Saturday, 1 October 2011

Kipande cha Hotuba ya Rais Jakaya Kikwete kuhusu Igunga.

Rais Jakaya Kikwete

Uchaguzi wa Igunga
Ndugu Wananchi;
Kama mnavyofahamu siku ya Jumapili tarehe 2 Oktoba, 2011 ndugu zetu wa Jimbo la Igunga, Mkoani Tabora watapiga kura kuchagua Mbunge katika uchaguzi mdogo.  Napenda kutumia fursa hii kuwatakia wananchi wa Igunga uchaguzi mwema na kuwaomba siku hiyo wajitokeze kwa wingi kutumia haki yao ya kikatiba ya kumchagua mtu wanayemtaka kuwa Mbunge wao kwa kupiga kura.  Haitakuwa sawa hata kidogo kama ndugu zetu wa Igunga wataacha kutimiza wajibu wao huo wa msingi kama raia. 
Ndugu Wananchi;
 Ningependa kuwahakikishia kwamba Serikali imejiandaa vya kutosha kutimiza ipasavyo wajibu wake wa ulinzi na usalama kwa wananchi wa Igunga katika kipindi hiki cha uchaguzi.  Hivyo wananchi wajitokeze kwa wingi kupiga kura bila wasiwasi wowote.  Usalama utakuwa wa uhakika katika vituo vyote na kamwe hatavumiliwa mtu yeyote atakayefanya au hata kujaribu kufanya vitendo vya uvunjifu wa amani, vurugu au fujo.  Hatukubali siku ya kupiga kura iwe ni siku ya watu kujifungia ndani au kuogopa kutoka nje.  Nawahakikishia hilo halitatokea huko Igunga.  Na wanaodhani kuwa tunatania wathubutu, watadhibitiwa ipasavyo.
Nawasihi, wananchi wa Igunga kuendelea kudumisha amani, kabla ya uchaguzi, wakati wa uchaguzi na baada ya matokeo kutangazwa.  Nawaomba msikubali wanasiasa wawageuze chambo cha kuendeleza maslahi yao binafsi ya kisiasa na tamaa zao za madaraka zilizovuka mipaka.  Amani ya nchi yetu ni tunu adhimu ya taifa letu tuliyoirithi kutoka kwa waasisi wa taifa letu Baba wa Taifa hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na hayati Mzee Abeid Amani Karume.  Tumeapa kuidumisha na kuiendeleza na tumefanya hivyo kwa mafanikio hadi hivi sasa. 
Ndugu zangu, Watanzania Wenzangu;
 Tume ya Taifa ya Uchaguzi imeshawahakikishia wapiga kura wa Igunga kwamba maandalizi yote yamekamilika na shughuli za uchaguzi kule Igunga zitakwenda kama inavyotarajiwa.  Wamesema vifaa vyote tayari vimesambazwa katika Kata zote, Wasimamizi wa Vituo na Mawakala wa vyama wamekamilika.  Kwa jinsi Tume ya Uchaguzi ilivyojipanga,  ninayo imani kuwa mchakato mzima wa uchaguzi utakwenda vizuri.    
Ni matumaini yangu kwamba Tume itaendelea kuwaelimisha wananchi taratibu za kufuata ili wananchi washiriki kwa ukamilifu katika kutimiza haki yao ya kikatiba.  Ningependa kuona kuwa kila mtu aliyejiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura anapata fursa ya kupiga kura kwa uhuru na bila bugudha yoyote.  Nawatakia uchaguzi mwema.
Mungu Ibariki Afrika!
Mungu Ibariki Tanzania!
Asanteni kwa Kunisikiliza.

No comments: