo jukumu kubwa katika kutekeleza wajibu wake hii inamaana kuwa iwapo Serikali itafanya kazi yake , sekta binafsi nazo zikafanya kazi yake bila shaka mafanikio yatakuwa makubwa.

Kwa upande wa Wizara katibu amesema wamedhamiria kukiimarisha kitengo cha jumuiya na hivi karibuni wanatarajia kufanya kazi muhimu za kupitia sheria ya jumuiya ( sheria Nam 6 ya 1995)  ili kukiwezesha kuwafikia zaidi walengwa  ambao ni jamii.

Aidha ameziomba taasisi zote kufahamu kuwa sera hiyo inatoa mwelekeo wa tunakotaka kuelekea lakini sheria imebainisha zaidi yale yaliotajwa katika sera.

Katibu huyo amesema Sheria inazitaka jumuiya zote kuelekeza kikamilifu suala zima la kuhakikisha ripoti za hesabu za jumuiya zinawasilishwa na kuangaliwa kwa usahihi wa hali ya juu.

Aidha akichangia mradi huo Mwenyekiti wa Umoja wa Wavuvi wa Kojani ( KOFDO) Omari Muhammed Ally ameiomba Serikali kutokuangalia upande wa ardhi tu ila na upande wa bahari utizamwe kwani hali inazidi kua mbaya sambamba na kuwashirikisha Wavuvi kikamilifu katika kuundwa sheria zinazo husu maswala ya bahari.

Mradi huo ambao umeanza hivi karibuni unategemewa  utaendeshwa kwa muda wa mwaka mmoja  chini ya Zanzibar Current Generation Forum ZCGF




  

DKT BILAL KATIKA MSIBA WA BALOZI ATHUMAN MHINA LEO


Makamu Wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akisalimiana na Mwenyekiti wa Wazazi wa CCM Zanzibar, Bi. Dogo Mabruk, wakati alipokuwa akiwasili nyumbani kwa aliyekuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM Taifa, marehemu Balozi Athuman Mhina, kwa ajili ya kuhudhuria shughuli za maziko, Madale jijini Dar es Salaam, leo Januari 3, 2012. Kulia ni Sophia Simba. Picha zote na Muhidin Sufiani-OMR

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akiweka saini katika kitabu cha maombolezo wakati alipofika nyumbani kwa  aliyekuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM Taifa, marehemu Balozi Athuman Mhina, kwa ajili ya kuhudhuria shughuli za maziko, Madale jijini Dar es Salaam, leo Januari 3, 2012.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akisalimiana na Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Pius Msekwa, wakati akiwasili  nyumbani kwa aliyekuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM Taifa, marehemu Balozi Athuman Mhina, kwa ajili ya kuhudhuria shughuli za maziko, Madale jijini Dar es Salaam, leo Januari 3, 2012.



Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akijumuika na baadhi ya Viongozi na wananchi kuomba dua maalum kwa  aliyekuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM Taifa, marehemu Balozi Athuman Mhina, wakati wa shughuli za maziko zilizofanyika nyumbani kwa marehemu Madale jijini Dar es Salaam leo, Januari 3, 2012.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akiagana na Mufti Mkuu wa Baraza la waislam Tanzania, Sheikh Shaaban Simba, wakati akiondoka nyumbani kwa aliyekuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM Taifa, marehemu Balozi Athuman Mhina.

