Sunday, 16 October 2011

Thursday, 13 October 2011

IKULU: JK HAKUTOA MSAMAHA KWA WALIO MUUA LUTEN JENERAL IMRAN KOMBE

Rais Jakaya Kikwete
Gazeti la Mwananchi, matoleo ya jana, Jumatano, Oktoba 12 na leo, Alhamisi, Oktoba 13, 2011, limeandika habari zilizodai kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete alitoa msamaha wa kupunguza adhabu ya kifo iliyowakabili askari polisi wa zamani waliopatikana na hatia ya kumpiga risasi na kumwua kwa makusudi aliyepata kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa, Luteni Jenerali Imran Kombe Juni 30, 1996.
 Gazeti hili limedai kuwa Mheshimiwa Rais Kikwete alitoa msamaha huo kwa kupunguza adhabu ya kifo iliyokuwa inawakabili makonstebo wapelelezi Mataba Matiku na Juma Muswa na kuibadilisha kuwa kifungo cha miaka miwili.
 Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, inapenda kufafanua kuwa Mheshimiwa Rais Kikwete hajawahi na hajapata kuhusika hata kidogo kutoa msamaha wa kirais kwa kupunguza adhabu ya wauaji hao wa Luteni Jenerali Kombe tokea kuingia madarakani.
 Masuala yote yanayohusu polisi hao waliohukumiwa kifo kwa mauaji ya Luteni Jenerali Kombe yalifanyiwa maamuzi kabla ya Rais Kikwete kuingia madarakani Desemba 21, 2005.

Wednesday, 12 October 2011

KIKWETE KUUNGA MIKOA YOTE KWENYE GRIDI YA TAIFA

Rais Jakaya Kikwete
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete leo, Jumatano, Oktoba 12, 2011, amepokea ripoti kutoka makampuni mawili ya kimataifa kuhusu Mpango Kabambe ya mradi mkubwa wa umeme ambao utaunganisha kwenye Gridi ya Taifa mikoa yote sita ambayo kwa sasa haiko kwenye gridi hiyo.
 Rais Kikwete amepokea ripoti hiyo kutoka makampuni ya China National Machinery&Equipment Import&Export Corporation (CMEC) ya China na Siemens ya Ujerumani ambayo kwa pamoja yanatarajia kujenga kituo kikubwa cha kuzalisha umeme kutokana na gesi katika eneo la Mnazi Bay, mjini Mtwara na pia kujenga njia ya kusafirisha umeme ya kilomita 1,100 kutoka Mtwara hadi Singida.
 Mradi huo mkubwa wa umeme wa megawati 300 utakaogharimu karibu dola za Marekani milioni 684 na utakaozalisha umeme wa moja kwa moja na wenye nguvu kubwa ya 300 kV (300 kV High Voltage Direct Current – HVDC) utagharimiwa kwa pamoja na mkopo kutoka Benki ya Exim ya China na Serikali ya Tanzania.
Umeme kutokana na mradi huo utaunganishwa kwenye gridi ya taifa na kutoka Singida hatimaye utavutwa kupelekwa katika mikoa ya Kaskazini Magharibi mwa Tanzania ya Kagera, Kigoma na Rukwa ambako pia utaongeza upatikanaji wa umeme katika machimbo ya madini yaliyoko katika mikoa hiyo.
 Kwa mujibu wa ripoti hiyo, mbali na mikoa hiyo mitatu, pia mikoa ya Lindi na Mtwara ambayo nayo haiko katika Gridi ya Taifa nayo itaunganishwa katika Gridi hiyo kupitia umeme huo.
 Kuunganishwa kwa mikoa hiyo sita katika Gridi ya Taifa kupitia umeme wa mradi huo pamoja na Mkoa wa Ruvuma ambao utaunganishwa katika Gridi hiyo kwa mradi unaogharimiwa na Serikali ya Sweden kutakamilisha mpango wa Serikali ya Awamu ya Nne kuunganisha mikoa yote ya Tanzania kwenye umeme wa Gridi ya Taifa.
 Kwa sasa Mkoa wa Kagera unahudumiwa na umeme kutoka Uganda, wakati Mikoa ya Kigoma na Rukwa inahudumiwa na umeme wa mafuta ya dizeli. Mikoa ya Mtwara na Lindi inapata umeme wake kutoka kampuni ya Wentworth ambao haujaunganishwa kwenye gridi ya taifa.
 Kuunganisha mikoa yote ya Tanzania kwenye Gridi ya Taifa ilikuwa moja ya ahadi kubwa zilizotolewa na Serikali ya Rais Kikwete wakati anaingia maradakani na kwa kuuunganisha mikoa hiyo sita kwenye Gridi hiyo, Serikali hiyo itakuwa imetimimiza ahadi hiyo.
Akipokea ripoti hiyo, Rais Kikwete ameishukuru Wizara ya Fedha, Wizara ya Nishati na Madini pamoja na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa juhudi zao zilizofanikisha makubaliano ya kujengwa kwa mradi huo mkubwa wa umeme ambao utachangia kuongeza wingi wa umeme nchini katika kipindi ambacho kwa miezi kadhaa Tanzania imekabiliwa na mgawo wa umeme kutokana na ukame uliokausha maji kwenye mabwawa makubwa ya uzalishaji umeme nchini.
Rais Kikwete pia ameitaka Wizara ya Fedha kwa kushirikiana na Benki ya EXIM ya China kuhakikisha kuwa fedha za kutekeleza mradi huo zinapatikana haraka iwezekanavyo na pia ameitaka TANESCO na makampuni ya CMEC na Siemens baada ya kupatikana kwa fedha kuanza ujenzi wa mradi huo kwa kasi na kuukamilisha katika muda na ubora unaotarajiwa.

(Imetolewa na IKULU)

NAPE ALIA NA WANAOBEZA DHANA YA "KUJIVUA GAMBA"

Nape Nnauye
Kumekuwepo na juhudi za muda mrefu sasa kutaka kupotosha au hata kushawishi kubadili kabisa maamuzi ya Chama juu ya dhana nzima ya kufanya mageuzi ndani ya Chama (KUJIVUA GAMBA).
Juhudi hizi zimekuwa zikifanywa na kikundi kidogo sana cha watu wachache ambao kwa namna moja ama nyingine wameathiri wanamageuzi haya tunayoyafanya.
Tatizo kakikundi kenyewe kana nguvu kiasi ya pesa jambo linalofanya kelele zao ziwe kubwa lakini zisizo na mashiko.
Juhudi hizi za kujaribu kuhujumu mageuzi haya ndani ya chama zimekuwepo kwa muda mrefu sasa na tumejitahidi sana kuzipuuza, lakini nadhani umefika wakati wana CCM na Watanzania kujua ukweli walau kwa kiasi ya kinachoendelea.
Wanaofanya juhudi hizi wanadhani hatuzifahamu kwa sababu tu tumekaa kimya wakati wakicheza sarakasi zao za kujaribu kuupotosha umma.
Chama tunafahamu na kufuatilia kwa makini kila kinachoendelea hakuna tusichokijua juu ya juhudi hizi na zingine nyingi zikiwemo jitihada za kutaka kumhujumu hata Mwenyekiti mwenyewe. Nasisitiza tunazifahamu.
Juhudi za hivi karibu ni zilikuwa za kutaka Chama kishindwe Igunga ili kujaribu kuhalalisha hoja ya kwamba mageuzi tuyafanyayo hayana tija kwa Chama. Juhudi hizi zilifanyika bila kificho, tunajua hazikuwa na nia njema kwa Chama ila zilisukumwa na uroho na ubinafsi zikiwa na ujasiri mkubwa wa kifisadi, bila kujali masilahi mapana ya Chama kama taasisi na nchi yetu kwa ujumla.
Baada ya kushindwa kwa juhudi hizo Igunga, sasa wanaanza kujaribu kutumia watu mbalimbali kuimba wimbo wao wa zamani kuwa tunapotosha dhana ya kujivua gamba bila kusema usahihi ni upi kama tunachokifanya ni kupotosha. Ikumbukwe huu sio wimbo mpya uliimbwa sana mara tu baada ya kutangaza maamuzi ya NEC.
Bahati nzuri vimeshakaa vikao vya Kamati Kuu karibu mara mbili, ambavyo vyote vimepongeza utekelezaji wa haya mageuzi ndani ya chama. Mapema mwaka huu Baraza Kuu la UVCCM Taifa chini ya Uenyekiti wa Makamu Mwenyekiti wa UVCCM Taifa katika taarifa yake kwa vyombo vya habari walipongeza utekelezaji wa maazimio ya NEC.
Sasa pengine tujiulize kama wana CCM na Watanzania kwa ujumla hawa wanaodai tunapotosha maamuzi ya NEC ni kina nani na kwa masilahi ya nani?
