Lowassa |
‘Anazungumza leo’ , ‘anazungumza leo’, ‘atasema ya moyoni’. Kila mtu alitamani kusikia kile ambacho mmoja wa wanasiasa wa siku nyingi wa nchi hii aliyepata kuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa angekizungumza kwenye mkutano wake na waandishi wa habari leo.
Kimsingi, Lowassa amezungumza hayo aliyoyazungumza na kwa wale tuliopata hotuba yake, tukaisoma kwa kina tumeona kwamba kwa kiasi kikubwa ameangazia siasa za kupakana matope na jinsi asivyohusika na baadhi ya tuhuma zinazoelekezwa dhidi yake.
Bila shaka aliyoyazungumza Lowassa yalikuwa yanategemewa na wengi lakini pia kwa kiasi fulani amewaacha Watanzania na kiu, kiu ya kutaka kujua zaidi kuhusu shutuma mbalimbali ambazo anatuhumiwa kwazo.
Mwenyewe amekiri kwenye hutuba yake kwamba vyombo vya habari vimemchafua sana na bila shaka amelizungumzia hili akiwa anajua kwamba kwa kuchafuliwa huko wapo watu ambao tayari wanamuona ni mchafu.
Ingawa amezungumzia nia yake ya kuchukua hatua za kisheria ili umma ujue ukweli, tatizo hapa ni muda kwa kuwa milolongo ya kisheria inachukua muda mrefu na pengine angejitahidi kugusa kila eneo ambalo amechafuliwa angalau kwa minajili ya kuweka mambo sawa wakati sheria inasubiriwa kuchukua mkondo wake.
Kwa kujibu baadhi ya shutuma Lowassa hakuwatendea haki Watanzania waliokua na shahuku ya kujua msimamo wake juu ya shutuma zote zinazotolewa kupitia vyombo vya habari haswa ikizingatiwa kwamba watu wengi wanaamini yale wanayoyasikia kwenye vyombo hivyo.
Ilitarajiwa pia kwamba atayazungumzia yote anayoshutumiwa kwayo kama alivyokanusha shutuma juu ya;
1. Kuchochea fujo kwenye siasa za UVCCM Arusha
2. Shutuma kwamba anauhusiano mbaya na Rais Jakaya Kikwete, na
3. Tuhuma kwamba alitaka kugombea Urais mwaka jana.
Lowassa hakuzungumzia kabisa tuhuma kwamba anachochea siasa za makundi ndani ya CCM kwa lengo la kutaka kugombea Urais 2015. Pengine wapo watu ambao wangependa kujua msimamo wa mwanasiasa huyu juu ya tuhuma hizo.
Je, Lowassa anaona mantiki gani kwa watu kudhani kwamba mtu kama yeye ambaye kwenye hutuba yake amejieleza kama mwanaCCM mwadilifu na aliyelelewa na chama, hastahiki kua na nia ya kugombea nafasi ya juu ya uongozi wa nchi hii?
Yote kwa yote, Lowassa amevunja ukimya, japo kwa uchache, lakini angalau amezungumza.
No comments:
Post a Comment