JK ATOA AGIZO LA KUMREJESHA MNYAMA

Rais Jakaya Kikwete ameiagiza taasisi ya utafiti wa wanyamapori (Tanzania Wildlife Research Institute - TAWIRI-) kutafiti sababu za kutoweka kwa mnyama aina ya Palahala (Roosevelt Sable Antelope) katika Hifadhi ya Taifa ya Saadani  mkoani Pwani na maeneo mengine  walikokuwa wakionekana kwa wingi hapo awali.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu leo, Rais Kikwete ametoa agizo hilo mwanzoni mwa wiki kwa Mkurugenzi Mkuu wa TAWIRI Dkt. Simon Mduma, baada ya kupokea maelezo ya  Mpango wa Kitaifa wa Kuhifadhi Tembo nchini  (Tanzania  Elephant   Management   Plan),  alipokutana na uongozi  wa taasisi hiyo katika hifadhi ya Taifa ya Serengeti mkoani Mara.
Mpango   huo  umeainisha   vipaumbele vinavyohitaji   kutiliwa   maanani   katika   kuhifadhi  na   kudhibiti  Tembo   katika   kipindi   cha miaka mitano ijayo.
Rais aliiagiza TAWIRI kwamba pamoja na kupata chanzo cha kutoweka kwa wanyama hao, pia itafutwe njia ya kuwarejesha tena, akisisitiza kwamba Palahala  ni mnyama anayevutia sana na  anaweza  akawa kivutio cha ziada katika Hifadhi ya Taifa ya Saadani,  hasa kwa utalii wa upigaji picha.
PALAHALA
Palahala ni mnyama anayevutia sana kutokana na umbo lake ambapo wawindaji hupendelea sana kumuwinda ili kupata pembe zake ndefu ambazo hutumika kama mapambo katika nyumba.  Pembe hizo pia hutumika kuchezea ngoma za kiasili.
 Rais Kikwete pia ameagiza kufanyike uchunguzi wa kina ili kujua sababu zilizosababisha kupungua kwa kasi kwa idadi ya tembo katika ukanda wa mbuga za wanyama za  Selous na Mikumi, baada ya kustushwa  na ripoti inayoonyesha kwamba zaidi ya tembo 30,000 wametoweka katika kipindi kifupi.
Rais alitoa agizo hilo baada ya Mkurugenzi Mkuu wa TAWIRI. Simon Mduma kutoa takwimu zilizoonyesha  kwamba  katika mbuga za Selous na Mikumi mwaka 2006 kulikuwa na tembo 74,900, na sensa iliyofanyika mwaka 2009 ilionyesha wamesalia 43,552.

Saturday, 10 December 2011

UHURU NI MIAKA 50: SHEREHE ZAFANA UWANJA WA UHURU

Rais Kikwete anakagua gwaride

Wanapendeza

Makomandooo

Makomandoooo

Mambo ya komandooo hayo

Kifaru



Hii ilikua inatoa heshima kwa kupinda bawa moja chini

Watoto wa halaiki

Hawa wamegonga 50, walizaliwa siku ya uhuru

Rais Kikwete anasema tumetoka mbali, tumefanya mengi lakini bado safari ni ndefu.

Monday, 5 December 2011

MWENGE WA UHURU HUOOOOO KUELEKEA KILELENI-MLIMA KILIMANJARO

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Mhe.Leonidas Gama akimpa mkono wa kumtakia heri mmoja wa vijana wanaopandisha Mwenge wa Uhuru kwenye kilele cha Mlima Kilimanjaro kwenye hifadhi ya Mlima Kilimanjaro zilizoko Marangu Mkoani Kilimanjaro leo tarehe 5.12.2011.

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Mhe. Leonidas Gama pamoja na Viongozi wa Mkaoa wa Kilimanjaro na wawakilishi wa Wizara ya Habari ,Vijana ,Utamaduni na Michezo wakiwasindikizaVijana wanaopandisha Mwenge wa Uhuru kwenye Kilele cha Mlima Kilimanjaro tayari kwa safari leo Marangu kwenye Hifadhi ya Mlima Kilimanjaro Mkoani Kilimanjaro.


Vijana wanaopandisha Mwenge wa Uhuru kwenye kilele cha Mlima Kilimanjaro wakiwa tayari kwa kuanzakupandisha mlima huo na Mwenge. Kwa picha zaidi; http://fullshangwe.blogspot.com/


Thursday, 1 December 2011

SHEREHE ZA KILELE CHA MBIO ZA MWENGE WA UHURU ZAFANA JIJINI DAR ES SALAAM LEO

Rais Jakaya Kikwete na Mkewe Mama Salma wakiwaslili Uwanja wa Uhuru kwenye kilele cha sherehe za mbio za mwenge.

Rais Jakaya Kikwete akiongozana na viongozi mbalimbali wa kitaifa kuelekea jukwaa kuu.

Maandamano ya wananchi.

Gwaride la Chipkizi


Wednesday, 30 November 2011

WAZIRI MKUU ASISITIZA WAWEKEZAJI SIYO LAZIMA WATOKE NJE, ASEMA NA YEYE PIA NI MWEKEZAJI


Pinda
WAZIRI MKUU, Mizengo Pinda amesema suala la uwekezaji hapa nchini haliwalengi watu wa nje tu bali hata wa ndani wanaweza kuwekeza hata kama ni kwa kiwango kidogo.

Ametoa kauli hiyo jana usiku (Jumatatu, Novemba 29, 2011) wakati akizungumza na wakazi wa mikoa ya Rukwa, Ruvuma na mkoa tarajiwa wa Katavi katika chakula cha jioni ambacho aliwaandalia kwenye makazi ya Waziri Mkuu, Oysterbay jijini Dar es Salaam.

Wakazi hao zaidi ya 100 walikuwa wamealikwa kuja jijini Dar es Salaam kushiriki tamasha la Utamaduni la mikoa ya Rukwa na mkoa tarajiwa wa Katavi ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara. Tamasha hilo lilifanyika Novemba 25-27, 2011, katika kijiji cha Makumbusho jiini Dar es Salaam.

Akifafanua kuhusu uwekezaji Waziri Mkuu alisema yeye alipochukua mkopo waliopatiwa wabunge wa sh. milioni 90, hakuona haja ya kununua gari bali aliamua kuwekeza katika ujenzi wa nyumba ya kulala wageni kijijini kwao, Kibaoni wilayani Mpanda.

“Nilichukua mkopo mwingine benki ya NMB na kuamua kujenga vyumba 24 pale kijijini kwetu. Kama ningetaka ningechukua mafundi wazuri kutoka Kariakoo, (Dar es Salaam) lakini niliamua kutumia mafundi wa kijijini ili kutokana na zile fedha nao pia waweze kununua bati na kuezeka katika nyumba zao, jambo ambalo limewezekana,” alisema.

“Ujenzi wa vyumba 24 karibu unakamilika, … kiasi kingine cha fedha nililima shamba la mahindi na nikafanikiwa kuvuna magunia 380,” aliongeza.

Waziri Mkuu anasema aliamua kuuza magunia 300 kati ya hayo aliyovuna na kupata sh. milioni 11 ambazo aliziwekeza tena katika mradi wa ufugaji nyuki kijijini kwao na Dodoma.

“Nina mizinga 250 kule Dodoma na Kibaoni (kijijini kwao) nina mizinga 600, kila mzinga unauzwa sh. 50,000/- na kila mmoja una uwezo wa kutoa lita 10 za asali. Bei ya asali hapa mjini ni sh. 10,000/- kwa hiyo katika kila mzinga unaweza kupata sh. 100,000/-,” alisema.

Alisema suala la uwekezaji ni muhimu na haliepukiki na kumtaja Mbunge wa Mpanda Mjini, Bw. Said Arfi ambaye alikuwepo katika hafla hiyo kwamba ni miongoni mwa wawekezaji wadogo kwani ana ekari 200 za mahindi na Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga, Kanali Antonio Mzurikwao kuwa naye ana ekari 100 za mahindi. “Hawa nao ni wawekezaji lakini tunawaita wawekezaji wadogo,” alisema.

Akifafanua kuhusu uwekezaji, Waziri Mkuu alisema nchi zote zilizoendelea zilifaulu kufiki hatua hiyo kwa kupunguza idadi ya wakulima wadogo na kuongeza idadi wa wakulima wakubwa. “Mkiona wakulima wadogo ni wengi mjue kuwa bado hamjapunguza umaskini,” aliongeza.

Alisema Taifa bado linakabiliwa na changamoto ya kupunguza umaskini kwa kuhahakikisha kwamba kuna uzalishaji wa chakula cha kutosha ili watu kwanza washibe lakini pia akaongeza kusema kwamba inabidi uzalishaji uwe na tija ili wakulima wapate mazao mengi na kujiongezea kipato.

