Wednesday, 26 October 2011

TUKITIMIZA WAJIBU AJALI ZITAKOMA

Basi la Delux likiteketea
Jamii yetu inazongwa na mabalaa mengi, hili la ajali za barabarani linaonekana kukua siku hadi siku. Jana tumepoteza wenzetu zaidi ya kumi kwenye ajali ya basi la Delux Coach iliyotokea huko Misugusugu, Pwani.
Mwendo kasi umezoeleka kua ndio chanzo kikukuu cha ajali nyingi hapa nchini, lakini ajali hii inasemekana ilitokana na kupasuka kwa gurudumu, ikapinduka na kisha ikalipuka.
Katika salamu zake za rambirambi kwa Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Rais Jakaya Kikwete amesema ajali zitaendelea kama polisi na wanajamii hawatashirikiana kuhakikisha usalama wa vyombo vya usafiri unakuwepo.
Kwa wale tuliowahi kusafiri kwa mabasi, tunajua abiria ndio wanakuwa vinara wa kuchochea mwendo kasi kwa madereva, dereva anayetembea taratibu anakua adui wa abiria, lakini ole wake dereva itokee ajali, lawama zote zinamuelekea yeye.
“Dereva alikua anatembea kwa mwendo wa kasi sana” ndio yamekuwa maelezo ya abiria zinapotokea ajali. Lakini utajiuliza kwanini hakupiga simu polisi? Jibu lake ni kwamba alikuwa akifurahia mwendo ule, lakini kwa kuwa ajali imetokea anambebesha lawama dereva.
Kwa hili la kupasuka kwa gurudumu, polisi hawawezi kukwepa lawama, wao ndio wanayakagua magari na kuyaruhusu yaendelee na safari, wakati mwingine wakijua kabiasa kwamba magari hayo yanakasoro kadhaa za kiufundi.
Kwa mfano gurudumu kipara linaonekana tu kwa macho, wala halihitaji utaalamu wowote kugundua, lakini kwa nini mabasi yanaachwa yatembelee matairi mabovu? Je ni nguvu ya rushwa au ni upofu wa askari wa usalama barabarani?
Tanzania bila ajali inawezekana, kila mmoja achukua hatua.

KIKWETE AMTAKIA KILA LA HERI CHANDE ICC

Tanzania itapata heshima kubwa iwapo Jaji Mkuu Mheshimiwa Mohammed  Chande  Othman atachaguliwa kuwa muongoza Mashtaka Mkuu wa Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya  Jinai,  maarufu kama  International Criminal Court (ICC),  yenye makao yake makuu mjini Haque, Nertherlands baada ya kumalizika kwa muda wa Jaji Jose Luis Moreno Ocampo anayemaliza muda wake.
Jina la jaji Othman ni moja kati ya majina manne yaliyopendekezwa na Kamati Maalum inayoundwa na mabalozi.  Nafasi hii huwa haiombwi bali Kamati Maalum hukaa na kupendekeza majina ambayo hupitia mchujo ndani ya kamati hiyo na hatimaye kupata jina moja.
Wengine waliopendekezwa ni kutoka Gambia, Uingereza na Uhispania.
Kama Jaji Mkuu atapata nafasi hii, atakuwa ametumikia serikali kwa muda mfupi sana baada ya kuteuliwa na Rais Jakaya Mrisho Kikwete kushika wadhifa huo serikalini.
Hata hivyo, Rais anaona jambo hili ni jema, si kwa Mheshimiwa Chande tu, bali hata kwa nchi ya Tanzania, na anaona hili ni jambo  jema na ambalo litailetea sifa nyingi na kuiweka Tanzania katika ramani ya mambo makubwa na muhimu yenye dhamana kubwa ulimwenguni.
Rais anamtakia Jaji Othman  Heri  na  akifanikiwa kupata nafasi hiyo, Rais atakubaliana na uteuzi huo na itambidi ateue Jaji Mkuu mwingine kutokana na majaji wengi tulio nao Tanzania.
Jaji Mkuu Othman ameshika wadhifa wa Jaji Mkuu wa Tanzania kuanzia tarehe 28 Disemba, 2010 baada ya kustaafu kwa mujibu wa sheria kwa Jaji Augustino Ramadhani aliyestaafu tarehe 27 Disemba, 2010.
Jaji Othman amekuwa Jaji wa Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufaa kwa muda wa miaka saba, amekuwa  mtaalamu binafsi juu ya hali ya Haki za Binadamu huko Sudan Kusini hadi mwezi August, 2011.
Jaji Othman amezaliwa tarehe 1Januari, 1952, ana shahada ya kwanza ya Sheria kutoka Chuo Kikuu cha Dar-Es-Salaam na Shahada ya Uzamili kutoka Chuo Kikuu cha Webster, Geneva-Uswis.
Pia amewahi kuwa Mwendesha Mashtaka wa Mahakama ya Rwanda huko Arusha na pia kawahi kushika nafasi sawa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali huko Timor Mashariki.
Mwisho.
Imetolewa na Premi Kibanga,
Mwandishi wa Habari wa Rais  Msaidizi,
Ikulu.
Dar es Salaam.
26 Oktoba, 2011