Naendelea kusisitiza hakuna kilichopotoshwa. Ushindi wa Igunga kwenye uchaguzi mdogo, pamoja na ule wa chaguzi ndogo za Udiwani kwenye kata kumi na saba kati ya ishirini na mbili zilizofanya uchaguzi ni uthibitisho wa kukubalika kwa mageuzi tuyafanyao. Nachukua nafasi hii kuwashukuru sana wa na CCM nawananchikwaujumlakuungamkonomageuzituyafanyayokwaniMwalimualishatuasa “BILA CCM MADHUBUTI NCHI YETU ITAYUMBA”
Walikwenda na kaulimbiu Igunga “TUSHINDWE ILI TUHESHIMIANE” wakasahau kuwa Chama ni taasisi si mtu, ushindi ule Igunga na kwenye kata mbalimbali ni Ushindi wa wana CCM na wapenda nchi hii wote! …Hivyo basi “TUMESHINDA ILI TUHESHIMIANE” Bahati mbaya kwao hawa kutegemea kutokea yaliyotokea. Nawasihi wasiweweseke watulie na kutafakari upya wayafanyayo huku wakikumbuka…HAKUNA TUSICHOKUJUA.
Nichukue nafasi hii kuwaomba wana CCM nchi nzima kutulia na kuzipuuza juhudi hizi kwani tukifanyacho ni kwa masilahi mapana ya Chama chetu na nchi yetu, hakuna sababu ya kutiwa hofu, kila kitu kiko salama. SABABU YA KUSHINDA TUNAYO, NIA YA KUSHINDA TUNAYO NA UWEZO WA KUSHINDA TUNAO.
Malengo mengine makubwa waliyo kuwa nayo kupitia kushindwa kwa CCM Igunga kama kungetokea ili kuwa kuipa nguvu kampeni yao kubwa na ya muda mrefu ya kujaribu kujenga hoja ya kutenganisha Uenyekiti waTaifa wa CCM na Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Bahati mbaya kwao na wapambe wao mambo yamekwenda kinyume na dua zao. Changa moto ni nayo itoa kwao, kwa nini wasitoke wenyewe kutoa madai wayatoayo hadharani badala yake wanatumia watu? Hii hoja ya kutenganisha kofia kama ina masilahi kwa chama nasi kwa kikundi kidogo kwa nini wanatumia nguvu ya pesa kutaka kushawishi wajumbe? Anayeamini kwa nini asiilete kikaoni bila kushawishi watu kwa pesa?
Mwenendo wa siasa nchini unadhihirisha kuwa upinzani hauna nguvu kiasi hicho ila unapata nguvu ndogo waliyo nayo kutoka kwa kikundi hiki kidogo sana cha Wanaojiita wana CCM lakini kwa kweli ni waasi. Wengi wao walianza kwa kuasi Imani ya CCM na sasa wana endesha kampeni ya watu kuasi maamuzi halali ya vikao halali vya Chama chetu. Naomba
niwakumbushe TULIAMUA, TUKAAHIDI NA TUTATEKELEZA HAKUNA KINACHOBADILIKA KWA SARAKASI ZA BARABARANI, WANAPOTEZA MUDA.
Yaliyobaki yanayofanywa na wapambe na wanaotaka kutumiwa ya kimaadili tutayashughulikia kwenye vikao. Chama cha siasa makini ni vikao.
Ahsanteni kwa kunisikiliza.
Imetolewa na:-
Nape Nnauye
KATIBU WA HALMASHAURI KUU YA TAIFA
ITIKADI NA UENEZI
12/10/2011

WARIOBA: ACHENI KAMPENI ZA UCHAGUZI ZISIZO NA KIKOMO


Warioba

Waziri Mkuu Mstaafu, Jaji Joseph Warioba ameonya dhidi ya kampeni zisizoisha, akasisitiza kwamba chaguzi zimemalizika na huu ni wakati wa kuleta maendeleo bila kujali itikadi za vyama.
Amesema hayo leo jana Jijini Dar es Salaam mara baada ya kutembelea mabanda ya maonesho yaliyoandaliwa na Ofisi ya Waziri Mkuu kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara.
 Alisema vyama vya siasa havina budi kujifunza kushindanisha sera ili wananchi waweze kuchagua chama ambacho wanaona sera zake zinafaa na siyo kushindana kwa maneno tu.
 “Sasa hivi ukitazama magazeti ya kila siku, sote tunazungumzia siasa tupu… ni lazima tutambue kuwa tukimaliza uchaguzi, tunaingia katika shughuli za kuleta maendeleo, tujiepushe na kampeni za uchaguzi zisizoisha,” aliongeza.
 Alisema vyama vya siasa havina budi pia kuhakikisha kuwa vinaimarisha demokrasia nchini na ndani ya vyama vyenyewe na kuongeza kwamba: “Demokrasia ni pamoja na kutofautiana mawazo bila kupigana.”
 Alisema kama kuna suala linaisumbua nchi, kuna haja ya kukaa pamoja na kutafuta njia mbadala kwa maslahi ya Taifa. “Sisi na kundi jingine hatuna budi tukae pamoja na kujiuliza ni nini cha kufanya ili tusonge mbele... na hapa nataka kusisitiza kuwa kila awamu ilikuwa na matatizo yake, hakuna wakati ambapo nchi yetu haikuwa na matatizo lakini tulikaa pamoja na kutafuta ufumbuzi,” alisema.
 Akifafanua zaidi, Jaji Warioba alisema katika awamu ya kwanza kulikuwa na uasi wa jeshi, vita vya kumng’oa nduli Iddi Amin, kulikuwa na msukosuko wa kiuchumi baada ya kuvunjika kwa jumuiya ya Afrika Mashariki lakini yote yalitatuliwa na nchi ikasonga mbele.
 “Mimi nilipoingia madarakani (1985-1990) wakati wa awamu ya pili chini ya Mzee Ali Hassan Mwinyi, nchi haikuwa na bidhaa madukani kwa sababu tulikuwa hatuna fedha za kigeni za kutosha kuagiza bidhaa nje ya nchi; nchi ilikumbwa na baa la njaa lakini tulimaliza tatizo la njaa, tukazalisha kwa wingi zaidi mpaka ikabidi tuanze kujenga maghala kwa ajili ya kuhifadhi chakula cha ziada,” alisema.
 “Tulitumia umoja wa nchi yetu kutatua matatizo yaliyoikumba nchi na mara tatizo lilipotokea hatukunyoosha kidole kwa mtu mmoja… lilikuwa ni tatizo la wote.”
Alisisitiza haja ya kuilinda misingi ya umoja wa kitaifa na kutambua juhudi za kuleta maendeleo lakini akaongeza kuwa kuwa kuna haja ya kuangalia changamoto zinazojitokeza na kuainisha njia za kukabiliana nazo.
 (Kwa hisani ya PMO)

WACHAGA WASHAURIWA KUHAMIA MIKOA MINGINE YENYE ARDHI KUBWA

  
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama (wa pili kushoto) akiwa na Mkuu wa wilaya ya Siha, Anna Nyamubi walipotembela Kambi ya “Ndarakwai Camp” katika hifafadhi ya msitu wa wanyamapori na mifugo wa North Kilimanjaro wilayani Siha. Wengine ni wataalam kutoka halmashauri ya wilaya ya Siha.

 Wananchi wa kijiji cha Ngarenairobi Wilaya Siha, Kilimanjaro  wameahidiwa kutafutiwa ardhi ya kilimo katika mikoa mingine endapo watakuwa tayari kuhama katika eneo la kijiji hicho kinachakabiliwa na uhaba wa ardhi ya makazi na kilimo.

Ahadi hiyo imetolewa jana na mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro Mheshimiwa Leonidas Gama alipotembelea kijiji hicho ikiwa ni sehemu ya ziara yake katika wilaya ya Siha yenye lengo la kuufahamu mkoa na kutaka kujionea mafanikio na changamoto zinazowakabili wananchi hasa wa vijijini katika mkoa wa Kilimanjaro.

Akijibu swali la mwanakijiji aliyejitambulisha kwa jina la Rashid salim ambaye alimuomba mkuu wa mkoa awasaidie waweze kuongezwa ardhi kutoka sehemu ya shamba la mradi wa ufugaji la  West Kilimanjaro lilinalomilikiwa na Shirika la Ranchi za Taifa  (NARCO) Mheshimiwa Gama amesema eneo hilo ni maaalum kwa ajili ya wanyama na endapo wataona ardhi waliyopewa kwa ajili ya makazi haitawatosha ni vema wengine wakapungua kwa kutafuta ardhi katika mikoa mingine ambayo bado ina ardhi ya kutosha.

Halmashauri ya wilaya ya Siha tayari imeshaanza mchakato wa kuirasimisha sehemu ya ardhi waliyopewa wanakijiji hao kwa ajili ya makazi lakini ardhi hiyo haitatosha kwa shughuli za kilimo kutokana na ufinyu wa ardhi hiyo.

Aidha Gama amewaeleza kuwa eneo hilo ni sehemu ya mapitio ya wanyama pori wanaotokea katika hifadhi za nchi jirani ya Kenya na kuingia katika hifadhi ya wanyama pori ya Arusha na kuwaelimisha kuwa kuna sheria zinazowalinda wanyama pori wanapokuwa katika shughuli zao na kijitafutia chakula na maji kwa mujibu wa mahitaji yao.

Kuhusu Magendo ya Sukari na Nafaka.

Kuhusu tatizo la uvushwaji wa nafaka na sukari kwa njia za magendo Mheshimiwa Gama amewataka wananchi hao ambao wanaishi jirani mpaka wa Tanzania na nchi jirani ya Kenya kutoa taafa kwa vyombo husika na zawadi itatolewa kwa mwananchi yeyote atayefanikisha kukamatwa kwa shehena ya magendo katika eneo hilo.

Mbali hilo aliwaahidi wanakijiji hao kuwa endapo watafanikiwa kutoa taarifa hizo na mzigo wa magendo kukamatwa  chakula hicho kitauzwa kwa bei nafuu kwa wananchi wa kijiji hicho ili wanufaike na uzalendo wao.

(Kwa hisani ya Mdau, Shaaban wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Kilimanjaro)


Warioba: ACHENI KULALAMIKA, FANYENI KAZI

Warioba
Waziri Mkuu Mstaafu, Jaji Joseph Warioba amesifu jitihada zilizofanywa na Serikali katika kuleta maendeleo nchini lakini amewaonya Watanzania waache tabia ya kulalamikia kila jambo na badala yake wafanye kazi.
 Ametoa kauli hiyo leo mchana (Jumanne, Oktoba 11, 2011) wakati akijibu maswali ya waandishi wa habari mara baada ya kutembelea mabanda ya maonesho yaliyoandaliwa na Ofisi ya Waziri Mkuu kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara.
 Amesema kuna mambo mengi ambayo yamefanyika tangu nchi ipate uhuru lakini hakuna anayetambua mchango huo na badala yale kila mmoja amekuwa mwepesi wa kutoa lawama. “Kuna kitu kimoja kinachonipa matatizo nacho ni kuona nchi imekuwa ni ya watu waliokata tamaa… wananchi na viongozi ni watu wa kulalamika tu, sisi sote ni walalamikaji,” alisema mbele ya waandishi hao.
 “Kwa hali ilivyo, nasema tujihadhari kwa sababu tunaweza kupata matatizo ya kiuchumi kwa sababu ya matatizo ya umeme, bei kubwa ya mafuta na kushuka kwa thamani ya shilingi. Kama shilingi itaendelea kushuka, mfumuko wa bei utakuwa mkubwa na atakayeumia ni mwananchi wa kawaida,” alibainisha.
 Alisema kazi ya kutafuta uhuru ilikuwa ngumu na kulikuwa na baadhi ya watu walioamini kuwa Tanganyika isingepata uhuru wake kwa sababu kazi ya kumtoa Mwingereza haikuwa rahisi. “Mimi ni mmoja wa watu waliokuwepo uwanjani kushuhudia bendera ya Mwingereza ikishusha na kuona bendera ya Tanganyika ikipandishwa.”
 “Jeuri tuliyokuwa nayo wakati wa harakati za kutafuta uhuru ilikuwa kubwa… dhamira tuliyokuwa nayo ibaki vilevile, tuwe ni watu wa kuthubutu. Kama tuliweza wakati ule, tukiwa hatuna hatuna teknolojia za kisasa kama sasa, naamini hakuna kitu kinachoweza kuturudisha nyuma,” alisisitiza.
 Alisema umefika wakati wa wananchi kukaa pamoja na kujadili changamoto zinazolikabili Taifa na kukubali kuwa matatizo siku zote yapo. “Matatizo ni sehemu ya maisha, ukithubutu kuyapatia ufumbuzi unaweza kupata suluhu ya matatizo hayo. Maonesho haya yanatukumbusha jinsi tulivyoweza kuthubutu, yanatukumbusha tulikotoka,” alisisitiza.
(Kwa hisani ya Ofisi ya Waziri Mkuu)

Friday, 7 October 2011

TEMBO KUDHIBITIWA ROMBO

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama
Serikali Mkoani Kilimanjaro imewaahidi wananchi wa Wilaya ya Rombo kuwa tatizo la mgogoro kati ya binadamu na wanyama pori hususani tembo  ambalo limekuwapo wilayani humo kwa muda mrefu litapatiwa ufumbuzi wa kudumu ili kuhakikisa usalama wa raia wa wilaya hiyo na mali zao.

Ahadi hiyo imetolewa leo na Mkuu wa mkoa wa kilimajaro Mheshimiwa Leonidas Gama alipokuwa katika ziara ya kikazi katika kituo cha kudhibiti uharibifu wa wanyamapori kalichopo katika kijiji cha Ngoyoni katia tarafa ya Mengwe wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro.

Tayari serikali Mkoani Kilimanjaro kwa kushirikiana na Kikosi cha Kupambana na Ujangili kutoka Mkoa wa Arusha  imejenga kituo cha kuzuia wanyamapori aina ya tembo katika kijiji cha Ngoyoni ambacho kitasaidia madhara ya wanyama hao kwa binadamu bila ya kuwaua au kuwadhuru wanyama hao kwa namna yoyote.

Ili kuhakikisha kuwa mradi huo ambao ujenzi wake umeshatekelezwa kwa kiasi kikubwa unakamilika mapema iwezekanavyo Mheshimiwa Gama amesema atawaita wahusika ofisini kwake ili ajue ni kwa nini kasi ya utekelezaji wa kituo hicho imekuwa ndogo.

”Sijaridhishwa na kasi ya utekelezaji wa mradi huu kwani naona imekuwa ndogo ikilinganishwa na umuhimu wa mradi wenyewe” alisisitiza Mheshimiwa Gama.

 Mheshimiwa gama alitoa ahadi hiyo mara baada ya kupokea taarifa iliyowasilishwa kwake na uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Rombo ambayo imeeleza kuwa kuanzia mwaka 1992 hadi sasa matukio ya uharibifu mkubwa wa mazao,makazi pamoja kupoteza maisha kwa baadhi ya wananchi  yamekuwa yakitokea.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo maeneo yaliyopata madhara makubwa ya wanyamapori hao ni pamoja na Holili, Mamsela Chini,,Shimbi, Ibukoni,,Msaranga,Kirongo chini na hifadhi ya misitu ya Rongai.

Mbali na hilo Mheshimiwa Gama amewapongeza wananchi wa kijiji cha ngoyoni kwa moyo wa kujitolea katika kutekeleza miradadi ya maeneleo kwa kuchangia ardhi yenye ukubwa wa eneo upatao heka moja na robo kwa ajili ya mradi wa kujenga kituo cha hicho cha kudhibiti uharibifu wa mali,makazi na mazao unaofanywa na wanyamapori hao.

Akitoa ufafanuzi wa namana mgogoro huo baina ya binadamu na wanyamapori Mkuu wa wilaya ya Rombo Mheshimiwa Peter Toima Kiroya amesema kuwa Wilaya ya Rombo ipo katikati ya hifadhi za wanyamapori hivyo basi, njia wanazopita tembo hao ambao hutokea katika hifadhi za  nchi jirani ya Kenya na kuingia katika Hifadhi ya Taifa ya Kilimanjaro (KINAPA) ni njia zao za asili zilizokuwepo tangu zamani.

Aiha Mheshimiwa Kiroya amesema kuwa takika kipindi cha miaka 30 iliyopita binadamu wameongezeka na kujikuta wanalima na kujenga katika njia za wanyama hao jambo ambalo limesababisha kuwepo kwa mgogoro huo wakati tembo hao wanapotaka kupita katika njia zao zao hizo kwa ajili ya kujitafutia chakula na maji.

 (Habari kwa hisani ya Mdau Shaaban wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Kilimanjaro)

Thursday, 6 October 2011

NAPE SWALI LA IGUNGA NI GUMU, USITOE MAJIBU MEPESI

Katibu wa Halmashari Kuu ya Taifa ya CCM (Itikadi na Uenezi) Bw Nape Nnauye
Chama cha Mapinduzi CCM kimeibuka na ushindi (sio wa kishindo) kwenye uchaguzi uliofanyika Jumapili ya wiki iliyopita huko Igunga na tayari kimetamba kwamba ushindi huo ni ishara ya kukubalika kwa mageuzi ndani ya chama.

Katibu wa Halmashari Kuu ya Taifa ya CCM (Itikadi na Uenezi) Bw Nape Nnauye alinukuliwa akisema kwamba ushindi wa Igunga na ushindi katika kata 77 ni ishara kwamba mabadiliko ndani ya chama yanakubalika.
Bendera ya CCM
Pengine Nape anasema ukweli kuhusu kata 77, lakini tukirudi Igunga kauli yake haina ukweli. Hii inatokana na ukweli kwamba nguvu ya CCM Igunga imepungua sana kwa matokeo ya uchaguzi huu.
Kweli ushindi ni ushindi, lakini kama alama ya chini ya kufaulu ni tano na wewe umezoea kupata kumi, siku ukipata saba huwezi kujisifu, utakachotakiwa kufanya nikukaa na kujiuliza juu ya alama tatu ulizopoteza kwa kua kuna uwezekano kwamba mtihani ujao zitapungua zaidi.
Kama Nape haoni tatizo Igunga basi anakataa tu lakini ukweli ni kwamba kitendo cha chama ambacho hakina historia inayoeleweka kwenye Jimbo la Igunga kuibuka wakati wa uchaguzi na kuvuna kura 23,360 dhidi ya kura 26,488 za CCM sio jambo la kujisifu.

Mbunge wa Igunga, Dk Dalaly Kafumu

Lazima ikumbukwe kwamba ni sera mpya za CCM na uongozi wa Nape ambao kwa kiasi kikubwa ulimfanya Rostam Aziz aliyekua mbunge wa Igunga kujiuzulu wadhifa wake, sasa ikiwa wananchi walifurahishwa na hatua hiyo mbona kura zimepungua kutoka zaidi ya elfu 30 mpaka 26 elfu?
Ukweli ni kwamba CCM imepunguza umaarufu wake Igunga kwa kiasi kikubwa na kama chama ipo haja ya kuweka nguvu zaidi kukijenga badala ya kubweteka na kujisifu wakati mtaji unaporomoka.

Wednesday, 5 October 2011

KIKWETE MGENI RASMI MKUTANO WA UWEKEZAJI RUKWA

Mkutano wa uwekezaji wa ukanda wa Ziwa Tanganyika mikoa ya Katavi, Kigoma na Rukwa utafanyika Wilayani Mpanda Mkoani Rukwa tarehe 17 Oktoba 2011 katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpanda, Mpanda mjini.
Mgeni rasmi katika mkutano huo atakuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete. Wageni wengine maarufu watakaokuwepo ni Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Mizengo Pinda, Mabalozi, Mawaziri, wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi na wadau wengine wa uwekezaji.
Rais Jakaya Kikwete (Kulia) na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.
Lengo la mkutano huo ni kuzinadi fursa nyingi za uwekezaji zilizopo katika Ukanda wa Uwekezaji wa Ziwa Tanganyika na kufungua ukanda huo ambao kwa mda mrefu ulikabiliwa na miundombinu mibovu hivyo kuwa vigumu kufikika.
Fursa hizo ni Madini, ardhi yenye rutuba inayofaa kwa kilimo, utalii (Kalambo Falls, Bismark Fort, Mv Liemba, Mbuga ya Katavi na Gombe Kigoma), biashara, miundombinu, elimu, afya na ufugaji.

Kwa kufungua ukanda huu itaongeza ajira kwa wananchi wa ukanda huo na hivyo kuinua uchumi wa Mtanzania.
Serikali ya Tanzania imeshachukua hatua ya kufungua ukanda huu kwa kuimarisha miundombinu ya barabara za lami, umeme, reli, viwanja vya ndege na usafiri katika Ziwa Tanganyika.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Eng Stella Manynya

Barabara ya Tunduma-Laela-Sumbawanga inajengwa kwa kiwango cha lami. Barabara ya Sumbawanga-Kasanga, Sumbawanga Mpanda nayo pia inajengwa kwa kiwango cha lami, miradi yote hii itakamila ifikapo mwaka 2013.
Kongamano hilo la uwekezaji litakuwa la aina yake kwani litaambatana na maonyesho ya siku nne kuanzia tarehe 15-18 mwenzi huu wa Oktoba ambapo wajasiriamali, wawekezaji na taasisi za Serikali watapata fursa ya kunadi sera zao, bidhaa na mipango mbalimbali kupitia mabanda.
Siku ya kongamano lenyewe tarehe 17 Oktoba 2011 kutakuwa na mijadala mbalimbali ambayo itaambatana na kila wilaya katika mikoa hii mitatu (Katavi, Kigoma na Rukwa) kuweza kunadi miradi yake ambayo inahitaji uwekezaji.
(Kwa hisani ya Mdau, Temba wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Rukwa)

MARUFUKU KUEGESHA MALORI HIMO

Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama amepiga marufuku uegeshwaji wa malori  yaliyobeba bidhaa za nafakaka yakiwemo mahindi pamoja na sukari katika eneo la mji mdogo wa Himo katika wilaya ya Rombo Mkoani  Kilimanjaro ili kudhibiti utoroshaji wa bidhaa hizo kwenda nchi jirani ya Kenya.

Gama amesema hayo katika kikao chake na watumishi wa halmashauri ya wilaya ya Rombo alipofanya ziara ya kikazi katika halmashauri ikiwa ni sehemu ya ziara zake alizojiwekea katika kujua changamoto zinazowakabili wananchi na kupanga vipaumbele vya kimaendeleo katika kuwawezesha wananchi kujiletea maendeleo.

Katika utekelezaji wa agizo hilo Gama amewataka watumishi wote wa umma kuwa waadilifu na waaminifu kwa serikali ili kukomesha kabisa biashara za magendo katika mkoa wa Kilimanjaro hasa katika mipaka na nchi jirani ya Kenya.

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Mh Leonidas Gama akiwa na Waziri wa Nchi OWM -TAMISEMI Kapteni Mstaafu George Mkuchika (Katikati) wa pili kulia ni mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Rombo walipotembelea Kijiji cha Mengwe kata ya Mengwe wilaya ya Rombo.

Kuhusu suala la utii wa  sheria  Gama ameonya tabia ya baadhi ya  wananchi na wafanyabiashara kudharau na kukaidi amri halali za mamlaka na viongzi wa nchi ambazo zitambulika kisheria kuwa hatakuwa tayari kuwafumbia macho na kuwaonea  aibu watu  wenye tabia hizo.

Aidha Mkuu huyo mpya wa mkoa aliwakumbusha watumishi wote wa umma kuwa majukumu ya watumishi wa umma  ni kusaidia kupatikana kwa maendeleo ya wananchi na hivyo basi  hawana hiyari katika kuhakikisha kuwa wanakuwa waadirifu kwa kutumia vizuri ofisi za serikali kwa kuwepo katika maeneo ya kazi katika nyakati za kazi, hawapokei wala kutoa rushwa pamoja na kutimiza wajibu kwa wakati.

Bwana Gama amesema kuwa tuhuma za kushiriki biashara za magendo kwa watumishi wa umma ni moja ya mambo yanayomkera na ni ya aibu kwa serikali na hatakuwa tayari kuvumilia uovu huo katika mkoa wa anaouongoza. “ Nikilazimika kumuondoa mtu katika nafasi ya kiutumishi aliyonayo nitafanya hivyo” alisisitiza.

( Picha na Habari kwa hisani ya Mdau, Shaban Pazi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa)