Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (NEC-CCM) inamaliza kikao chake leo huko Dodoma.
Kikao hicho cha siku mbili ambacho kilitanguliwa na vikao vya Kamati Kuu (CC) kinamalizika huku vyombo vya habari mbalimbali vikiendelea kuibua labdalabda kuhusu hatma ya chama hicho ambacho kwa sasa ndicho kinachoongoza nchi.
Kwa hakika zimekua siku kadhaa za kurushana roho, kupandishana na kushushana presha lakini yote kwa yote inaonekana mambo ni magumu kuliko watu wanavyodhani.
Wapo watu ambao wanafikiria kwamba itakua jambo rahisi kwa CCM kuwatoa kafara watu wanaotajwa kwenye kashfa mbalimbali bila kusoma alama za nyakati, lakini wapo ambao wanaona kwamba kisiasa kufanya hivyo sio suluhisho.
Na kwa maneno ya Mwenyekiti wa CCM ambaye pia ni Rais wa Nchi, Jakaya Kikwete aliyoyatoa kwenye mkutano wa NEC jana kuwataka wajumbe wawe na amani na kuwaeleza kwamba CCM ni chama kikubwa na hakuna kitakacho haribika, ni ishara tosha kwamba hilo la ‘kuvuana magamba’ kwa minajili ya ‘kuwajibishana’ halitakuwepo.
Kinachoonekana hapa ni kwamba hata kama pilipili ni kali lakini bado inahitajika kuungia mboga.
No comments:
Post a Comment