Akitoa shukrani katika hafla hiyo, Mbunge wa Mpanda Mjini, Bw. Said Arfi aliwashukuru wajumbe wa Kamati za maandalizi katika mikoa ya Dar es Salaam na Rukwa kwa maandalizi mazuri hadi wakafanikisha tamasha la utamaduni wa mikoa hiyo miwili.

Alisema utamaduni na lugha ni vitu vikubwa vinavyotambulisha utaifa wa watu na kwamba bila utamaduni hakuna Taifa. “Taifa lisilo na utamaduni ni Taifa lililokufa… tujihadhari kwani kumbukumbu zetu nyingi zimeanza kutoweka… wazo la kuanzisha hifadhi ya kumbukumbu kule nyumbani ni jema sana nami nitakuwa tayari kuwaunga mkono wakati wowote,” alisema huku akishangiliwa.

Aliwataka wana-Rukwa na mkoa tarajiwa wa Katavi wawe na umoja na kusisitiza kwamba siku zote wawe na mwamko mmoja wa kuleta maendeleo katika mikoa yao ya Rukwa na Katavi. “Tutumieni kila inapowekezekana sisi ambao tuko katika nafasi za uongozi ili tusaidie kuleta maendeleo kwa mikoa yetu,” alisema.


IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 3021,
DAR ES SALAAM.
JUMANNE, NOVEMBA 29, 2011

Thursday, 10 November 2011

JAJI MKUU ZANZIBAR AWATUNUKU VYETI MAWAKILI KWA UTUMISHI ULIOTUKUKA

Khadija Khamis – Idara ya Habari Maelezo Zanzibar                           

Jaji Othuman
Jaji Mkuu wa Zanzibar Omar Othman Makungu  amewatunuku vyeti mawakili 22 wapya  na wawili wakongwe vya kuwakubali kuwatumikia wananchi katika mahakama mbali mbali hapa  nchini

Akiwatunuku vyeti hivyo huko mahakama kuu vunga alisema kwamba vyeti hivyo ni alama ya kukubaliwa kuwatumikia wananchi kwa uwadilifu na kuwatendea haki kisheria 

Alisema kuwa  taaluma hii ni ya wasomi na yenye heshima duniani, kwa hivyo wanapaswa kufanyakazi kwa kuzingatia nidhamu na maadili mema, ili kuepukana na tuhuma mbali mbali kwa wananchi.

Jaji Makungu amweatahadharisha wahitimu hao kuacha kabisa kujiingiza katika   masula ya rushwa na siasa, ili kuepuka kuingizwa mtegoni kwani fani yao ni chachu ya msingi katika mambo yote muhimu ya taifa .

“samaki akioza mmoja huoza wote kwa hivyo muepukane na rushwa na kujiingiza katika mambo ya siasa ili msipatwe kuingizwa mtegoni ” alisema jaji huyo

Aidha alisema kuwa mawakili wakitekeleza majukumu yao kwa ufanisi mkubwa wananchi watafaidika sana na taaluma hiyo, kwa kusimamiwa haki zao ipasavyo bila ya kujali kujuana kwa mtu urafiki, udugu ,ukabila na kadhalika .

Alisisitiza kwa mawakili wapya kuenzi taaluma ya sheria ili isipoteze hadhi yake,na  wasikubali kuchafuliwa na baadhi ya wanasiasa na utapiamlo .wa mtu mwenyewe binafsi .
Pia amewataka mawakili hao kujadili mjadala wa katiba ya jamhuri ya muungano ili kuweza kutetea sheria za wananchi  wa Zanzibar kwa kuweza kupatiwa haki zao ipasavyo .

Nae Rais wa chama cha mawakili Awadh Ali Said amesema kuwa  siku hii ni muhimu na kihistoria katika  kuwekewa  kumbukumbu ya kupata mawakili wengi, ambao wataweza kutoa huduma za kisheria na kuweza kusambaa zaidi kwa jamii.

Amesema ongezeko la mawakili  pia ni fursa pekee kwa wananchi kuondokana na tatizo la uhaba wa mahakimu kwa lengo la  kupata haki zao, pamoja na kutendewa uwadilifu usio shaka bila ya aina Fulani ya kichocheo.

Aidha alisema kuwa vichocheo vya rushwa hutegemea muhusika mwenyewe amewekwa kwenye mazingira ya kuchochea rushwa pamoja na maslahi duni ambayo hayaendani na haki na majukumu ya kazi zao.

Kutunukiwa vyeti kwa mawakili 22 kunafanya idadi ya mawakili kufikia 163 tangu kuanzishwa kwa kitengo cha sheria mwaka 1967.

Friday, 4 November 2011

MHESHIMIWA MNYIKA UNAIFAHAMU BARABARA HII JIMBONI KWAKO?



Mnyika
 Takriban mwaka mzima sasa barabara hii  ya Tandale Uzuri imejaa mashimo na inaonekana kama imesahaulika. Wananchi na watumiaji wa barabara hii nikiwemo mimi najiuliza hivi watendaji wako wapi?

Kwa bahati mbaya au nzuri, barabara hii ipo kwenye Jimbo la Ubungo, Jimbo la John Mnyika ambaye anatokea chama cha Upinzani-CHADEMA, hili ni doa kwa uongozi wake ambao ndio kwanza una mwaka mmoja. Je Mheshimiwa anafahamu kwamba hii barabara ipo hivi? 

"Hali hii inasababisha tukose imani na wanasiasa, kwa kuwa ni mwaka jana tu walikuwa wanazunguka nyumba kwa nyumba wakisaka kura na moja ya ahadi zao ilikuwa kwamba wataboresha barabara, lakini kama uboreshaji wenyewe ndio huu basi naona hakuna haja ya kupiga kura," anasema mpiga kura mmoja wa Sinza ambaye barabara hii ni kero kwake.


Mzee huyu mwenye nguo nyeusi amejitolea kujaza kifusi kwenye barabara na anawatoza madereva kati ya shilingi mia na miambili, kwa sababu watumiaji wanakerwa na hali hii, basi hawana namna lazima watoe, lakini sasa huyu mzee naye hataki kumaliza haraka kwa kuwa hiki sasa kimekua kitega uchumi. (KUFA KUFAANA)


Hapa ukija kichwakichwa unavunja sample.

Kila mtu anapita pembeni, labda kazi ya kujaza kifusi ikikamilika italeta ahueni.

Tuesday, 18 October 2011

JK AMTEUA TENA BALAZO KAZAURA KUIONGOZA UDSM

Balozi Kazaura
Rais Jakaya Mrisho Kikwete amemteua Balozi Fulgence Kazaura kuwa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa kipindi kingine cha miaka minne.
Taarifa iliyotolewa leo, na Katibu Mkuu Kiongozi Phillemon Luhanjo imesema kuwa uteuzi huo unaanza mara moja (leo hii).
Balozi Kazaura alikuwa Mkuu wa Chuo hicho katika kipindi kilichopita  kilichoishia Julai, mwaka huu, 2011.

Wednesday, 5 October 2011

KIKWETE MGENI RASMI MKUTANO WA UWEKEZAJI RUKWA

Mkutano wa uwekezaji wa ukanda wa Ziwa Tanganyika mikoa ya Katavi, Kigoma na Rukwa utafanyika Wilayani Mpanda Mkoani Rukwa tarehe 17 Oktoba 2011 katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpanda, Mpanda mjini.
Mgeni rasmi katika mkutano huo atakuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete. Wageni wengine maarufu watakaokuwepo ni Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Mizengo Pinda, Mabalozi, Mawaziri, wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi na wadau wengine wa uwekezaji.
Rais Jakaya Kikwete (Kulia) na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.
Lengo la mkutano huo ni kuzinadi fursa nyingi za uwekezaji zilizopo katika Ukanda wa Uwekezaji wa Ziwa Tanganyika na kufungua ukanda huo ambao kwa mda mrefu ulikabiliwa na miundombinu mibovu hivyo kuwa vigumu kufikika.
Fursa hizo ni Madini, ardhi yenye rutuba inayofaa kwa kilimo, utalii (Kalambo Falls, Bismark Fort, Mv Liemba, Mbuga ya Katavi na Gombe Kigoma), biashara, miundombinu, elimu, afya na ufugaji.

Kwa kufungua ukanda huu itaongeza ajira kwa wananchi wa ukanda huo na hivyo kuinua uchumi wa Mtanzania.
Serikali ya Tanzania imeshachukua hatua ya kufungua ukanda huu kwa kuimarisha miundombinu ya barabara za lami, umeme, reli, viwanja vya ndege na usafiri katika Ziwa Tanganyika.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Eng Stella Manynya

Barabara ya Tunduma-Laela-Sumbawanga inajengwa kwa kiwango cha lami. Barabara ya Sumbawanga-Kasanga, Sumbawanga Mpanda nayo pia inajengwa kwa kiwango cha lami, miradi yote hii itakamila ifikapo mwaka 2013.
Kongamano hilo la uwekezaji litakuwa la aina yake kwani litaambatana na maonyesho ya siku nne kuanzia tarehe 15-18 mwenzi huu wa Oktoba ambapo wajasiriamali, wawekezaji na taasisi za Serikali watapata fursa ya kunadi sera zao, bidhaa na mipango mbalimbali kupitia mabanda.
Siku ya kongamano lenyewe tarehe 17 Oktoba 2011 kutakuwa na mijadala mbalimbali ambayo itaambatana na kila wilaya katika mikoa hii mitatu (Katavi, Kigoma na Rukwa) kuweza kunadi miradi yake ambayo inahitaji uwekezaji.
(Kwa hisani ya Mdau, Temba wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Rukwa)

Saturday, 1 October 2011

Hatua zichukuliwe kukabili mvua Dar es Salaam


Mvua za rasharasha zilizonyesha Jijini Dar es Salaam siku ya Ijumaa, zimeonyesha kwamba bado miundombinu ya maji taka jijini haipo katika hali nzuri.
Mvua hizi zinakuja siku chache tangu Mameya kutoka miji mbalimbali nchini walipofanya mkutano wao juzi jijini chini ya mwavuli wa Mtandao wa Miji Tanzania (TACINE).

Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Dk Didas Masaburi
Wakati wa mkutano huo, Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Dk Didas Massaburi alisema mambo kadhaa yamefanyika kuzuia mafuriko yanayosababishwa na miundombinu hafifu ya maji taka.
 
Massaburi aliyataja maeneo hayo kua ni pamoja na makutano ya barabara za Bibi Titi na Morogoro (eneo la NSSF Akiba) na Mtaa wa Uhio.

Eneo la Akiba (Makutano ya Bibi Titi na Morogoro Road)

Hata hivyo halihalisi iliyojitokeza siku ya Ijumaa inaonyesha kwamba tatizo bado ni kubwa na haswa ikizingatiwa kwamba yale yalikua manyunyu tu au rasharasha.
Hivyo ni vyema uongozi wa jiji ukajipanga vizuri zaidi katika kuhakikisha kwamba mitaro yote (sio Ohio na Akiba tu) inazibuliwa.


Uchafu
 Viongozi pia wanaowajibu wa kusimamia sheria ndogondogo za miji na majiji ipasavyo na kwa kufanya hivyo tutaepuka matatizo kama haya ya miundombinu ya maji taka kuziba.

Kwa mfano viongozi wote wanakiri kwamba, kutupa taka mitaani ovyo ni kosa la kisheria lakini nani amewahi kukamatwa jijini Dar es Salaam kwa kutupa chupa ya maji barabarani? Pengine hata wananchi wenyewe hawajui kwamba ni makosa kufanya hivyo. 
Taka hizo zinazotupwa ovyo ndio zinazoziba miundombinu ya maji taka na mwisho wa siku barabara za jiji zinageuka kua mito.
Wakati mwingine suala la usafi wa barabara zetu limekua halitiliwi maanani, michanga inajaa barabarani, haifagiliwi na matokeo yake mvua zinaponyesha michanga yote inasukumwa mitaroni na inapelekea kuziba.
Maswali ni mengi, kwa mfano barabara zetu zimejaa matangazo ya biashara lakini ni chafu. Mapato yanakwenda wapi?