Tuesday, 8 November 2011

MADIWANI ROMBO WASISITIZA WAO NI WATANZANIA

Habari na Picha kwa hisani ya SHABANI wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa-KLM

Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Rombo wamekana taarifa zilizoenea nchini kuwa wametaka kupandisha bendera ya Jamhuri ya Kenya kutokana na kuwekwa kizuizi cha kuingiza bidhaa katika eneo la Himo

Mwanzoni mwa juma lililopita zilienea habari  zilizodai kuwa  madiwani wa Halmasahauri hiyo walitishia kupandisha bendera ya nchi jirani ya Kenya kutokana na kuwekwa kizuizi cha kuzuia biashara ya magendo ya sukari na mahindi inayofanywa na baadhi ya wafanyabiashara kupeleka nchi za jirani bila kufuata taratibu.

Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Antony Tesha alisema hayo katika kikao cha dharura kilichoitishwa katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Rombo ili kumsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama alipotembelea wilaya hiyo kwa lengo la kukagua hali ya usambazaji wa sukari
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Rombo, Anthony Tesha (kushoto) akiwasilisha msimamo wa madiwani wa Halmashauri hiyo juu ya uvumi wa kutaka kupandisha bendera ya Kenya, katikati ni Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama na kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Rombo, Peter Toima Kiroya. 

“Sisi tulipomaliza uchaguzi na kuchaguliwa na wananchi kama wawakilishi wao tulikula kiapo cha utii kwa serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Rais Jakaya Mrisho Kikwete”alifafanua  Tesha

“Mheshimiwa  mkuu wa mkoa pamoja na mkuu wa wilaya sisi ndio wawakilishi wa wananchi hatuwezi kukiuka sheria za nchi na wala hatuwezi kudanganyika na maneno ya mitaani yanayoenezwa ambayo yanaweza kuvunja amani ya wilayani yetu lazima tusimamie sheria za nchi kama tulivyoapa”alisisitiza

“Sisi kama wawakilishi wa wananchi tutaendelea kulinda chama na serikali yake na hatutayumbishwa na itikadi za vyama tunavyotoka ila tuhakikisha sheria inafuatwa na jamii nzima ili kuendelea kuwahudumia wananchi wetu waweze kupata huduma zinazostahili”aliongeza mwenyekiti huyo

Naye Mkuu wa Mkoa Gama alisema kuwekwa kwa kizuizi katika eneo la Himo kumelenga kuzuia biashara ya Magendo ambayo imekuwa ikichangia zaidi kushuka kwa dhamani ya shilingi ya Tanzania na kukuza uchumi wa nchini jirani.

Alisema ushirikiano kati ya viongozi na wananchi utasaidia kupunguza kasi ya usafirishaji wa sukari nje ya nchi kwani sukari iliyopo ni nyingi na inaweza kuhudumia walaji wa  bidhaa hiyo bila matatizo na kwa bei elekezi   ya Serikali.

Gama alisema ili kuondoa tatizo la upatikanaji wa bidhaa hiyo ni lazima kuwabainisha watu waaminfu kupitia vijiji wanavyotoka ili waweze kupatiwa bidhaa hiyo na kuuza kwa wananchi kwa kiasi cha shilingi 1,900/- tu

Alifafanua kuwa viongozi wa vijiji wanatakiwa kuona uchungu na nchi yao na kuwa wazalendo kwa kuwachagua wafanyabiashara waaminifu watakao weza kutoa huduma bila upendeleo na kwa muda wote bila kuvusha bidhaa nje ya nchi
 

No comments: