Tambo, mbwembwe na vurugu za kampeni zinafikia mwisho leo huko Igunga, uchaguzi umewadia, ambapo kesho wapiga kura wa Jimbo hilo watafanya maamuzi juu ya wanayemtaka awe Mbunge wao.
Wagombea walikua nane, lakini dakika tisini za mchezo zilitawaliwa na wagombea watatu kutoka vyama vya CCM, Chadema na CUF.
Hata hivyo kupitia yale yaliyokua yakiripotiwa kwenye vyombo vya habari, kampeni za Igunga zilitawaliwa na visa na vituko zaidi kuliko sera za wagombea.
Lakini, yote kwa yote wapo wagombea waliotoa ahadi japo kwa uchache na wapo waliotangaza sera zao japo kwa uchache.Hapo kwenye ahadi na sera ndipo wapigakura wanapopaswa kuegemeza maamuzi yao.
Matatizo ya Igunga yanafahamika, ambayo ni pamoja na;
- Maji
- Daraja la Mbutu
- Ukame (unaopelekea njaa mara kwa mara)
- Rasilimali za madini ambazo wenyeji wanadai hawafaidi vya kutosha
- Shule hazina waalimu wa kutosha
- Huduma hafifu za afya, na
- Miundombinu duni.
Maamuzi yawe ya kimantiki zaidi, maamuzi yanayotokana na uchambuzi wa sera za wagombea na uwezo wao wa kusukuma mbele gurudumu la maendeleo ya Jimbo la Igunga.
Wapigakura waache jazba, waache ushabiki, wasiongozwe na ushawishi wa rushwa, wawe watulivu na wajitokeze kwa wingi kumchagua Mbunge wao.
Kila la heri Igunga.
No comments:
Post a Comment