Tuesday, 4 October 2011

Obama ni Rais wa Wayahudi?

Baada ya hotuba ya Rais Obama wa Marekani kwenye mkutano wa hivi majuzi wa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa (UN), baadhi ya wachambuzi wameshangazwa na tabia ya Rais huyo kuendelea kulinyenyekea Taifa la Israel.

Obama ni “Rais wa kwanza Marekani Myahudi?”. Hicho kilikua kichwa cha habari kwenye Jarida moja la Marekani-New York Magazine.   Kwa kumsikiliza Obama anaongea UN, wengi wangekubaliana na kichwa hicho cha habari.
Obama
Rais wa Marekani amekumbatia maamuzi ya Israeli kukataa kuunga mkono kutambuliwa na UN kwa Palestina kama taifa huru.

Hata hivyo baadhi ya wachambuzi wamesema, kukataa kuitambua Palestina sio msimamo wa Wayahudi wote au Wamarekani wote, lakini Obama amewashangaza wengi kwa kuonyesha unazi huo kwa Israel ambao unaelezwa kua unazidi hata ule aliokua nao, Rais Gorge Bush. 

Wachunguzi wa hali ya mambo wanasema Obama alisoma hotuba yake kana kwamba ni Baba wa Taifa la Israel na kwamba inaonekana kana kwamba hotuba ile iliandikiwa Israel naye akapewa tu asome.

Msimamo huo wa Obama unawastusha wengi haswa ikizingatiwa kwamba aliingia madarakani kwa kauli mbiu ya “change we can believe in”-akimaanisha “mabadiliko tunayoweza kuyaamini”.

Ni kutokana na kauli mbiu hiyo, Rais Obama alisema kwamba angependa kuyaona mataifa ya Kiarabu yakifurahia amani, lakini juzi amefanya kinyume.

Kiongozi wa Mamlaka ya Palestina, Mahmoud Abbas
Obama anadai kwamba Waarabu ndio wanaochochea vita kwa kuwachokoza Waisrael. Lakini historia inaonyesha kinyume chake, Israel ndio wachokozi, ndio waliochochea vita mwaka: 1956, 1967, 1982, 2006 na 2008. Vita ya mwaka 1973 peke yake ndiyo ilichochewa na Waarabu na hiyo ilikua ni baada ya Israel na Marekani kukataa mpango wa amani.

Kwanini Wapalestina wawe wahanga wa siasa za Marekani wakati wanashikiliwa mateka na Israeli kwa miongo sita sasa?

Msimamo wa Tanzania:

Rais Jakaya Kikwete alisema wazi kwenye mkutano huo wa UN kwamba Tanzania inaunga mkono jitihada za Palestina kutambuliwa na UN kama taifa huru.

Naye Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe alisema kwamba Wapalestina wanaishi kwenye ardhi yenye mabakamabaka kama ngozi ya chui kutokana na kutokua na mipaka inayoeleweka.

“Waisrael wamezungushia kuta maeoneo yote ambayo yanarasilimali na wanayaita kwamba ni nchi yao, Wapalestina wamebaki kutangatanga bila kujua hatima yao, tunataka nao wawe na uhuru na taifa lao,” alisema Membe.

Membe alionya kwamba msimamo wa Marekani huenda ukazua mgogoro wa kidiplomasia baina yake na mataifa mengine.


Monday, 3 October 2011

Nani kala mtaji wa CUF Igunga?

Uchaguzi wa Igunga umemalizika, CCM wamevuna neema, Chadema wamevuna matumaini, CUF wamevuna aibu. Swali kubwa la kujiuliza hapa, “Nani kala mtaji wa CUF?”.

Ikumbukwe kwamba vyama vyote vilivyokwenda Igunga vilikwenda kutafuta kura, lakini tofauti na wengine CUF wao walidai kwamba hata kabla ya kampeni walikua na mtaji wao wa kura 11,000.

Siku za mwanzo kabisa, Naibu Katibu Mkuu wa CUF (Bara), Julius Mtatiro alinukuliwa akisema kwamba Chadema hawana nia ya dhati ya kujenga upinzani imara nchini, akadai kwamba wao (CUF) ndio wenye nguvu Igunga na Chadema walitakiwa wawaunge mkono ili wachukue jimbo.
Mbunge wa Igunga, Dk Dalaly Kafumu

Wakati akiyasema haya, Mtatiro pengine hakua akifahamu vizuri hali halisi ya Igunga, Igunga kulikua na mambo mawili: Kwanza Chadema hawakua na mgombea kwenye uchaguzi mkuu mwaka jana. Pili kura 11,000 za CUF zilitokana na Wanachadema walioungana kumpigia mgombea wa CUF.

Ukweli huu unajidhihirisha pale ambapo, Dr Slaa ambaye hakupita kabisa Igunga kwenye kampeni za Urais, alipata kura 8,000 wakati CUF ambacho kilikua na mgombea wa Ubunge, Mgombea wake wa Urais, Prof Ibrahim Lipumba alipata kura 3,000 tu.

Kwa matokeo kama haya, CUF hawakutakiwa kwenda Igunga kifua mbele, walitakiwa kujua kwamba mtu aliyepata kura 8,000 bila kampeni, akifanya kampeni chama chake kitapata kura nyingi zaidi, na hilo ndilo lililotokea.

Mtatiro

Kwa hali ilivyojitokeza, pengine CUF ndio walipaswa kuwaachia wenzao Jimbo, ili wasigawe kura lakini ndio hivyo wameshalikoroga.

Hata hivyo, Mtatiro alidai kwamba kamwe hawatakiunga Chadema mkono sehemu yeyote hata kama kina nguvu, akadai kwamba msimamo huo wa CUF unatokana na ukweli kwamba Chadema wao hawaamini katika kusaidiana.

“Mwaka jana niligombea Ubungo, nilikua najua kabisa kwamba Chadema wananguvu, lakini singeweza kuwaachia kwa kuwa hata wao hawajawahi kutuachia maeneo ambayo tunanguvu kama hapa Igunga,” alisema mwanasiasa huyo ambaye mwaka jana aligombea Ubunge kwenye Jimbo la Ubungo.

Hata hivyo, baada ya matokeo kutangazwa Igunga, Mtatiro na aliyekua mgombea wa CUF, Leopold Mahona wamelalamika kwamba kampeni za Igunga zilitawaliwa na kumwaga fedha.

Lakini hawakueleza kiundani, ikiwa hiyo ndiyo sababu pekee iliyowafanya wafanye vibaya kiasi hicho pamoja na kutumia helikopta kwa mara ya kwanza katika historia ya chama hicho.

Ismail Jussa ambaye ni Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi kwa tiketi ya CUF na ambaye alikua Igunga ameandika kwenye mtandao wa kijamii wa Facebook akisema watakaa kama chama watafakari ya Igunga.

Jussa
“Tumefanya kila lililo kwenye uwezo wetu kuendesha kampeni Igunga na tuliamini tutafanya vizuri. Wapiga kura wa Igunga wameamua vinginevyo. Tunayaheshimu maamuzi yao hata kama hayatufurahishi.

Ndiyo matakwa ya demokrasia! Kama Chama, tutakaa na kufanya tathmini na kisha kuchukua hatua zinazofaa katika kukirejesha kwenye chati” amesema Jussa.

Katika uchaguzi huo, Mgombea wa CCM, Dk Dalaly Peter Kafumu ameshinda kwa kura 26,488, akifuatiwa kwa karibu na Mgombea wa Chadema, Joseph Kashindye aliyepata kura 23,360 na Mahona wa CUF ameambulia kura 2,104.

Ni katika uchaguzi ambao Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imesema watu wachache sana walijitokeza kupiga kura, ni watu 53,672 tu, kati ya 171,077 waliojiandikisha.


Sunday, 2 October 2011

Hongereni Igunga kwa Utulivu

Tofauti na ilivyokua ikitarajiwa, uchaguzi wa Igunga umemalizika jioni ya leo kwa amani na utulivu. Lakini bado tatizo la wapiga kura kujitokeza linaonekana ni kubwa.

Ripoti zinaonyesha kwamba vituo vingi vya mjini wamejitokeza kama asilimia hamsini (50%) tu ya wapiga kura ambapo pia katika matokeo ya awali CCM wanaonekana kuchuana vikali na Chadema, huku CUF na vyama vingine vikifanya vibaya.

Kura

Hata hivyo mchezo ni dakika tisini, na kwa mujibu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) dakika tisini za mchezo huu ni masaa 24. Ndani ya masaa hayo mshindi atatajwa na hapo kutakua hakuna tena minongono wala nini.

Hongereni Igunga kwa kua watulivu katika kipindi hichi.

Saturday, 1 October 2011

Kipande cha Hotuba ya Rais Jakaya Kikwete kuhusu Igunga.

Rais Jakaya Kikwete

Uchaguzi wa Igunga
Ndugu Wananchi;
Kama mnavyofahamu siku ya Jumapili tarehe 2 Oktoba, 2011 ndugu zetu wa Jimbo la Igunga, Mkoani Tabora watapiga kura kuchagua Mbunge katika uchaguzi mdogo.  Napenda kutumia fursa hii kuwatakia wananchi wa Igunga uchaguzi mwema na kuwaomba siku hiyo wajitokeze kwa wingi kutumia haki yao ya kikatiba ya kumchagua mtu wanayemtaka kuwa Mbunge wao kwa kupiga kura.  Haitakuwa sawa hata kidogo kama ndugu zetu wa Igunga wataacha kutimiza wajibu wao huo wa msingi kama raia. 
Ndugu Wananchi;
 Ningependa kuwahakikishia kwamba Serikali imejiandaa vya kutosha kutimiza ipasavyo wajibu wake wa ulinzi na usalama kwa wananchi wa Igunga katika kipindi hiki cha uchaguzi.  Hivyo wananchi wajitokeze kwa wingi kupiga kura bila wasiwasi wowote.  Usalama utakuwa wa uhakika katika vituo vyote na kamwe hatavumiliwa mtu yeyote atakayefanya au hata kujaribu kufanya vitendo vya uvunjifu wa amani, vurugu au fujo.  Hatukubali siku ya kupiga kura iwe ni siku ya watu kujifungia ndani au kuogopa kutoka nje.  Nawahakikishia hilo halitatokea huko Igunga.  Na wanaodhani kuwa tunatania wathubutu, watadhibitiwa ipasavyo.
Nawasihi, wananchi wa Igunga kuendelea kudumisha amani, kabla ya uchaguzi, wakati wa uchaguzi na baada ya matokeo kutangazwa.  Nawaomba msikubali wanasiasa wawageuze chambo cha kuendeleza maslahi yao binafsi ya kisiasa na tamaa zao za madaraka zilizovuka mipaka.  Amani ya nchi yetu ni tunu adhimu ya taifa letu tuliyoirithi kutoka kwa waasisi wa taifa letu Baba wa Taifa hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na hayati Mzee Abeid Amani Karume.  Tumeapa kuidumisha na kuiendeleza na tumefanya hivyo kwa mafanikio hadi hivi sasa. 
Ndugu zangu, Watanzania Wenzangu;
 Tume ya Taifa ya Uchaguzi imeshawahakikishia wapiga kura wa Igunga kwamba maandalizi yote yamekamilika na shughuli za uchaguzi kule Igunga zitakwenda kama inavyotarajiwa.  Wamesema vifaa vyote tayari vimesambazwa katika Kata zote, Wasimamizi wa Vituo na Mawakala wa vyama wamekamilika.  Kwa jinsi Tume ya Uchaguzi ilivyojipanga,  ninayo imani kuwa mchakato mzima wa uchaguzi utakwenda vizuri.    
Ni matumaini yangu kwamba Tume itaendelea kuwaelimisha wananchi taratibu za kufuata ili wananchi washiriki kwa ukamilifu katika kutimiza haki yao ya kikatiba.  Ningependa kuona kuwa kila mtu aliyejiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura anapata fursa ya kupiga kura kwa uhuru na bila bugudha yoyote.  Nawatakia uchaguzi mwema.
Mungu Ibariki Afrika!
Mungu Ibariki Tanzania!
Asanteni kwa Kunisikiliza.

Nukuu kuhusu uchaguzi Igunga.

Mwenyekiti wa Muda wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Prof Amon Chaliga amenukuliwa na gazeti moja la kila siku la hapa nchini akisema yafuatayo kuhusu uchaguzi wa Igunga.
MATOKEO
“Tunaamini kwamba kila kitu kitakwenda sawa na kama hivyo ndivyo, basi hakutakuwa na sababu ya kuchelewesha kutangaza matokeo... na kila uchaguzi mdogo uliofanyika, imethibitika kwamba matokeo yanaweza kutangazwa mapema,”

MAWAKALA
"Hawa mawakala wana wajibu wa kulinda maslahi ya vyama vyao na wagombea wanaowawakilisha, hawa wanashiriki katika mchakato mzima wa uchaguzi, lazima wafanye hivyo ili kuhakikisha kwamba taratibu zinafuatwa,”

POLISI
“Sasa hapo ndipo nasema kwamba mawakala na polisi wanatakiwa wafanye kazi yao, masanduku ya kura yanapokusanywa yanasindikizwa na mawakala wa vyama wanaokuwa katika vituo ukusanyaji wa masanduku unapoanzia,”

Kila la heri Igunga

Tambo, mbwembwe na vurugu za kampeni zinafikia mwisho leo huko Igunga, uchaguzi umewadia, ambapo kesho wapiga kura wa Jimbo hilo watafanya maamuzi  juu ya wanayemtaka awe Mbunge wao.
Wagombea walikua nane, lakini dakika tisini za mchezo zilitawaliwa na wagombea watatu kutoka vyama vya CCM, Chadema na CUF.


Mgombea Ubunge Jimbo la Igunga kwa tiketi ya CCM, Dk Dalaly Kafumu (katikati) akiwa ameshikana mikono na wagombea wenzake Joseph Kashindye wa Chadema (kushoto) na Leopold Mahona wa CUF baada ya kumalizika kwa mdahalo wa pamoja uliofanyika kwenye ukumbi wa Sakao mjini Igunga hivi karibuni.
Hata hivyo kupitia yale yaliyokua yakiripotiwa kwenye vyombo vya habari, kampeni za Igunga zilitawaliwa na visa na vituko zaidi kuliko sera za wagombea.
Lakini, yote kwa yote wapo wagombea waliotoa ahadi japo kwa uchache na wapo waliotangaza sera zao japo kwa uchache.Hapo kwenye ahadi na sera ndipo wapigakura wanapopaswa kuegemeza maamuzi yao.

Matatizo ya Igunga yanafahamika, ambayo ni pamoja na;
  1.  Maji
  2.  Daraja la Mbutu
  3. Ukame (unaopelekea njaa mara kwa mara)
  4.  Rasilimali za madini ambazo wenyeji wanadai hawafaidi vya kutosha
  5.  Shule hazina waalimu wa kutosha
  6. Huduma hafifu za afya, na
  7. Miundombinu duni.
Mwenye majawabu ya mambo hayo hapo juu, atakua ndiye mwenye kisu kikali na mwenye kisu kikali ndiye mla nyama.

Maamuzi yawe ya kimantiki zaidi, maamuzi yanayotokana na uchambuzi wa sera za wagombea na uwezo wao wa kusukuma mbele gurudumu la maendeleo ya Jimbo la Igunga.
Wapigakura waache jazba, waache ushabiki, wasiongozwe na ushawishi wa rushwa, wawe watulivu na wajitokeze kwa wingi kumchagua Mbunge wao.
Kila la heri Igunga.

Hatua zichukuliwe kukabili mvua Dar es Salaam


Mvua za rasharasha zilizonyesha Jijini Dar es Salaam siku ya Ijumaa, zimeonyesha kwamba bado miundombinu ya maji taka jijini haipo katika hali nzuri.
Mvua hizi zinakuja siku chache tangu Mameya kutoka miji mbalimbali nchini walipofanya mkutano wao juzi jijini chini ya mwavuli wa Mtandao wa Miji Tanzania (TACINE).

Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Dk Didas Masaburi
Wakati wa mkutano huo, Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Dk Didas Massaburi alisema mambo kadhaa yamefanyika kuzuia mafuriko yanayosababishwa na miundombinu hafifu ya maji taka.
 
Massaburi aliyataja maeneo hayo kua ni pamoja na makutano ya barabara za Bibi Titi na Morogoro (eneo la NSSF Akiba) na Mtaa wa Uhio.

Eneo la Akiba (Makutano ya Bibi Titi na Morogoro Road)

Hata hivyo halihalisi iliyojitokeza siku ya Ijumaa inaonyesha kwamba tatizo bado ni kubwa na haswa ikizingatiwa kwamba yale yalikua manyunyu tu au rasharasha.
Hivyo ni vyema uongozi wa jiji ukajipanga vizuri zaidi katika kuhakikisha kwamba mitaro yote (sio Ohio na Akiba tu) inazibuliwa.


Uchafu
 Viongozi pia wanaowajibu wa kusimamia sheria ndogondogo za miji na majiji ipasavyo na kwa kufanya hivyo tutaepuka matatizo kama haya ya miundombinu ya maji taka kuziba.

Kwa mfano viongozi wote wanakiri kwamba, kutupa taka mitaani ovyo ni kosa la kisheria lakini nani amewahi kukamatwa jijini Dar es Salaam kwa kutupa chupa ya maji barabarani? Pengine hata wananchi wenyewe hawajui kwamba ni makosa kufanya hivyo. 
Taka hizo zinazotupwa ovyo ndio zinazoziba miundombinu ya maji taka na mwisho wa siku barabara za jiji zinageuka kua mito.
Wakati mwingine suala la usafi wa barabara zetu limekua halitiliwi maanani, michanga inajaa barabarani, haifagiliwi na matokeo yake mvua zinaponyesha michanga yote inasukumwa mitaroni na inapelekea kuziba.
Maswali ni mengi, kwa mfano barabara zetu zimejaa matangazo ya biashara lakini ni chafu. Mapato yanakwenda wapi?  

Friday, 30 September 2011

Zambia yapata Makamu wa Rais Mzungu.

Habari kutoka Zambia zinasema , Rais wa Nchi hiyo, Michael Sata amemteua mzungu, Guy Scott kua Makamu  wake.
Guy Scott

Hatua hiyo imeibadilisha kabisa historia ya nchi hiyo ambayo haijawahi kua na kiongozi wa ngazi ya juu mzungu tangu ipate uhuru.
Kwa mujibu wa Katiba ya Zambia, Rais akifariki makamu wake anashika hatamu lakini uchaguzi lazima ufanyike ndani ya siku 90.

Thursday, 29 September 2011

Nukuu ya Leo

"Serikali ya Marekani huenda ikaingia kwenye mgogoro wa kidiplomasia na nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa (UN) endapo itatumia turufu kuzuia ombi la Palestina kua nchi"  Bernard Membe (Waziri wa Mambo ya Nnje na Ushirikiano wa Kimataifa)

Papa Benedict XVI aipongeza Tanzania

Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, Baba Mtakatifu Benedict XVI ameeleza kufurahishwa na kuridhishwa kwake na amani, utulivu na uvumilivu wa kidini ulioko baina ya dini mbalimbali nchini.
Rais Jakaya Kikwete (Kulia) akimkaribisha Ikulu Balozi wa Makao Makuu ya Baba Mtakatifu ya Vatican katika Tanzania anayemaliza muda wake, Mhashamu Askofu Mkuu Joseph Chennoth.

 Kwa mujibu wa Taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu msimamo huo wa Papa Benedict umetolewa Alhamisi wiki hii na Balozi wa Makao Makuu ya Baba Mtakatifu ya Vatican katika Tanzania, Mhashamu Askofu Mkuu Joseph Chennoth.
Mhashamu Askofu Mkuu Chennoth alikuwa anamuaga Rais Jakaya Kikwete baada ya kumaliza muda wake wa uwakilishi wa Vatican katika Tanzania.
Askofu Mkuu Chennoth amefanya kazi nchini miaka sita ikiwa ni sehemu ya miaka 15 ambayo ameiwakilisha Vatican katika nchi mbalimbali Afrika.

Ikulu imetoa nembo rasmi za Miaka 50 ya Uhuru

Viongozi wa NTC ya Libya kutua Dar Oktoba

Bernard Membe
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe amesema uongozi wa Baraza la Mpito la Libya (NTC) unatarajiwa kutembelea Tanzania wakati wowote mwenzi Oktoba.

Membe amesema, wakiwa nchini viongozi hao watafanya mazungumzo na Rais Jakaya Kikwete juu ya mipango yao ya kuijenga upya nchi ya Libya.

Kilombero: Mvua ni raha na karaha

Wakati msimu wa mvua unaanza, Kilombero ni raha na karaha. Raha kwa kua kilimo kinakubali sana lakini karaha kwa kua barabara hua hazipitiki. Pichani ni barabara inayounganisha Mji wa Ifakara na Kata ya Mbingu, Kilombero.

Kilombero hua hivi wakati wa mvua.


Mbowe: Udini ni hatari

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ameonya juu ya kuigawa nchi katika misingi ya kiimani, akisema kwamba madhara yake ni makubwa kwa mustakbali wa taifa letu.

Freeman Mbowe
 Angalizo hilo la Mbowe ambalo alilitoa Igunga jana kwenye mfululizo wa kampeni za chama chake huenda limewalenga viongozi wa dini ya Kiislamu ambao wamekua wakiwataka wafuasi wa dini hiyo wasiwapigie kura Chadema kwa kile kinachodaiwa kua chama hicho kimemdhalilisha na kumvua hijabu Mkuu wa Wilaya ya Igunga, Fatma Kimario.

Helikopta kivutio Igunga

Taarifa mbali mbali zilizorushwa na luninga za hapa nchini zimethihirisha ukweli kwamba helikopta ni kivutio kikubwa kwa wananchi na pengine ni msaada mkubwa kwa wagombea kwa kua wanapata fursa ya kuwahutubia wapiga kura wengi kwa wakati mmoja.


Hamasa za Helikopta Igunga
 "Hakuna haja ya kutangaza, wanakuja wenyewe" alisema Noel Mwakalindile mtangazaji wa TBC1 baada ya helikopta ya CUF kutua Igunga mjini na punde ikazingirwa na wananchi kibao kutoka sehemu mbalimbali.

Wednesday, 28 September 2011

Weusi wanabakwa na kuchinjwa kama kuku Libya

Ikiwa ni muda mfupi tangu waasi wa Libya wajigambe kuutwaa mji mkuu wa nchi hiyo-Tripol, tayari vitendo vya kinyama kwa watu weusi (wasio waarabu) vimeripotiwa kushika kasi.

Baathi ya wachambuzi wanajiuliza iweje mapinduzi yaliyokusudiwa kuwakomboa wanyonge (kama wanavyodai waasi) yaishie katika unyama wa kuwabaka na kuwachinja wanyonge?
Kiongozi wa Baraza la Mpito la Libyan (NTC) Mustafa Abdul Jalil
Weusi hao ambao walikimbilia Libya kutafuta maisha mazuri wakati wa Gadafi na wengine wakitafuta njia ya kuendea Ulaya, waliishi kwa furaha na amani chini ya utawala wa Gadafi lakini sasa wanakiona cha moto.

Iweje Waafrika wabaguliwe Afrika na hakuna mtu wa kuwasemea?, viongozi wa Umoja wa Afrika (AU) kwanini wanalifumbia macho suala hili?

Igunga: Kampeni za Jimbo kwa helikopta?

CHADEMA
CCM    




Vilio viwili vikuu Igunga.


Daraja la Mbutu.


Uhaba wa maji.








Tuesday, 27 September 2011

Siasa ni maendeleo ya watu


Seneta wa zamani wa Jimbo la Minnesota, Marekani, Bw Paul David Wellstone aliwahi kunukuliwa akisema, “Siasa ni maendeleo ya maisha ya watu, ni kufanya vizuri kwa ajili ya watu”.



                                                          Paul David Wellstone 
                                               (Julai 21, 1944 – Octoba 25, 2002)



Matamshi ya Wellstone yanaashiria kwamba hali ya maisha ya mwanadamu (mabaya au mazuri) inatokana na mwenendo mzima wa siasa za nchi husika.

Kwenye nukuu nyingine anasema “Siasa ambazo hazijali maisha ya watu, ambazo hazizungumzii watu ni siasa za kipuuzi ambazo ni lazima zishindwe”.

Hebu tujiulize kama nchi tuko wapi?

Igunga: Mwisho wa ubaya aibu.




                                            Mwl Joseph Kashindye


Wahenga walisema mwisho wa ubaya ni aibu, haya yanathihirika kila uchao haswa kwenye maisha ya wanasiasa kwa kua siasa za kileo hapa kwetu zimetawaliwa na fitna na kupakazana matope.

Msemo huo wa wahenga umejithihirisha waziwazi juzi kwenye mdahalo wa wagombea wa kiti cha Ubunge kwenye Jimbo la Igunga lililoachwa wazi kufuatia kujiuzulu kwa Rostam Azizi (CCM) aliyeongoza jimbo hilo tangu mwaka 1994.

Mdahalo huo ambao uliwaleta pamoja wagombea, Dr Dalaly Kafumu (CCM), Leopold Mahona (CUF) na Joseph Kashindye (Chadema) uligeuka shubiri kwa wagombea wa CCM na Chadema.

Wagombea hao walijikuta wakiwekwa kikaangoni na mgombea wa CUF ambaye tofauti na wenzake hajawahi kufanya kazi serikalini.

Bwana Mahona aliwatupia wenzake lawama kwamba matatizo ya Igunga yametokana kwa kiasi fulani na ubadhirifu wa viongozi wa serikali wakiwemo wao ambapo Kashindye alikua Mkaguzi wa Shule kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Igunga na Kafumu alikua Kamishna wa Madini kwenye Wizara ya Nishati na Madini.

Nani angefikiria kwamba Kashindye ambaye chama chake kinaongoza kwa kuwashutumu viongozi wa serikali kua ni mafisadi angekutwa katika wakati mgumu kiasi cha kuanza kujitetea kwenye mdahalo? 

Mwisho wa ubaya………………………………