Tuesday, 8 November 2011

NATIONAL PARKING SYSTEM WAGOMA WAKIDAI MASLAHI BORA



Mkurugenzi Mtendaji wa NPS, Bwana Hassan Khan akizungumza na wafanyakazi wake leo asubuhi akiwashawishi waende kwenye vituo vyao vya kazi wakati menejimenti ikishuhulikia madai yao. Wafanyakazi hao wanadai kwamba wemekuwa wakipunjwa posho zao na wahasibu ambapo wengine wamekuwa wakiambulia 20,000/- kwa mwenzi.
 

Hapa wanatawanyika baada ya kuahidiwa kwamba suala lao litashuhulikiwa na kwamba watapewa majibu siku ya Jumapili. Hata hivyo kwa takriban masaa mawili jamaa hawa hawakufanya kazi leo na hivyo bila shaka kampuni limepata hasara.


KAMATI YA JAIRO YAKABIDHI RIPOTI KWA SPIKA WA BUNGE


Mwenyekiti wa kamati Teule ya Bunge iliyoundwa kwa ajili ya kuchunguza uhalali wa utaratibu wa Wizara ya Nishati na Madini  kuchangisha fedha kupitisha Bajeti na kubainisha endapo kitendo cha Katibu Mkuu Kiongozi kutoa taarifa  kwa waandishi wa habari juu ya uchunguzi wa suala la fedha zilizokuwa zimechangishwa kimeingilia na kuathiri madaraka ya Bunge, Mhe. Ramo Matala Makani (Mb) akimkabidhi ripoti ya Uchunguzi huo Spika wa Bunge Mhe. Anne Makinda Ofisini kwake Bungeni Leo. Pembeni ni Makamu Mwenyekiti was Kamati hiyo Mhe. Martha Umbulla (Mb) akiwa amebeba viambatanisho vya ripoti hiyo.Picha na Owen Mwandumbya wa Bunge

JK AIMWAGIA SIFA UINGEREZA


Rais Jakaya Kikwete na Mama Salma kikwete wakiowapokea Mtoto wa Malkia Prince Charles na Mkewe Duchess of Cornwall Ikulu leo asubuhi jijini Dar es salaam. Picha na Ikulu

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ameielezea Uingereza kama mshirika kakati (strategic partner) katika maendeleo ya Tanzania kutokana na miaka 50 ya ushirikiano na misaada ya maendeleo na ya kiufundi kutoka kwa nchi hiyo.
Aidha, Rais Kikwete ametaka nchi zote mbili, Tanzania na Uingereza, kuongeza jitihada za kuvutia uwekezaji zaidi katika Tanzania kutoka Uingereza ambao thamani yake kwa sasa inafikia dola za Marekani bilioni 1.8 (sawa na sh. bilioni 3060).
Rais Kikwete ameyasema hayo usiku wa jana, Jumatatu, Novemba 8, 2011, Ikulu, Dar es Salaam, wakati wa Chakula cha Kitaifa alichomwandalia Mtoto wa Malkia wa Uingereza, Prince Charles ambaye anatembelea Tanzania na mkewe, Mama Camilla.  Prince Charles na Mama Camilla wako kwenye ziara ya siku tatu nchini Tanzania.
Rais Kikwete amesema kuwa ziara ya Prince Charles imetoa nafasi kwa Tanzania kuwashukuru wananchi wa Uingereza kwa misaada yao mikubwa ambayo kwa miongo mitano iliyopita wametoa kuchangia maendeleo ya Tanzania.
 “Misaada ya Serikali ya Malkia na wananchi wa Uingereza imekuwa muhimu sana katika jitihada zetu za kujikomboa kutoka umasikini na kuelekea katika maisha bora zaidi.  Katika miaka 50 iliyopita mumekuwa nasi katika nyakati za raha na nyakati za shida na wananchi wa Tanzania wamenufaika sana kutoka na misaada ya maendeleo na ya ufundi kutoka Uingereza,” Rais Kikwete amemwambia Prince Charles na ujumbe wake.
 Ameongeza Rais Kikwete katika hotuba yake fupi: “Misaada muliyotupa imesaidia sana kuboresha kiwango cha maisha ya Watanzania wengi. Imeleta tofauti kubwa katika maisha ya wananchi wetu.”
 Rais kikwete amesema kuwa mbali na Uingereza kuwa chanzo kikubwa zaidi cha misaada ya maendeleo na ya kiufundi, nchi hiyo pia imekuwa chimbuko kubwa zaidi la mitaji inayoingia katika uchumi wa Tanzania.
 “Ninayo furaha kusema kuwa mbali na kuwa chanzo kikubwa zaidi cha misaada ya maendeleo na ufundi, Uingereza pia imekuwa nchi inayoongozwa kwa kuleta uwekezaji na mitaji katika nchi yetu. Kwa sasa uwekezaji kutoka Uingereza unafikia dola za Marekani bilioni 1.8.  Lakini utakubaliana nami kuwa kwamba tunaweza kufanya vizuri zaidi kuliko tulipo na lazima tulenge kufanya vizuri zaidi.  Kwa hakika, Uingereza ni mshirika kakati wa maendeleo yetu,” Rais Kikwete amesema.
 Prince Charles yuko nchini kwa mwaliko wa Serikali kwa ajili ya kushiriki katika sherehe za miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara. Alikuwa Prince Philip (Duke of Edinburgh), baba yake Prince Charles, ambaye alimkabidhi funguo za Uhuru wa Tanzania Bara Mwalimu Julius Nyerere, waziri mkuu wa kwanza wa Tanganyika huru na Baba wa Taifa la Tanzania.

Imetolewa na:
 Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
08 Novemba, 2008

SLAA NA TUNDU LISSU WAPO MIKONONI MWA POLISI ARUSHA

Habari kutoka Arusha zinatanabahisha hivyo, polisi wanatarajiwa kuzungumza baadae.

Monday, 7 November 2011

CHADEMA WAIBUA MENGINE ARUSHA JIONI HII

Chadema wamechachamaa tena jioni hii huko Aurusha, habari kutoka huko zinasema wafuasi wa chama hicho wakiongozwa na mwenyekiti wao, Freeman Mbowe wameamua kupiga kambi pale kwenye viwanja vya NMC kwa siku tatu mfululizo mpaka mbunge wao, Godbless Lema apewe dhamana
.
Taarifa za awali zilidai kwamba viongozi wa chama hicho walitoa masaa 24 kwa serikali, Lema awe ameachiwa la sivyo wangetoa kauli.

Haya yanatokea wakati ambapo Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Arusha imemnyima dhamana Lema asubuhi ya leo na kumpa barua ya kufika mahakamani hapo na wadhamini wake tarehe 14 mwenzi huu.

Lema yupo rumande mara baada ya kukataa yeye mwenyewe kuchukua dhamana wiki iliyopita alipofikishwa mahakamani haopo akidaiwa kuongoza maandamano haramu.

Vijana wa Chadema wakielekea viwanja vya NMC ambako wameenda kupiga kambi huko. Polisi wanasema bado wanalifuatilia suala hilo kwa karibu.




WAKULIMA WA KARAFUU WAHAKIKISHIWA UWEPO WA SOKO

Karafuu
Wakulima wa zao la Karafuu Zanzibar wametakiwa kutokuwa na wasiwasi wa kununuliwa Karafuu zao kwani Serikali ina fedha za kutosha za kununulia zao hilo.
 
Akizungumza katika Baraza la Idd ALhaj lililofanyika leo (jana) huko katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi Wete Pemba Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi  Alhaj Dk Ali Mohamed Shein amesema kuwa wananchi wasidanganyike na uzushi ulioenezwa baadhi ya watu kuwa  Serikali  haina fedha zakutosha za kununulia karafuu   jambao ambao sio kweli ni la uzushi na uongo mtupu.
 
Amesema kuwa Serikali  imefarajika kwa jitihada za Wakulima kwa kuuza karafuu zao katika vituo vya Shirika la Biashara la Taifa Zanzibar(ZSTC) ambapo hadi juzi jumla ya tani 2136.91 zenye thamani ya shilingi zaidi ya Billioni 31 zimeshanunuliwa kutoka kwa Wakulima.
 
Alhaj Shein ametowa wito kwa Wakulima kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali kuacha kuuza karafuu
kwani kufawa njia ya Magendo   kwani kufanya hivyo tutakuwa tumeuhami uchumi wetu ambao ni tegemeo kwa Taifa zima.
 
Aidha Dk Shein amevitaka Vyombo vya Ulinzi kuongeza jitihada zake za kupambana na Magendo ya Karafuu.
 
Akizungumzia juu ya usafirishaji wa Mahujaji  wa Zanzibar wanaokwenda Mecca kuhiji Alhaj Shein amewataka mawakala wa Mashirika yanayosafirisha Mahujaji kwaajili yakutekeleza ibada ya Hijja kuondowa usumbufu kwa Mahujaji hao.
 
Amesema pamoja na kuwa idadi ya Mahujaji wa Zanzibar inaongezeka kila mwaka lakini kuna baadhi ya Mahujaji hupata usumbufu katika kutekeleza ibada hiyo kutoka kwa baadhi ya Taasisi zinazosafirisha Mahujaji.
 
Vile vile amezitaka Taasisi zinazoshughulikia safari za Hijja kujenga mashirikiano na sio mashindano wakielewa kuwa huko kufuata njia ya Mwenyezi Mungu kwa kutegemea malipo kutoka kwa Mola.
 
Kuhusu kuwalinda vijana na dawa za kulevya Dk Shein amesema Serikali yake kupitia kamisheni ya kupambana na dawa za kulevya iliopo katika ofisi ya Makamo wa Kwanza wa Rais imejipanga vizuri kuhakikisha kuwa vita dhidi  ya Madawa yakulevya hapa nchini zinafanikiwa.
 
Amezipongeza Taasisi binafsi zinazoshughulia walioathirika na madawa yakulevya kwa jitahada zao za kuwakusanya vijana hao ili watokane na tatizo lautumiaji wa madawa hayo zikiwamo Zanzibar youth forum,Drug Free Zanzibar na Jumuiya Yatawabina ambapo hivi sasa Zanzibar ina jumla ya Nyumba tisa ambapo kila moja ina vijana kati ya kumi na tano hadi ishirini.
 
 
IMETOLEWANA HABARI MAELEZO PEMBA
6/11/2011

HALI SI SHWARI NYUMBA YA MUNGU

Na SHABAN PAZI
 
Hali ya Bwawa la Nyumba ya Mungu, Wilaya ya Mwanga, Kilimanjaro sio nzuri kutokana na kukauka kwa kiasi kikubwa cha maji katika bwawa hilo ikiwa ni matokeo ya mabadiliko ya tabia nchi na uharibifu wa mazingira ulifanywa na shughuli za binadamu.
 
Akitoa taarifa ya hali ya Bwawa hilo kwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Mheshimiwa Leonidas Gama Ofisa Mkuu wa Ofisi ya Maji ya  Bonde la Mto Pangani  Bwana Hamza Sadiki amesema kiwango cha upungufu wa maji katika bwawa hilo kimefikia asilimia 70.
 
Kwa mujibu wa Bwana  Sadiki  kina cha maji katika Bwawa hilo kilikuwa mita 683.13 juu ya usawa wa bahari sawa na mita za ujazo milioni 233.27.
 
Mheshimiwa Gama ameadhimia kufanya ziara juma lijalo katika maeneo ambayo ni vyanzo vya maji vya bwawa hilo  ili kujionea hali ya uharibifu wa mazingira katika vyanzo hivyo.
 
 Mkuu wa Mkoa wa KILIManjaro Mheshimiwa Leonidas Gama akiongea na wananchi wanaishi karibu na bwawa la Nyumba ya Mungu wilayani Mwanga
         



Sehemu ya Miundombinu ya kuzalishia umeme katika bwawa la Nyumba ya Mungu
 
 
 

