Na FAKI MJAKA-Maelezo Zanzibar 12/01/2012
Dkt Shein akikagua gwaride. |
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Ali Mohamed Shein,amesema serikali yake imejidhatiti katika kuimarisha huduma za jamii kwa kasi zaidi ili ziweze kukidhi mahitaji ya wananchi wake.
Rais Shein ameyasema hayo leo alipokuwa akilihutubia taifa katika kilele cha maadhimisho ya Sherehe za miaka 48 ya Mapinduzi ya Zanzibar yaliyofanyika Uwanja wa Amani Zanzibar
Amesema mafanikio mbalimbali yaliyopatikana katika kipindi hicho cha miaka 48 ni pamoja na mfumo wa utawala bora ambapo alisema Zanzibar ya sasa imepiga hatua kubwa katika kuongoza kisheria kuliko ilivyokuwa kabla Mapinduzi hayo.
Alisema mikakati iliyopo sasa, ni kuhakikisha kilimo kinapewa kipaumbele ili kiendeshwe kitaalamu jambo litakalopelekea kuzalisha kwa wingi mazao ya chakula na biashara.
Dk Shein pia, alisema katika serikali yake inayoendeshwa kwa mfumo wa umoja wa kitaifa, kumekuwa na ushirikiano mzuri kwa watendaji, ambao unawapa imani wananchi hasa baada ya ujio wa serikali hiyo kuzika kabisa siasa za chuki na uhasama.
Alieleza kuridhishwa kwake na kasi ya maendeleo, na kuahidi kuwa serikali yake itaendelea na dhamira ya kuwapatia wananchi huduma muhimu na za uhakika kama vile elimu, afya, maji safi na salama pamoja na kuweka mazingira mazuri kwa wafanya biashara na wafanyakazi.
Katika hatua nyingine Dk. Shein amewataka Wananchi wa Zanzibar kuacha woga wa kutoa maoni yao wanayodhani yanafaa kwa Tume ya kukusanya maoni ya kupata Katiba mpya pale ambapo tume hiyo itaanza kazi zake.
Amesema Katiba inayokusudiwa kutungwa ni ya Wananchi wote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hivyo Wazanzibari ni haki yao kutoa maoni yao wala hakuna mtu atakayewabeza
Aidha amewaasa wale wote wenye tabia ya kudharau maoni ya wenzao waache kufanya hivyo kwani kila mmoja ana uhuru wake wa kutoa maoni kulingana na anavyoamini yatasaidia.
Mapema, Dk Shein alipokea saluti kutoka kwa askari wa vikosi vya ulinzi na usalama, pia kukagua Gwaride la vikosi vya Ulinzi na Usalama vya Tanzania pamoja na Maandamano ya Wananchi na Wafanyakazi wa Wizara mbalimbali za uma na sekta binafsi.
Sherehe hiyo ya kilele cha kuadhimisha miaka 48 ya Mapinduzi ya Zanzibar ilihudhuriwa na viongozi wa kitaifa akiwamo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Jakaya Mrisho Kikwete, Marais wastaafu Mabalozi mbalimbali wa Nchi za Nje waliopo Tanzania Viongozi mbalimbali wa Serikali pamoja na wananchi mbali mbali kutoka maeneo ya Tanzania Bara na Visiwani.
No comments:
Post a Comment