Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama amepiga marufuku uegeshwaji wa malori yaliyobeba bidhaa za nafakaka yakiwemo mahindi pamoja na sukari katika eneo la mji mdogo wa Himo katika wilaya ya Rombo Mkoani Kilimanjaro ili kudhibiti utoroshaji wa bidhaa hizo kwenda nchi jirani ya Kenya.
Gama amesema hayo katika kikao chake na watumishi wa halmashauri ya wilaya ya Rombo alipofanya ziara ya kikazi katika halmashauri ikiwa ni sehemu ya ziara zake alizojiwekea katika kujua changamoto zinazowakabili wananchi na kupanga vipaumbele vya kimaendeleo katika kuwawezesha wananchi kujiletea maendeleo.
Katika utekelezaji wa agizo hilo Gama amewataka watumishi wote wa umma kuwa waadilifu na waaminifu kwa serikali ili kukomesha kabisa biashara za magendo katika mkoa wa Kilimanjaro hasa katika mipaka na nchi jirani ya Kenya.
Kuhusu suala la utii wa sheria Gama ameonya tabia ya baadhi ya wananchi na wafanyabiashara kudharau na kukaidi amri halali za mamlaka na viongzi wa nchi ambazo zitambulika kisheria kuwa hatakuwa tayari kuwafumbia macho na kuwaonea aibu watu wenye tabia hizo.
Aidha Mkuu huyo mpya wa mkoa aliwakumbusha watumishi wote wa umma kuwa majukumu ya watumishi wa umma ni kusaidia kupatikana kwa maendeleo ya wananchi na hivyo basi hawana hiyari katika kuhakikisha kuwa wanakuwa waadirifu kwa kutumia vizuri ofisi za serikali kwa kuwepo katika maeneo ya kazi katika nyakati za kazi, hawapokei wala kutoa rushwa pamoja na kutimiza wajibu kwa wakati.
Bwana Gama amesema kuwa tuhuma za kushiriki biashara za magendo kwa watumishi wa umma ni moja ya mambo yanayomkera na ni ya aibu kwa serikali na hatakuwa tayari kuvumilia uovu huo katika mkoa wa anaouongoza. “ Nikilazimika kumuondoa mtu katika nafasi ya kiutumishi aliyonayo nitafanya hivyo” alisisitiza.
No comments:
Post a Comment