Tuesday, 4 October 2011

Obama ni Rais wa Wayahudi?

Baada ya hotuba ya Rais Obama wa Marekani kwenye mkutano wa hivi majuzi wa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa (UN), baadhi ya wachambuzi wameshangazwa na tabia ya Rais huyo kuendelea kulinyenyekea Taifa la Israel.

Obama ni “Rais wa kwanza Marekani Myahudi?”. Hicho kilikua kichwa cha habari kwenye Jarida moja la Marekani-New York Magazine.   Kwa kumsikiliza Obama anaongea UN, wengi wangekubaliana na kichwa hicho cha habari.
Obama
Rais wa Marekani amekumbatia maamuzi ya Israeli kukataa kuunga mkono kutambuliwa na UN kwa Palestina kama taifa huru.

Hata hivyo baadhi ya wachambuzi wamesema, kukataa kuitambua Palestina sio msimamo wa Wayahudi wote au Wamarekani wote, lakini Obama amewashangaza wengi kwa kuonyesha unazi huo kwa Israel ambao unaelezwa kua unazidi hata ule aliokua nao, Rais Gorge Bush. 

Wachunguzi wa hali ya mambo wanasema Obama alisoma hotuba yake kana kwamba ni Baba wa Taifa la Israel na kwamba inaonekana kana kwamba hotuba ile iliandikiwa Israel naye akapewa tu asome.

Msimamo huo wa Obama unawastusha wengi haswa ikizingatiwa kwamba aliingia madarakani kwa kauli mbiu ya “change we can believe in”-akimaanisha “mabadiliko tunayoweza kuyaamini”.

Ni kutokana na kauli mbiu hiyo, Rais Obama alisema kwamba angependa kuyaona mataifa ya Kiarabu yakifurahia amani, lakini juzi amefanya kinyume.

Kiongozi wa Mamlaka ya Palestina, Mahmoud Abbas
Obama anadai kwamba Waarabu ndio wanaochochea vita kwa kuwachokoza Waisrael. Lakini historia inaonyesha kinyume chake, Israel ndio wachokozi, ndio waliochochea vita mwaka: 1956, 1967, 1982, 2006 na 2008. Vita ya mwaka 1973 peke yake ndiyo ilichochewa na Waarabu na hiyo ilikua ni baada ya Israel na Marekani kukataa mpango wa amani.

Kwanini Wapalestina wawe wahanga wa siasa za Marekani wakati wanashikiliwa mateka na Israeli kwa miongo sita sasa?

Msimamo wa Tanzania:

Rais Jakaya Kikwete alisema wazi kwenye mkutano huo wa UN kwamba Tanzania inaunga mkono jitihada za Palestina kutambuliwa na UN kama taifa huru.

Naye Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe alisema kwamba Wapalestina wanaishi kwenye ardhi yenye mabakamabaka kama ngozi ya chui kutokana na kutokua na mipaka inayoeleweka.

“Waisrael wamezungushia kuta maeoneo yote ambayo yanarasilimali na wanayaita kwamba ni nchi yao, Wapalestina wamebaki kutangatanga bila kujua hatima yao, tunataka nao wawe na uhuru na taifa lao,” alisema Membe.

Membe alionya kwamba msimamo wa Marekani huenda ukazua mgogoro wa kidiplomasia baina yake na mataifa mengine.


1 comment:

Anonymous said...

Uwepo wa Obama kama Rais haujaleta nafuu yoyote kwa mataifa masikini. Ukandamizaji wa siasa za Marekani umezidi sasa kuliko wakati mwingine wowote. Hakuna Change ni yaleyale tu.