Wednesday, 12 October 2011

WACHAGA WASHAURIWA KUHAMIA MIKOA MINGINE YENYE ARDHI KUBWA

  
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama (wa pili kushoto) akiwa na Mkuu wa wilaya ya Siha, Anna Nyamubi walipotembela Kambi ya “Ndarakwai Camp” katika hifafadhi ya msitu wa wanyamapori na mifugo wa North Kilimanjaro wilayani Siha. Wengine ni wataalam kutoka halmashauri ya wilaya ya Siha.

 Wananchi wa kijiji cha Ngarenairobi Wilaya Siha, Kilimanjaro  wameahidiwa kutafutiwa ardhi ya kilimo katika mikoa mingine endapo watakuwa tayari kuhama katika eneo la kijiji hicho kinachakabiliwa na uhaba wa ardhi ya makazi na kilimo.

Ahadi hiyo imetolewa jana na mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro Mheshimiwa Leonidas Gama alipotembelea kijiji hicho ikiwa ni sehemu ya ziara yake katika wilaya ya Siha yenye lengo la kuufahamu mkoa na kutaka kujionea mafanikio na changamoto zinazowakabili wananchi hasa wa vijijini katika mkoa wa Kilimanjaro.

Akijibu swali la mwanakijiji aliyejitambulisha kwa jina la Rashid salim ambaye alimuomba mkuu wa mkoa awasaidie waweze kuongezwa ardhi kutoka sehemu ya shamba la mradi wa ufugaji la  West Kilimanjaro lilinalomilikiwa na Shirika la Ranchi za Taifa  (NARCO) Mheshimiwa Gama amesema eneo hilo ni maaalum kwa ajili ya wanyama na endapo wataona ardhi waliyopewa kwa ajili ya makazi haitawatosha ni vema wengine wakapungua kwa kutafuta ardhi katika mikoa mingine ambayo bado ina ardhi ya kutosha.

Halmashauri ya wilaya ya Siha tayari imeshaanza mchakato wa kuirasimisha sehemu ya ardhi waliyopewa wanakijiji hao kwa ajili ya makazi lakini ardhi hiyo haitatosha kwa shughuli za kilimo kutokana na ufinyu wa ardhi hiyo.

Aidha Gama amewaeleza kuwa eneo hilo ni sehemu ya mapitio ya wanyama pori wanaotokea katika hifadhi za nchi jirani ya Kenya na kuingia katika hifadhi ya wanyama pori ya Arusha na kuwaelimisha kuwa kuna sheria zinazowalinda wanyama pori wanapokuwa katika shughuli zao na kijitafutia chakula na maji kwa mujibu wa mahitaji yao.

Kuhusu Magendo ya Sukari na Nafaka.

Kuhusu tatizo la uvushwaji wa nafaka na sukari kwa njia za magendo Mheshimiwa Gama amewataka wananchi hao ambao wanaishi jirani mpaka wa Tanzania na nchi jirani ya Kenya kutoa taafa kwa vyombo husika na zawadi itatolewa kwa mwananchi yeyote atayefanikisha kukamatwa kwa shehena ya magendo katika eneo hilo.

Mbali hilo aliwaahidi wanakijiji hao kuwa endapo watafanikiwa kutoa taarifa hizo na mzigo wa magendo kukamatwa  chakula hicho kitauzwa kwa bei nafuu kwa wananchi wa kijiji hicho ili wanufaike na uzalendo wao.

(Kwa hisani ya Mdau, Shaaban wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Kilimanjaro)


No comments: