|
JAIRO |
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, David Jairo aliyekuwa anatuhumiwa kwa shutuma za kuchangisha fedha kwa ajili ya kupitisha bajeti ya wizara yake (2011/2012) amepata mridhi wa nafasi yake.
Wakati huohuo, Katibu Mkuu Kiongozi Philemoni Luhanjo naye amepata mrithi wa nafasi yake. Luhanjo naye alituhumiwa kumbeba Jairo na kulidharau Bunge pale alipojaribu kumrudisha kazini Bwana Jairo katika hali ya utata.
Hii inakuja muda mfupi baada ya Bunge kupitisha maadhimio kwamba, Jairo na Luhanjo walikuwa na makosa kwa kitendo hicho cha kuchangisha fedha kutoka kwenye idara na taasisi zote zilizopo chini ya wizara hiyo na wakamtaka Rais Jakaya Kikwete awawajibishe.
Taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu inasema kwamba nafasi ya Jairo inazibwa na Bwana Eliakim C. Maswi, ambaye kabla ya uteuzi huo alikua anakaimu nafasi hiyo.
“Kabla ya uteuzi wake, Bwana Maswi alikuwa Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa. Kwa sasa anakaimu nafasi ya Katibu Mkuu, Nishati na Madini” imesema taarifa hiyo.
|
LUHANJO |
Taarifa hiyo ambayo inanukuu taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi, Philemoni Luhanjo (Muda Mfupi kabla hajamaliza muda wake) inasema kwamba Rais Jakaya Kikwete pia amefanya uteuzi wa Makatibu Wakuu na Naibu Katibu Mkuu na pia amefanya uhamisho wa Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu kuanzia Alhamisi wiki hii.
Taarifa inasema kwamba Bwana Fanuel E. Mbonde, Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Ikulu, anahamishiwa Wizara ya Katiba na Sheria, na Bwana Alphayo Kidata, Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Ikulu, anahamishiwa Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).
Rais Kikwete pia amemteua Bwana Peter Ilomo, Mratibu Mkuu wa Sera na Mipango, Ofisi ya Rais, Ikulu, kuwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Ikulu.
Naye Bibi Susan Paul Mlawi ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Ikulu. Kabla ya uteuzi huu, Bibi Mlawi alikuwa Msaidizi wa Katibu wa Baraza la Mawaziri (Cabinet Under Secretary) Kamati ya Katiba na Bunge ya Baraza la Mawaziri.
Taarifa hiyo inamalizia kwa kusema kuwa mabwana Maswi na Ilomo pamoja na Bibi Mlawi wataapishwa Jumatatu, Januari 2, 2012, saa nne asubuhi, Ikulu, Dar es Salaam.
|
BALOZI SEFUE |
KATIKA HATUA NYINGINE, Rais Jakaya Kikwete amemteua Balozi Ombeni Yohana Sefue kuwa Katibu Mkuu Kiongozi.
Balozi Sefue anachukua nafasi inayoachwa wazi na Bwana Phillemon Luhanjo ambaye anahitimisha mkataba wake wa utumishi wa umma kesho, Jumamosi, Desemba 31, 2011.
Kabla ya uteuzi wake, Balozi Sefue alikuwa Balozi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, New York, Marekani. Kabla ya hapo, Balozi Sefue alikuwa Balozi wa Tanzania nchini Marekani na kabla ya hapo alikuwa Balozi wa Tanzania nchini Canada tokea Oktoba 2005.
Balozi Sefue anatarajiwa kuapishwa leo saa nne asubuhi ( Desemba 31, 2011) Ikulu, Dar es Salaam.