Monday, 24 October 2011

KIKWETE KUHUDHURIA MKUTANO AUSTRALIA

Rais Jakaya Kikwete ameondoka nchini jioni hii kuelekea Perth, Australia kuhudhuria Kikao cha Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Madola kinachofanyika kuanzia tarehe 28-30 mwezi huu.




Kabla ya Mkutano Mkuu kuanza, tarehe 25 Oktoba, kutakuwa  na vikao  kadhaa kikiwemo kikao cha wafanyabiashara ambacho Rais Kikwete anatarajiwa kutoa hotuba ya ufunguzi  na baadaye kujumuika na viongozi kadhaa wa  nchi  chache katika kikao maalum na  wafanyabiashara.




Kwa mujibu wa taarifa ya Kurugenzi ya Mawasliano Ikulu iliyotolewa leo, Rais anatarajiwa kurejea nchini tarehe 3 Novemba, 2011.

CASTRO: NATO NI JESHI LA KINYAMA

Castro
Rais wa Zamani wa Cuba, Fidel Castro emewakosoa vikosi vya NATO kwa kuvamia na kisha kumuondoa madarakani na kupelekea kuuwawa kwa Kiongozi wa Libya Muammar Gaddafi.

Bwana Castro amesema “Ukatili wa kijeshi uliofanywa na NATO unaonesha kwamba jeshi hilo ni la hatari kuliko yote taliyopata kutokea katika historia ya binadamu”.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, Castro (85) ameelezea kuuliwa kwa Gaddafi wiki iliyopita na jinsi mwili wake ulivyozalilishwa  kama “ni kitendo cha kuzalilisha na ambacho kinavunja misingi ya dini ya Uislamu na imani nyingine”.

Msimamo wa Castro umekuwa hasi tangu mwanzo kabisa wa uvamizi wa NATO na amekuwa akimsifu Gaddafi kwa kuonyesha ushujaa.

Mwenzi uliopita, serikali ya Cuba iliondoa maafisa wa Ubalozi wake Libya na kusema kwamba kwamwe haitatambua uongozi wa nchi hiyo utakaowekwa kwa msaada wa nchi za Magharibi.

DK SHEIN AAPISHWA, AHUDHURIA KIKAO CHA BARAZA. RAIS KIKWETE APOKEA HATI ZA UTAMBULISHO WA MABALOZI WAPYA WA SUDANI NA JAPAN IKULU LEO.

Rais Jakaya Kikwete (kushoto) akishuhudia Jaji Mkuu, Mohamed Chande Othuman  akimwapisha Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohammed Shein kuwa mjumbe wa Baraza la Mawaziri.
Baada ya Kuapishwa kilifuata kikao cha Baraza la Mawaziri
Rais Jakaya Kikwete (kushoto) akipokea hati za utambulisho kutoka kwa Balozi Mpaya wa Sudan,   Yassir Mohamed Ali.
Rais Jakaya Kikwete (kulia) akizungumza na Balozi Mpya wa Japan, Masaki Okada muda mfupi baada ya balozi huyo kukabidhi hati za utambulisho Ikulu leo.

Sunday, 23 October 2011

TUNISIA WANAFANYA UCHAGUZI WA KIDEMOKRASIA KWA MARA YA KWANZA TANGU VUGUVUGU LA MABADILIKO LIZIKUMBE NCHI ZA KASKAZINI MWA AFRIKA


PEOPLE'S POWER NA WATU KIBAO

Waandamanaji wanaopinga Serikali ya Yemeni  wakiwa katiaka swala ya Ijumaa juzi.

ZAMU YA MAREKANI SASA

Harakati za kupinga matumizi mabaya ya madaraka na rushwa zinazoambatana na maandamano makubwa maarufu kwa jina la “Occupy Wall Street“  zimepamba moto huko Marekani ambako kutoka Wall Street, New York, tayari  zimeenea kwenye miji 847.
Maandamano na harakati hizo zimeanza wiki nne zilizopita bila kupumzika mpaka sasa. Hali inayoelezewa kuwa ni tete na pengine inaonekana kua ni sawa kabisa na ile ya nchi za Kiarabu za Africa maarufu kama ‘Arab Spring’.

Wataalamu wa masuala ya uchumi pia wameelezea kwamba wananchi wengi wa Marekani wamechoshwa na hali mbaya ya kiuchumi na wanaulalamikia utawala wa Rais Barack Obama kwa kushindwa kutekeleza ahadi zake kwa wananchi.

Kwa mujibu wa taarifa za vyombo mbalimbali vya habari, huko Chicago polisi wamewakamata raia 100 baada ya kugoma kutii amri wakati wa muendelezo wa maandamano hayo. ANGALIA PICHA ZIFUATAZO....



 












Wednesday, 19 October 2011

JAPO KWA UCHACHE, LOWASSA AMEVUNJA UKIMYA

Lowassa
‘Anazungumza leo’ , ‘anazungumza leo’, ‘atasema ya moyoni’. Kila mtu alitamani kusikia kile ambacho mmoja wa wanasiasa wa siku nyingi wa nchi hii aliyepata kuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa angekizungumza kwenye mkutano wake na waandishi wa habari leo.
Kimsingi, Lowassa amezungumza hayo aliyoyazungumza na kwa wale tuliopata hotuba yake, tukaisoma kwa kina tumeona kwamba kwa kiasi kikubwa ameangazia siasa za kupakana matope na jinsi asivyohusika na baadhi ya tuhuma zinazoelekezwa dhidi yake.
Bila shaka aliyoyazungumza Lowassa yalikuwa yanategemewa na wengi lakini pia kwa kiasi fulani amewaacha Watanzania na kiu, kiu ya kutaka kujua zaidi kuhusu shutuma mbalimbali ambazo anatuhumiwa kwazo.
Mwenyewe amekiri kwenye hutuba yake kwamba vyombo vya habari vimemchafua sana na bila shaka amelizungumzia hili akiwa anajua kwamba kwa kuchafuliwa huko wapo watu ambao tayari wanamuona ni mchafu.
Ingawa amezungumzia nia yake ya kuchukua hatua za kisheria ili umma ujue ukweli, tatizo hapa ni muda kwa kuwa milolongo ya kisheria inachukua muda mrefu na pengine angejitahidi kugusa kila eneo ambalo amechafuliwa angalau kwa minajili ya kuweka mambo sawa wakati sheria inasubiriwa kuchukua mkondo wake.
Kwa kujibu baadhi ya shutuma Lowassa hakuwatendea haki Watanzania waliokua na shahuku ya kujua msimamo wake juu ya shutuma zote zinazotolewa kupitia vyombo vya habari haswa ikizingatiwa kwamba watu wengi wanaamini yale wanayoyasikia kwenye vyombo hivyo.
Ilitarajiwa pia kwamba atayazungumzia yote anayoshutumiwa kwayo kama alivyokanusha shutuma juu ya;
1.      Kuchochea fujo kwenye siasa za UVCCM Arusha
2.      Shutuma kwamba anauhusiano mbaya na Rais Jakaya Kikwete, na
3.      Tuhuma kwamba alitaka kugombea Urais mwaka jana.
Lowassa hakuzungumzia kabisa tuhuma kwamba anachochea siasa za makundi ndani ya CCM kwa lengo la kutaka kugombea Urais 2015. Pengine wapo watu ambao wangependa kujua msimamo wa mwanasiasa huyu juu ya tuhuma hizo.
Je, Lowassa anaona mantiki gani kwa watu kudhani kwamba mtu kama yeye ambaye kwenye hutuba yake amejieleza kama mwanaCCM mwadilifu na aliyelelewa na chama, hastahiki kua na nia ya kugombea nafasi ya juu ya uongozi wa nchi hii?
Yote kwa yote, Lowassa amevunja ukimya, japo kwa uchache, lakini angalau amezungumza.


LEO NI LOWASSA

Lowassa
Waziri Mkuu aliyejiuzulu mwaka 2007, Edward Lowassa leo atazungumza na waandishi wa habari. 

Tayari wachunguzi mbalimbali wa hali ya mambo wamesema Lowassa huenda akatumia nafasi hiyo kujibu tuhuma mbalimbali ambazo zimekua zikielekezwa kwake tangu alipojiuzulu mpaka leo. 

Mwanasiasa huyo mkongwe ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Munduli  (CCM) yasemekana mkutano wake utazungumzia mambo makuu matatu likiwamo suala la Kampuni ya kufua umeme ya Richmond ambalo lilisababisha ajiuzulu wadhifa huo.


Suala jingine ambalo linatarajiwa kuzungumzwa na kiongozi huyo ni kuhusu mgogoro ndani ya CCM mkoani Arusha na hatma yake kisiasa.

SIASA ZA ARUSHA NA SURA MBILI ZA POLISI

Millya
Siasa za Arusha Mjini zinazidi kua tete kadri siku zinavyokwenda. Kumeshuhudiwa matukio mengi ya ghasia za kisiasa tangu ulipomalizika uchaguzi mkuu wa mwaka jana uliompa ushidi mgombea kwa tiketi ya Chadema, Bw Godless Lema.


Suala la uchaguzi wa Meya wa jiji hilo lilipelekea kumwagika kwa damu baada ya kile kilichodaiwa kua ni maandamano haramu yaliyofanywa na Chadema kuonesha hisia zao za kuupinga uchaguzi wa Meya kwa madai kwamba Chadema hawakushiriki.


Hata hivyo mwisho wa siku Chadema waligeukana wenyewe kwa wenyewe mara baada ya madiwani wake kukubaliana kuingia kataika maridhiano na CCM juu ya uongozi wa Halmashauri. Msimamao ambao ulipelekea uongozi wa juu wa Chama hicho kuwatimua madiwani wake.


Baada ya kimbunga hicho cha Chadema, juzi yameibuka mengine mapya kabisa, ambapo kundi la wafuasi wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) kutoka wilaya mbalimbali za Mkoa wa Arusha lilizingira Makao Makuu ya Polisi Mkoa ambako mwenyekiti wao, James Millya alikwenda kujisalimisha.


Licha ya shamrashamra, hamasa  na  kuimba wakati wakiwa nje ya makao hayo ya polisi, vijana hao walimsindikiza kwa maandamano mwenyekiti wao hadi kwenye ofisi za chama chao mara baada ya kutoka kwenye mahojiano hayo ambayo yaliripotiwa kuchukua takribani dakika 15.


Swali kubwa la kujiuliza hapa; Kwanini wafuasi hawa waliachiwa wafanye hayo waliyoyafanya bila kutawanywa na polisi?  


Mambo kama haya yanajenga tabaka baiana ya wafuasi wa vyama vya siasa kwa kuwa polisi wamekuwa wakiyatawanya maandamano ambayo hayana baraka zake au mikusanyiko ambayo haina kibali cha polisi.

Tuesday, 18 October 2011

NAPE: TOFAUTI KUBWA YA KIPATO NI HATARI KWA AMANI YA NCHI

Nape
Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi wa CCM Ndg. Nape Nnauye amesema ipo haja sasa kujadili kwa kina namna ya kupunguza tofauti kubwa ya kipato iliyopo kati ya masikini na matajiri kwani ni hatari kwa amani ya nchi.

Nape ameyasema hayo kwenye viwanja vya sokoni Igoma jijini Mwanza wakati akihutubia mkutano mkubwa wa hadhara ulioandaliwa na Chama hicho katika ziara ya baadhi ya viongozi wa Chama hicho mkoani Mwanza.
Nape alisema nchi nyingi duniani machafuko tunayoyaona ni matokeo ya kuachiwa kukua kwa tofauti kubwa ya kipato iliyopo kati ya masikini ambao ndio wengi kwa idadi na matajiri ambao kwakweli ni wachache.
" ukiona mwenzio ananyolewa wewe tia maji!.. Heri kuziba ufa kuliko kujenga ukuta. Ni muhimu leo wapenda amani wa nchi hii tujadili kwa kina namna bora ya kupunguza tofauti kubwa ya kipato nchini kwani ikiachwa hivi baada ya muda nchi hii itachafuka" alisema Nape.

Aliwageukia vijana na kusema kuwa ikiwa vijana ambao ndio wenye nguvu kucha kuchwa wanabakia kulumbana juu ya siasa tu vijiweni bila kutafakari na kujituma kupunguza tofauti hii kubwa ya kipato kati ya masikini na matajiri nchini, wao ndio waathirika wakubwa kwani wataishi leo na kesho.

Alisisitiza kuwa Tanzania sio masikini kwa rasilimali ilizonazo lakini mara kadhaa wamekuwa wanatokea watu si waaminifu wakipewa dhamana wanazitumia vibaya matokeo yake rasilimali inatumika kuneemesha watu wachache.

Akatoa wito kwa vijana kuwa,  kwa maswala yanayohusu matumizi mabaya yarasilimali za umma lazima waende mbali zaidi ya mipaka ya itikadi, akiwataka washikamane na kutosahau kuwa wao wanadhamana ya leo na kesho.

"Hivi uzalendo leo uko wapi? Unaweza kukuta Mtanzania tena kijana anashabikia watu kutumia watakavyo rasilimali za nchi hata kuhujumu nchi na bado akaonekana ni shujaa! Tusipoamua kubadilika tutakua tunabomoa nchi kwa mikono yetu wenyewe." alisema Nape kwa uchungu.

Aidha Nape ameitaka wizara ya uwezeshaji chini ya Dr. Mary Nagu kuhakikisha wanaowezeshwa kwa sehemu kubwa ni vijana wazalendo wa kitanzania kwani hiyo ni njia moja wapo ya kupunguza tofauti kubwa ya kipato kati ya masikini na matajiri.

"lengo la wizara ile ni kuhakikisha wazalendo wa kitanzania wanawezeshwa kuumiliki uchumi wao, sasa isije wakawa wanaongezewa uwezo matajiri tu na vijana masikini wa kitanzania wanaachwa wakitoa macho,  hiyo haitakuwa sawa! Tutaomba wizara itoe takwimu kila mara za Idadi ya wanaowezeshwa na ni kina nani" alisisitiza Nape.

Naye Katibu wa NEC uchumi na fedha  Ndg. Lameck Nchemba Mwigulu akisalimia wananchi wa jiji la Mwanza alihoji ugonjwa gani unawaingia watanzania leo kiasi kwamba muda wote wanawaza uchaguzi tu mpaka wamesahau hata kufanya shughuli za maendeleo.
" sikuhizi ni rahisi kukuta watumishi wengi hata serikalini wanajadili uchaguzi wa mwaka 2015 utadhani ni kesho, kama vile wameagana na Mungu watakua hai. Wanajadili kiasi cha kusahau hata kuwajibika. Nani katuloga sisi?" alihoji Nchemba.

Huku akishangiliwa kwa nguvu na kelele za kufurahia ushindi wa CCM Igunga, Mwigulu alisema anashangazwa na kelele zilizopigwa na Chadema kuhusu ushindi wa CCM Igunga kwani taratibu zote zilifanyika kwa uwazi na ukweli kiasi hata kipofu angeweza kuona kuwa uchaguzi ulikuwa huruna wa haki.
" nilistuka nilipowasikia baadhi ya viongozi wa Chadema wakilalamikia matokeo ya uchaguzi mdogo wa Igunga, lakini nashukuru kwa sasa wamenyamaza kwasababu wameona aibu kuendelea kulalamika katika mazingira yale" alisikika Nchemba.
Aidha Nchemba alikemea utaratibu ambao umeanza kujengeka  hasa kwa nchi masikini zinazoendelea, wa viongozi wengi wa kisiasa na vyama vyao kuudanganya umma kuwa kila wanaposhindwa uchaguzi basi haukuwa huru na haki, mpaka washinde wao ndio uchaguzi unakuwa huru na wa haki.

Ziara hiyo ya viongozi  wa CCM taifa kanda ya ziwa itaendelea kwenye wilaya ya Geita na Ukerewe, lengo likiwa ni kuamsha ari ya wanachama hasa baada ya uchagizi mkuu wa mwaka jana ambapo CCM inaonekana kuto fanya vizuri kama ilivyokua mwaka 2005.

Pamoja na Nape na Nchemba, msafara huo pia umeambatana na Mhe. Livingstone Lusinde ambaye ni Mbunge wa Mtera na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, pamoja na Katibu Msadizi Mkuu wa Idara ya Itikadi Ndg. Sixtus Mapunda.

JK AMTEUA TENA BALAZO KAZAURA KUIONGOZA UDSM

Balozi Kazaura
Rais Jakaya Mrisho Kikwete amemteua Balozi Fulgence Kazaura kuwa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa kipindi kingine cha miaka minne.
Taarifa iliyotolewa leo, na Katibu Mkuu Kiongozi Phillemon Luhanjo imesema kuwa uteuzi huo unaanza mara moja (leo hii).
Balozi Kazaura alikuwa Mkuu wa Chuo hicho katika kipindi kilichopita  kilichoishia Julai, mwaka huu, 2011.

ASKARI MMOJA WA ISRAEL ANAPOWAPONYA WAPALESTINA ELFU

Leo ni siku ya furaha na faraja kwa siasa za Israeli na Palestina ambapo mpango wa kubadilishana wafungwa umeanza kutekelezwa.
Msafara wa wafungwa wa Kipalestina ukiondoka kwenye gereza la Ketziot, Kusini mwa Israel leo.
Mpango huo umejumuisha kuachiwa kwa Mwanajeshi mmoja wa Israeli, Gilad Shalit na maelfu ya wafungwa wa Kipalestina waliokua wakitumikia vifungo huko Israel.
Taarifa zinasema ilikua ni nderemo na vifijo huko Ukanda wa Gaza na Kingo za Magharibi (West Bank) ambako ndugu na jamaa walikusanyika kuwapokea.
Gilad Shalit (25) ametumikia kifungo miaka mitano, jitihada za kuponya roho yake, zimeponya roho zaidi ya elfu moja za Wapalestina.
Kwa ujumla Israeli inategemewa kuwaachia wafungwa 1,027 na kwa awamu ya kwanza itawaachia 477. Wafungwa hao wanaachiwa ikiwa baadhi yao wamekaa ndani zaidi ya miaka 30.
Wachunguzi wa hali ya mambo wamesema huenda hatua hiyo ikapunguza uhasama wa kisiasa uliopo kati ya Palestina na Israel.

Monday, 17 October 2011

Ahmadinejad: UCHUMI WA MAREKANI HAUWEZI KUIMARIKA KWA KUISHUTUMU IRANI

Rais wa Iran, Mahmoud Ahmadinejad ameitaka Serikali ya Marekani iliangazie kwa umakini suala la uchumi wa nchi yake unaotetereka kila uchao badala ya kutumia muda mwingi kuishutumu Iran.

Ahmadinejad amekiambia kituo cha televisheni cha Al-Jazeera kwenye mahojiano yaliyorushwa moja kwa moja kama nusu saa iliyopita kwamba nchi yake haina mpango wowote wa kugombana na Marekani.

"Nashangazwa na chuki ya Serikali ya Marekani dhidi ya taifa letu, sisi kila tunapokutana UN tunahubiri amani na nia ya kua na mahusiano mema na Marekani, lakini wao kila uchao wanaeneza chuki dhidi yetu" alisema.

