MNYIKA |
TAARIFA KWA UMMA
Kurugenzi ya Mambo ya Nje na Mahusiano ya Kimataifa ya CHADEMA inatoa mwito kwa Rais Jakaya Kikwete kutumia mazungumzo kuhusu mahusiano baina ya Tanzania na Uingereza yanayotarajiwa kufanyika wakati wa ziara ya mtoto wa Mfalme wa Uingereza Charles na mkewe kuanzia tarehe 7 Novemba 2011 kushughulikia masuala yaliyojitokeza hivi karibuni yenye kuweza kuathiri mahusiano ya nchi zetu.
Katika siku za karibuni Serikali ya Uingereza imepunguza misaada yake ya kibajeti kwa Tanzania kwa asilimia 30 kutokana na kutoridhishwa na utendaji wa serikali hususani kuhusiana na masuala ya kuboresha mazingira ya kibiashara na kutoa fursa kwa wananchi kuwawajibisha viongozi. Uamuzi huo wa Serikali ya Uingereza umeelezwa kupitia barua ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Nchi hiyo Andrew Mitchell ya tarehe 3 Agosti 2011 kwenda kwa Mwenyekiti wa Kamati Teule ya Bunge la Nchi hiyo kuhusu Uchumi .
“Ni vizuri pande zote mbili Rais Kikwete na Mwanamfalme Charles wakawaeleza watanzania kuhusu sababu za ziada za maamuzi haya. Vyanzo mbalimbali vinaeleza kuwa sababu halisi ni washirika wa maendeleo kutoridhika na kasi ya vita dhidi ya ufisadi kwa upande mmoja na kwa upande mwingine ukanda wa ulaya (Eurozone) kukumbwa na matatizo ya kifedha”.
Aidha, Rais Kikwete atumie mazungumzo ya ziara hiyo kuwaeleza watanzania mkakati wa nchi kupunguza tatizo la utegemezi ambalo linasababisha nchi kupewa misaada yenye masharti ya kibeberu, ikiwemo kulieleza taifa namna ambavyo nakisi ya bajeti inayotokana na wahisani kupunguza fedha zao kwa Tanzania itaweza kuzibwa kwa kuongeza uzalishaji, mauzo ya nje na kupunguza ubadhirifu katika serikali.
Kwa upande mwingine, pamoja na kauli iliyotolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Mahusiano ya Kimataifa Benard Membe kuwa Tanzania iko tayari kukubali kukosa misaada yote toka Uingereza ikiwa serikali ya nchi hiyo italazimisha kutungwa kwa sheria ya kuruhusu ushoga, usagaji na ndoa ya jinsia moja; ni muhimu kwa Rais Kikwete kutumia mazungumzo hayo kufikisha ujumbe kamili wa kupinga masuala hayo kwa niaba ya watanzania.
Kurugenzi ya Mambo ya Nje na Mahusiano ya Kimataifa ya CHADEMA inaunga mkono msimamo wa serikali ya Tanzania wa kukataa kufanya mabadiliko ya sheria ya kuruhusu vitendo hivyo ambavyo ni kinyume cha sheria na utamaduni wetu.
“Kwa mujibu wa katiba ya CHADEMA kifungu 3.1.8, kwa falsafa yetu ya nguvu ya umma na itikadi ya mrengo wa kati CHADEMA inaweka umuhimu wa pekee katika familia kama moja ya taasisi muhimu za kijamii. Hivyo, tunapinga vitendo vya ushoga, usagaji na ndoa ya jinsia moja kwa kuwa vinakinzana na misingi ya maadili na uwepo wa familia”.
Kurugenzi ya Mambo ya Nje ya CHADEMA inataka ujumbe mahususi utolewe na Rais Kikwete kupitia ziara hiyo sababu wakati wa kujadiliwa kwa ripoti ya ndani ya mustakabali wa Jumuia ya Madola (Internal Report on the future relevance of Commonwealth) katika Mkutano wa Jumuia ya Madola uliomalizika karibuni; Rais Kikwete hakutoa ujumbe mkali kwa Serikali ya Uingereza wakati wa kujadiliwa kwa masuala ya haki za binadamu tofauti na kauli ambayo serikali iliitoa kupitia vyombo vya habari wakati ujumbe wake uliporejea Tanzania.
Wenu katika demokrasia na maendeleo,
John Mnyika (Mb)
Mkurugenzi wa Mambo ya Nje na Mahusiano ya Kimataifa (CHADEMA)
06/11/2011
No comments:
Post a Comment