Monday, 3 October 2011

Nani kala mtaji wa CUF Igunga?

Uchaguzi wa Igunga umemalizika, CCM wamevuna neema, Chadema wamevuna matumaini, CUF wamevuna aibu. Swali kubwa la kujiuliza hapa, “Nani kala mtaji wa CUF?”.

Ikumbukwe kwamba vyama vyote vilivyokwenda Igunga vilikwenda kutafuta kura, lakini tofauti na wengine CUF wao walidai kwamba hata kabla ya kampeni walikua na mtaji wao wa kura 11,000.

Siku za mwanzo kabisa, Naibu Katibu Mkuu wa CUF (Bara), Julius Mtatiro alinukuliwa akisema kwamba Chadema hawana nia ya dhati ya kujenga upinzani imara nchini, akadai kwamba wao (CUF) ndio wenye nguvu Igunga na Chadema walitakiwa wawaunge mkono ili wachukue jimbo.
Mbunge wa Igunga, Dk Dalaly Kafumu

Wakati akiyasema haya, Mtatiro pengine hakua akifahamu vizuri hali halisi ya Igunga, Igunga kulikua na mambo mawili: Kwanza Chadema hawakua na mgombea kwenye uchaguzi mkuu mwaka jana. Pili kura 11,000 za CUF zilitokana na Wanachadema walioungana kumpigia mgombea wa CUF.

Ukweli huu unajidhihirisha pale ambapo, Dr Slaa ambaye hakupita kabisa Igunga kwenye kampeni za Urais, alipata kura 8,000 wakati CUF ambacho kilikua na mgombea wa Ubunge, Mgombea wake wa Urais, Prof Ibrahim Lipumba alipata kura 3,000 tu.

Kwa matokeo kama haya, CUF hawakutakiwa kwenda Igunga kifua mbele, walitakiwa kujua kwamba mtu aliyepata kura 8,000 bila kampeni, akifanya kampeni chama chake kitapata kura nyingi zaidi, na hilo ndilo lililotokea.

Mtatiro

Kwa hali ilivyojitokeza, pengine CUF ndio walipaswa kuwaachia wenzao Jimbo, ili wasigawe kura lakini ndio hivyo wameshalikoroga.

Hata hivyo, Mtatiro alidai kwamba kamwe hawatakiunga Chadema mkono sehemu yeyote hata kama kina nguvu, akadai kwamba msimamo huo wa CUF unatokana na ukweli kwamba Chadema wao hawaamini katika kusaidiana.

“Mwaka jana niligombea Ubungo, nilikua najua kabisa kwamba Chadema wananguvu, lakini singeweza kuwaachia kwa kuwa hata wao hawajawahi kutuachia maeneo ambayo tunanguvu kama hapa Igunga,” alisema mwanasiasa huyo ambaye mwaka jana aligombea Ubunge kwenye Jimbo la Ubungo.

Hata hivyo, baada ya matokeo kutangazwa Igunga, Mtatiro na aliyekua mgombea wa CUF, Leopold Mahona wamelalamika kwamba kampeni za Igunga zilitawaliwa na kumwaga fedha.

Lakini hawakueleza kiundani, ikiwa hiyo ndiyo sababu pekee iliyowafanya wafanye vibaya kiasi hicho pamoja na kutumia helikopta kwa mara ya kwanza katika historia ya chama hicho.

Ismail Jussa ambaye ni Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi kwa tiketi ya CUF na ambaye alikua Igunga ameandika kwenye mtandao wa kijamii wa Facebook akisema watakaa kama chama watafakari ya Igunga.

Jussa
“Tumefanya kila lililo kwenye uwezo wetu kuendesha kampeni Igunga na tuliamini tutafanya vizuri. Wapiga kura wa Igunga wameamua vinginevyo. Tunayaheshimu maamuzi yao hata kama hayatufurahishi.

Ndiyo matakwa ya demokrasia! Kama Chama, tutakaa na kufanya tathmini na kisha kuchukua hatua zinazofaa katika kukirejesha kwenye chati” amesema Jussa.

Katika uchaguzi huo, Mgombea wa CCM, Dk Dalaly Peter Kafumu ameshinda kwa kura 26,488, akifuatiwa kwa karibu na Mgombea wa Chadema, Joseph Kashindye aliyepata kura 23,360 na Mahona wa CUF ameambulia kura 2,104.

Ni katika uchaguzi ambao Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imesema watu wachache sana walijitokeza kupiga kura, ni watu 53,672 tu, kati ya 171,077 waliojiandikisha.


No comments: