Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe |
Wahenga walinena wakasema ‘Mwenda tezi na omo, marejeo ni ngamani”. Lakini pia wakatueleza ya kwamba “Mbio za sakafuni huishia ukingoni”.
Takriban kwa muda wa wiki nzima iliyopita tumeshuhudia mivutano mingi sana juu ya kile kilichojulikana kama mchakato, kuelekea katiba mpya ya Taifa letu.
Bungeni kuliwaka moto mara baada ya sehemu ya wabunge wa Kambi ya Upinzani (Chadema na NCCR-Mageuzi) kuukacha mjadala wa muswada wa katiba mpya ambao kwa sasa umepitishwa na unasubiria kusainiwa na Rais Jakaya Kikwete.
Viongozi wa asasi za kiraia nao hawakuwa nyuma katika kuonyesha kutoridhishwa kwao na mchakato mzima jinsi ulivyokwenda na wakatishia maandamano nchi nzima endapo mswada ungepita, tena wakasisitiza kwamba “HAKUNA WA KUTUZUIA”.
Haikupita muda Umoja wa VIjana wa CHADEMA nao wakatangaza maandamano nchi nzima kupinga kitendo cha Bunge kuendelea na mjadala ule ambao uliipitisha ile rasimu ya Katiba mpya.
Rais Jakaya Kikwete naye hakukaa kimya, akazungumza na wazee na kuelezea namna ambavyo yeye kama kiongozi wa nchi asivyoweza kuepukwa kwenye mchakato wa kuitafuta Katiba Mpya ya nchi na akatoa mfano wa nchi kadhaa.
Rais Kikwete alisema kwamba, kwa mfano nchi jirani ya Kenya ambayo kwa sasa inatumika kama mfano wa kuigwa ilihangaika kwa miaka 20 bila mafanikio, mpaka Rais Mwai Kibaki alipopewa jikumu lakuunda tume ya kukusanya maoni ndio ndoto za Wakenya zikatimia.
Pamoja na maelezo yote hayo ambayo Kikwete aliyatoa kwenya mazungumzo na wazee wa Dar es Salaam, bado Chadema wanaonekana kuwa na dukuduku ambalo jana baada ya kikao chao cha Kamati Kuu wamesema wanaomba kuonana na Rais Kikwete.
Suala kubwa la kujiuliza hapa ni kwamba ni kipi ambacho Chadema wanataka kumueleza Rais ambacho wameshindwa kuwaambia wananchi tena kwa kutumia forum yao kama wabunge pale Bungeni?
Kimsingi wapinzani katika taifa letu bado ni wachache Bungeni, uwepo wao ni kweli kwamba unaleta changamoto lakini, kukubali kwao au kutokukubali baadhi ya mambo hakuwezi kubadilisha chochote endapo wabunge wa CCM watapinga.
Ushahidi ni hotuba za bajeti mbalimbali ambazo wapinzani wamekuwa wakipinga lakini zinapita kilaini kwa kuwa wabunge wa CCM wanazipitisha na kwa zile zilizopita kwa shida, ilikuwa hivyo kwa sababu hata wa bunge wa CCM hawakukubaliana nazo.
Kwa hiyo hata hili la Katiba Mpya wapinzani wasijidanganye kwamba wanaweza kufanya mageuzi makubwa kwa misingi ya itikadi za vyama vyao, kinachotakiwa ni kuliendea suala hili katika sura ya utaifa zaidi.
Chadema wanaomba kuonana na Rais, halafu wanatishia kwamba asipowakubalia, wasilaumiwe. Haya maombi yanayoambatana na vitisho yanatija gani?
Katika taarifa zilizowahi kurushwa hewani na Blogu hii, ipo moja ambayo ilimnukuu, Prof Palamagamba Kabudi akisema kwamba “Sote tutaondoka lakini Tanzania itabakia” alikuwa akizungumza na wabunge juu ya mchakato wa kupata katiba mpya ambao ulihudhuriwa na wabunge wote wakiwemo wa Chadema.
Lakini mambo yanavyokwenda sasa inaonekana kana kwamba kuna ajenda ya siri ya wanasiasa katika mchakato huu.
Hata hivyo kama Chadema wanaamini kabisa kwamba mchakato umekosewa, kwanini wasielekeze nguvu zao kwa wananchi? Wawaelimishe ubaya wa mchakato huu halafu wao wapime na kama wataona kuna haja, basi watoe maoni yao wakati wa kukusanya maoni.
People’s power ni watu na demokrasia ni utawala wa watu, sio viongozi, na kwa hiyo watu ndio watakaoleta mabadiliko, lakini Rais Kikwete msimamo wake unaonekana kwamba anakubaliana na kilichotokea Bungeni na kwa vyovyote vile, inaonekana kabisa kwamba atausaini mswada huo ambao sasa upo mezani kwake.
No comments:
Post a Comment