Rais huyo alisema shutuma za hivi majuzi zilizotolewa na Rais Barack Obama kwamba Iran walikua na mpango wa kumuua Balozi wa Saudi Arabia  Marekani ni njama za serikali hiyo kutaka kuigombanisha Iran na Saudia.

"Matatizo ya uchumi wa Marekani ni makubwa sana, kwa kuishutumu Iran matatizo hayo hayawezi kupungua" alisema.

WALIOMUUA MCHINA KUKIONA

Viogozi mbalimbali wakitoa heshima zao, kutoka kulia ni, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe. Mke wa Rais Mama Salma Kikwete, Balozi wa China Liu Xinsheng na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu-Dar es Salaam, Suleiman Kova. 

Mama Kikwete akimfariji Mume wa Marehemu, Zhu Jinfeng ambaye ni Mwenyekiti wa Umoja wa Wafanyabiashara wa China.

Baadhi ya Wakazi wa Dar es Salaam wakitoa Salamu za pole kwa wafiwa.

Mjane akiwa na Mtoto wake.

Picha ya Marehemu, Han Bing.
Marehemu alipigwa risasi kichwani na watu wasiojulikana majira ya saa nne na nusu asubuhi siku ya Jumanne karibu na ofisini kwake iliyopo jirani na Chuo cha Diplomasia, Kurasini.

Inadaiwa mama huyo alibeba pesa taslim 30m/- akielekea benki na zilichukuliwa na watu hao waliotokomea kusikojulikana.

Kufuatia kifo hicho, Serikali kupitia Jeshi la Polisi imeahidi kwamba wahusika wa tukio hilo watakamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria.

Marehemu amezikwa kwenye makaburi ya Mwananyamala, Dar es Salaam mchana huu.

Sunday, 16 October 2011

CHADEMA WANAPOFUNGA MTAA MOSHI MJINI

Hapa Meya wa Manispaa ya Moshi, Jaffari Michael (CHADEMA) amefunga mtaa (Chagga Street), anajibu hoja za CCM walizo zitoa huko Boma Mbuzi hivi karibuni kwamba ndani ya mwaka mmoja Chadema wamepewa halmashauri na hawajafanya chochote cha maana.

Majibu ya Michael yalikua hivi "Wanatutuhumu sisi mwaka mmoja, wao wamefanya nini ndani ya miaka hamsini ya uhuru?" wananchi wakashangilia. Hii imekua kasumba, kwamba wanasiasa wanajibu shutuma kwa shutuma na kwa kua imezoeleka basi kawaida imekua kama sheria.    


MSOGA

Msoga hapa. Ametoka kiongozi mkuu wa nchi.

Thursday, 13 October 2011

IKULU: JK HAKUTOA MSAMAHA KWA WALIO MUUA LUTEN JENERAL IMRAN KOMBE

Rais Jakaya Kikwete
Gazeti la Mwananchi, matoleo ya jana, Jumatano, Oktoba 12 na leo, Alhamisi, Oktoba 13, 2011, limeandika habari zilizodai kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete alitoa msamaha wa kupunguza adhabu ya kifo iliyowakabili askari polisi wa zamani waliopatikana na hatia ya kumpiga risasi na kumwua kwa makusudi aliyepata kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa, Luteni Jenerali Imran Kombe Juni 30, 1996.
 Gazeti hili limedai kuwa Mheshimiwa Rais Kikwete alitoa msamaha huo kwa kupunguza adhabu ya kifo iliyokuwa inawakabili makonstebo wapelelezi Mataba Matiku na Juma Muswa na kuibadilisha kuwa kifungo cha miaka miwili.
 Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, inapenda kufafanua kuwa Mheshimiwa Rais Kikwete hajawahi na hajapata kuhusika hata kidogo kutoa msamaha wa kirais kwa kupunguza adhabu ya wauaji hao wa Luteni Jenerali Kombe tokea kuingia madarakani.
 Masuala yote yanayohusu polisi hao waliohukumiwa kifo kwa mauaji ya Luteni Jenerali Kombe yalifanyiwa maamuzi kabla ya Rais Kikwete kuingia madarakani Desemba 21, 2005.