MAZUNGUMZO YA JK NA MWANAMFALUME: CHADEMA WATOA ANGALIZO

MNYIKA
TAARIFA KWA UMMA
Kurugenzi ya Mambo ya Nje na Mahusiano ya Kimataifa ya CHADEMA inatoa mwito kwa Rais Jakaya Kikwete kutumia mazungumzo kuhusu mahusiano baina ya Tanzania na Uingereza yanayotarajiwa kufanyika wakati wa ziara ya mtoto wa Mfalme wa Uingereza Charles na mkewe kuanzia tarehe 7 Novemba 2011 kushughulikia masuala yaliyojitokeza hivi karibuni yenye kuweza kuathiri mahusiano ya nchi zetu.
Katika siku za karibuni Serikali ya Uingereza imepunguza misaada yake ya kibajeti kwa Tanzania kwa asilimia 30 kutokana na kutoridhishwa na utendaji wa serikali hususani kuhusiana na masuala ya kuboresha mazingira ya kibiashara na kutoa fursa kwa wananchi kuwawajibisha viongozi. Uamuzi huo wa Serikali ya Uingereza umeelezwa kupitia barua ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Nchi hiyo Andrew Mitchell ya tarehe 3 Agosti 2011 kwenda kwa Mwenyekiti wa Kamati Teule ya Bunge la Nchi hiyo kuhusu Uchumi .
“Ni vizuri pande zote mbili Rais Kikwete na Mwanamfalme Charles wakawaeleza watanzania kuhusu sababu za ziada za maamuzi haya. Vyanzo mbalimbali vinaeleza kuwa sababu halisi ni washirika wa maendeleo kutoridhika na kasi ya vita dhidi ya ufisadi kwa upande mmoja na kwa upande mwingine ukanda wa ulaya (Eurozone) kukumbwa na matatizo ya kifedha”.
Aidha, Rais Kikwete atumie mazungumzo ya ziara hiyo kuwaeleza watanzania mkakati wa nchi kupunguza tatizo la utegemezi ambalo linasababisha nchi kupewa misaada yenye masharti ya kibeberu, ikiwemo kulieleza taifa namna ambavyo nakisi ya bajeti inayotokana na wahisani kupunguza fedha zao kwa Tanzania itaweza kuzibwa kwa kuongeza uzalishaji, mauzo ya nje na kupunguza ubadhirifu katika serikali.
Kwa upande mwingine, pamoja na kauli iliyotolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Mahusiano ya Kimataifa Benard Membe kuwa Tanzania iko tayari kukubali kukosa misaada yote toka Uingereza ikiwa serikali ya nchi hiyo italazimisha kutungwa kwa sheria ya kuruhusu ushoga, usagaji na ndoa ya jinsia moja; ni muhimu kwa Rais Kikwete kutumia mazungumzo hayo kufikisha ujumbe kamili wa kupinga masuala hayo kwa niaba ya watanzania.
Kurugenzi ya Mambo ya Nje na Mahusiano ya Kimataifa ya CHADEMA inaunga mkono msimamo wa serikali ya Tanzania wa kukataa kufanya mabadiliko ya sheria ya kuruhusu vitendo hivyo ambavyo ni kinyume cha sheria na utamaduni wetu.
“Kwa mujibu wa katiba ya CHADEMA kifungu 3.1.8, kwa falsafa yetu ya nguvu ya umma na itikadi ya mrengo wa kati CHADEMA inaweka umuhimu wa pekee katika familia kama moja ya taasisi muhimu za kijamii. Hivyo, tunapinga vitendo vya ushoga, usagaji na ndoa ya jinsia moja kwa kuwa vinakinzana na misingi ya maadili na uwepo wa familia”.
Kurugenzi ya Mambo ya Nje ya CHADEMA inataka ujumbe mahususi utolewe na Rais Kikwete kupitia ziara hiyo sababu wakati wa kujadiliwa kwa ripoti ya ndani ya mustakabali wa Jumuia ya Madola (Internal Report on the future relevance of Commonwealth) katika Mkutano wa Jumuia ya Madola uliomalizika karibuni; Rais Kikwete hakutoa ujumbe mkali kwa Serikali ya Uingereza wakati wa kujadiliwa kwa masuala ya haki za binadamu tofauti na kauli ambayo serikali iliitoa kupitia vyombo vya habari wakati ujumbe wake uliporejea Tanzania.
Wenu katika demokrasia na maendeleo,
 
John Mnyika (Mb)
Mkurugenzi wa Mambo ya Nje na Mahusiano ya Kimataifa (CHADEMA)
06/11/2011

Friday, 4 November 2011

MHESHIMIWA MNYIKA UNAIFAHAMU BARABARA HII JIMBONI KWAKO?



Mnyika
 Takriban mwaka mzima sasa barabara hii  ya Tandale Uzuri imejaa mashimo na inaonekana kama imesahaulika. Wananchi na watumiaji wa barabara hii nikiwemo mimi najiuliza hivi watendaji wako wapi?

Kwa bahati mbaya au nzuri, barabara hii ipo kwenye Jimbo la Ubungo, Jimbo la John Mnyika ambaye anatokea chama cha Upinzani-CHADEMA, hili ni doa kwa uongozi wake ambao ndio kwanza una mwaka mmoja. Je Mheshimiwa anafahamu kwamba hii barabara ipo hivi? 

"Hali hii inasababisha tukose imani na wanasiasa, kwa kuwa ni mwaka jana tu walikuwa wanazunguka nyumba kwa nyumba wakisaka kura na moja ya ahadi zao ilikuwa kwamba wataboresha barabara, lakini kama uboreshaji wenyewe ndio huu basi naona hakuna haja ya kupiga kura," anasema mpiga kura mmoja wa Sinza ambaye barabara hii ni kero kwake.


Mzee huyu mwenye nguo nyeusi amejitolea kujaza kifusi kwenye barabara na anawatoza madereva kati ya shilingi mia na miambili, kwa sababu watumiaji wanakerwa na hali hii, basi hawana namna lazima watoe, lakini sasa huyu mzee naye hataki kumaliza haraka kwa kuwa hiki sasa kimekua kitega uchumi. (KUFA KUFAANA)


Hapa ukija kichwakichwa unavunja sample.

Kila mtu anapita pembeni, labda kazi ya kujaza kifusi ikikamilika italeta ahueni.

Thursday, 3 November 2011

JAMII YETU INATAFUNWA NA UMASIKINI?

Nipo maeneo ya Mwananyamala Hospitali hapa, nakutana na picha hii ya kusikitisha, jamaa wanaeleka kwenye chuma cha kuhifadhia maiti, Hospitali ya Mwananyamala.

Kilichonisisimua hapa ni kwamba sanduku la kubebea maiti limebebwa kwenye Bajaj, picha hii inaniambia pengine hii ni ishara ya umasikini, kwa kuwa kila mwanajamii angependa amsitiri kwa hali na mali ndugu yake anapoaga dunia, lakini hapa inaonekana hali na mali ndio imeishia kwenye Bajaj.

Hapa bajaj inakata mitaa.

Hapa wanaingia hospital. Mungu ailaze roho ya marehemu mahala pema peponi. Ameen

WAZAZI SHULE YA KIKONGO WAJADILI HATMA YA WATOTO WAO

Hali leo ilikua hivi; wanafunzi walikuwa wanazagaa kila mahali wakati wazazi walikua kwenye kikao cha kujadili hatma ya watoto wao.





Wednesday, 2 November 2011

MULUGO AFUNGA SHULE YA WAKONGO ILIYOFUNGULIWA KWENYE MAJENGO YA BAR SINZA

Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo (kushoto) akizungumza wakati wa akiifunga shule hiyo ( Ecole Francophone Des Grands Lacs) iliyopo Sinza Mori, Jijini Dar es Salaam, Kulia ni Mmiliki wa Shule, Bande Ndagundi.

Baadhi ya wanafunzi wakifuatilia maelezo ya Waziri, Mulugo.

Mmoja wa walimu wa shule hiyo ambae ni raia wa Congo akiwaza maisha baada ya leo. Hili ni moja ya madarasa ya shule hiyo.

Jengo hili ambalo zamani lilikuwa kaunta ya Bar,  sasa lilikuwa likitumiwa kama library ya shule hiyo.


Tuesday, 1 November 2011

JAJI WARIOBA AWASHAURI WABUNGE JUU YA UUNDWAJI WA KATIBA MPYA

Waziri Mkuu mstaafu Jaji Joseph Sinde Warioba (kulia) akitoa ushauri wa kitaalamu na uzoefu kwenye Kamati ya Sheria, Katiba na Utawala wakati wa mjadala wa Muswada wa Sheria ya Katiba ya Mwaka 2011 ambapo mwanasheria huyo mkongwe amewataka watanzania wote kwa ujumla kuwa kitu kimoja katika jambo hili.

Wajumbe na wataalam mbalimbali wa Kamati ya Sherai, Katiba na Utawala, Kamati ya Mashirika ya Umma, Kamati ya Fedha za Serikali za Mitaa na Kamati ya Hesabu za Srikali wakiwa katika mijadala mikali-mikali leo.

Kwa hisani ya; Prosper Minja wa Bunge

POLISI, WALINZI WA G4S WATIBUA MCHONGO WA MAJAMBAZI KUIBA KWENYE ATM ZA NBC MTONI KWA AZIZI ALI JIONI HII



KIMBANGULILE SUPPORT GROUP WAOMBA MSAADA WA JENGO

Watoto wa Kimbangulile Support Group
Kituo cha wasiojiweza cha Kimbangulile Support Group kimesema kinahitaji jengo kwa ajili ya ofisi na darasa kwani kwa muda wa miezi sita sasa hawajaweza kufundisha watoto 18 kati ya 64 wanaowahudumia katika kituo hicho.

Mwenyekiti wa kikundi hicho, Bi. Leokardia Mchau ametoa ombi hilo mwishoni mwa wiki wakati wafanyakazi wa kampuni ya DataVision International Limited walipotembelea kituo hicho na kutoa msaada wa vifaa mbalimbali vikiwemo vyakula na vifaa vya malazi.

Kituo hicho cha Kimbangulile Support Group kipo kata ya Mianzini, eneo la Mbagala Rangi Tatu, nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.

“Watoto tunaowahudumia hawalali hapa lakini wanakuja kujifunza kila siku, kuna watoto wanne wanaoratajia kufanya mtihani wa darasa la nne mwezi huu, pia wako watoto 10 ambao wataingia darasa la kwanza mwakani na wengine wanne ambao ni walemavu wa viungo; wote hawa tumeshindwa kuwafundisha ipasavyo,” alisema Bi. Mchau.

Akizungumzia kuhusu tatizo la darasa, Bi Mchau alisema hawajaweza kuwafundisha vizuri watoto hao kutokana na uamuzi wa mwenye nyumba waliyokuwa wakiitumia kuamua kupangisha chumba kilichokuwa kikitumika kama darasa.

Akifafanua kuhusu mahitaji ya kituo hicho, Bi. Mchau alisema wana watoto 10 ambao ni walemavu; mmoja anahitaji mguu wa bandia, mwingine ana matatizo ya macho hawezi kuona, yuko mwingine ambaye ni bubu na mwingine mmoja ana matatizo ya mifupa haikui. Pia wana watoto wenye utindio wa ubongo na bubu mmoja.

“Pamoja na yote hayo, tuna watoto wawili ambao wamefukuzwa shule kwa kukosa ada. Mmoja yuko kidato cha kwanza na mwingine yuko kidato cha pili... tunaomba wasamaria wema watusaidie kubeba mzigo tulionao,” aliongeza.

Akijibu baadhi ya maombi yao, Meneja Masoko na Mahusiano wa kampuni hiyo, Bi. Teddy Qirtu alisema wanaridhishwa na maendeleo ya kikundi hicho ikilinganishwa na hali ilivyokuwa Aprili, 2011 walipowatembelea mara ya kwanza. “Tunafurahi kuona juhudi za walezi na walimu kwani kuna maendeleo kwa watoto hawa hasa kielimu...,”

Alisema kampuni hiyo itawasaidia kulipia kodi ya vyumba watakavyopangisha na kuongea na uongozi wa shule iliyowafukuza watoto hao wawili. Pia aliahidi kumsaidia mtoto Fatuma ambaye anahitaji mguu wa bandia.

Wafanyakazi wa kampuni ya DataVision International Limited walitembelea kituo hicho mwishoni mwa wiki ikiwa ni sehemu ya mfumo wa kuendeleza jamii (growing people) na kutimiza wanayoyasema (walking the talk) ambao kampuni hiyo imejiwekea chini wa mpango wake wa huduma kwa jamii (Corporate Social Responsibility -CSR).