Thursday, 6 October 2011

NAPE SWALI LA IGUNGA NI GUMU, USITOE MAJIBU MEPESI

Katibu wa Halmashari Kuu ya Taifa ya CCM (Itikadi na Uenezi) Bw Nape Nnauye
Chama cha Mapinduzi CCM kimeibuka na ushindi (sio wa kishindo) kwenye uchaguzi uliofanyika Jumapili ya wiki iliyopita huko Igunga na tayari kimetamba kwamba ushindi huo ni ishara ya kukubalika kwa mageuzi ndani ya chama.

Katibu wa Halmashari Kuu ya Taifa ya CCM (Itikadi na Uenezi) Bw Nape Nnauye alinukuliwa akisema kwamba ushindi wa Igunga na ushindi katika kata 77 ni ishara kwamba mabadiliko ndani ya chama yanakubalika.
Bendera ya CCM
Pengine Nape anasema ukweli kuhusu kata 77, lakini tukirudi Igunga kauli yake haina ukweli. Hii inatokana na ukweli kwamba nguvu ya CCM Igunga imepungua sana kwa matokeo ya uchaguzi huu.
Kweli ushindi ni ushindi, lakini kama alama ya chini ya kufaulu ni tano na wewe umezoea kupata kumi, siku ukipata saba huwezi kujisifu, utakachotakiwa kufanya nikukaa na kujiuliza juu ya alama tatu ulizopoteza kwa kua kuna uwezekano kwamba mtihani ujao zitapungua zaidi.
Kama Nape haoni tatizo Igunga basi anakataa tu lakini ukweli ni kwamba kitendo cha chama ambacho hakina historia inayoeleweka kwenye Jimbo la Igunga kuibuka wakati wa uchaguzi na kuvuna kura 23,360 dhidi ya kura 26,488 za CCM sio jambo la kujisifu.

Mbunge wa Igunga, Dk Dalaly Kafumu

Lazima ikumbukwe kwamba ni sera mpya za CCM na uongozi wa Nape ambao kwa kiasi kikubwa ulimfanya Rostam Aziz aliyekua mbunge wa Igunga kujiuzulu wadhifa wake, sasa ikiwa wananchi walifurahishwa na hatua hiyo mbona kura zimepungua kutoka zaidi ya elfu 30 mpaka 26 elfu?
Ukweli ni kwamba CCM imepunguza umaarufu wake Igunga kwa kiasi kikubwa na kama chama ipo haja ya kuweka nguvu zaidi kukijenga badala ya kubweteka na kujisifu wakati mtaji unaporomoka.

3 comments:

Anonymous said...

Kweli Nape asome alama za nyakati, atafakari juu ya Igunga. Nachofahamu mimi ni kwamba Igunga CCM imepoteza kura zaidi ya elfu kumi na Chadema wametoka sifuri mpaka elfu 23. Hizi za Chadema kwa vyovyote vile zimetokana na mpasuko ndani ya CCM, sasa iweje ajisifu?

Anonymous said...

Kwanza Nape alinusa tu Igunga, hakurudi tena, pengine alishajua kwamba uwepo wake kwenye kampeni za Igunga kungepelekea watu kupata chuki zaidi kwa kua yeye ndiye anayeonekana kama tatizo japo nia yake ni nzuri. Lakini nia nzuri lazima iwekwe wazi kwa wana CCM pia, kusiwe na kuogopana. Kweli Igunga inahitaji tafakari. Hongera CCM kwa ushindi.

Anonymous said...

WanaCCM tunajua kama viongozi wetu wa juu wana nia nzuri na chama, tunawaunga mkono. Tupo nyuma yenu. Kidumu Chama cha Mapinduz. Viva Nape.