Wednesday, 12 October 2011

WARIOBA: ACHENI KAMPENI ZA UCHAGUZI ZISIZO NA KIKOMO


Warioba

Waziri Mkuu Mstaafu, Jaji Joseph Warioba ameonya dhidi ya kampeni zisizoisha, akasisitiza kwamba chaguzi zimemalizika na huu ni wakati wa kuleta maendeleo bila kujali itikadi za vyama.
Amesema hayo leo jana Jijini Dar es Salaam mara baada ya kutembelea mabanda ya maonesho yaliyoandaliwa na Ofisi ya Waziri Mkuu kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara.
 Alisema vyama vya siasa havina budi kujifunza kushindanisha sera ili wananchi waweze kuchagua chama ambacho wanaona sera zake zinafaa na siyo kushindana kwa maneno tu.
 “Sasa hivi ukitazama magazeti ya kila siku, sote tunazungumzia siasa tupu… ni lazima tutambue kuwa tukimaliza uchaguzi, tunaingia katika shughuli za kuleta maendeleo, tujiepushe na kampeni za uchaguzi zisizoisha,” aliongeza.
 Alisema vyama vya siasa havina budi pia kuhakikisha kuwa vinaimarisha demokrasia nchini na ndani ya vyama vyenyewe na kuongeza kwamba: “Demokrasia ni pamoja na kutofautiana mawazo bila kupigana.”
 Alisema kama kuna suala linaisumbua nchi, kuna haja ya kukaa pamoja na kutafuta njia mbadala kwa maslahi ya Taifa. “Sisi na kundi jingine hatuna budi tukae pamoja na kujiuliza ni nini cha kufanya ili tusonge mbele... na hapa nataka kusisitiza kuwa kila awamu ilikuwa na matatizo yake, hakuna wakati ambapo nchi yetu haikuwa na matatizo lakini tulikaa pamoja na kutafuta ufumbuzi,” alisema.
 Akifafanua zaidi, Jaji Warioba alisema katika awamu ya kwanza kulikuwa na uasi wa jeshi, vita vya kumng’oa nduli Iddi Amin, kulikuwa na msukosuko wa kiuchumi baada ya kuvunjika kwa jumuiya ya Afrika Mashariki lakini yote yalitatuliwa na nchi ikasonga mbele.
 “Mimi nilipoingia madarakani (1985-1990) wakati wa awamu ya pili chini ya Mzee Ali Hassan Mwinyi, nchi haikuwa na bidhaa madukani kwa sababu tulikuwa hatuna fedha za kigeni za kutosha kuagiza bidhaa nje ya nchi; nchi ilikumbwa na baa la njaa lakini tulimaliza tatizo la njaa, tukazalisha kwa wingi zaidi mpaka ikabidi tuanze kujenga maghala kwa ajili ya kuhifadhi chakula cha ziada,” alisema.
 “Tulitumia umoja wa nchi yetu kutatua matatizo yaliyoikumba nchi na mara tatizo lilipotokea hatukunyoosha kidole kwa mtu mmoja… lilikuwa ni tatizo la wote.”
Alisisitiza haja ya kuilinda misingi ya umoja wa kitaifa na kutambua juhudi za kuleta maendeleo lakini akaongeza kuwa kuwa kuna haja ya kuangalia changamoto zinazojitokeza na kuainisha njia za kukabiliana nazo.
 (Kwa hisani ya PMO)

No comments: