Baada ya Kupokea hati ya utambulisho, Rais Dkt Jakaya Kikwete akimtambulisha balozi mteule wa Uswisi nchini Tanzania Mh Oliver Chave kwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya mambo ya nje na ushirikiano wa Kimataifa Balozi Rajabu Gamaha ambaye anafuatiwa na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya ma marekani Bi. Grace Changali na Mkurugenzi Msaidizi katika idara hiyo Bi Vic
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete leo, Jumanne, Novemba 15, 2011, amepokea hati za utambulisho za mabalozi wapya watakaoziwakilisha nchi za Uswisi na Ufaransa katika Tanzania.
Katika sherehe fupi iliyofanyika Ikulu, Dar es Salaam, Rais Kikwete amepokea hati za utambulisho kutoka kwa Balozi mpya wa Uswisi, Mheshimiwa Oliver Chave, na kutoka kwa Balozi mpya wa Ufaransa, Mheshimiwa Marcel Escure.
Katika mazungumzo yaliyofuatia baada ya kuwa amepokea hati za Mheshimiwa Chave, Rais Kikwete ameishukuru Uswisi kwa misaada yake ya maendeleo kwa Tanzania hasa katika nyanja ya afya. “Misaada yenu katika eneo hili, Mheshimiwa Balozi, imeleta mabadiliko makubwa katika maisha ya Watanzania. Tunawashukuru sana kwa misaada hiyo.”
Rais Kikwete amemwelezea Balozi Chave kuhusu mipango ya Serikali katika kuboresha maisha ya wananchi kupitia sekta ya afya na hasa juhudi za Serikali kuhakikisha kuwa inajenga zahanati kila kijijiji na kituo cha afya kila kata ili kupunguza umbali ambao wananchi wanatembea kutafuta huduma za afya.
Balozi Chave amemwambia Rais Kikwete kuwa Uswisi na wananchi wa nchi hiyo wanaipongeza Tanzania na kuitakia heri katika kuadhimisha miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara.
Katika mazungumzo na Balozi Escure, Rais Kikwete ameishukuru Ufaransa kwa misaada yake katika maeneo mbalimbali hasa ya maji na utalii ambako nchi hiyo imesaidia ujenzi wa chuo kipya cha kufundisha wataalam wa utalii nchini ambacho ujenzi wake umekamilika mjini Dar es Salaam.
“Tunaishukuru Ufaransa kwa kutujengea chuo hiki. Tunafanya vizuri sana katika sekta ya utalii lakini hatukuwa na chuo cha kuweza kutufundishia wataalam wetu katika eneo hili. Tunashukuru kwamba Ufaransa imesaidia kujengwa kwa chuo hicho,” amesema Rais na kuongeza:
“Tunashukuru pia kwa kusaidia miradi ya maji katika miji yetu midogo. Wakati mwingine ni rahisi kuboresha miundombinu katika miji mikubwa na kuisahau ile midogo lakini tunashukuru kwa msaada wenu katika eneo hilo.”
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu,
DAR ES SALAAM.
15 Novemba, 2011
|
No comments:
Post a Comment