Friday, 30 December 2011

KITANZI CHA AHMAD RASHID MIKONONI MWA MAALIM SEIF LEO


KATIBU Mkuu CUF, Seif Shariff Hamad leo anaongoza Kikao cha Kamati ya Utendaji ya chama hicho kitakachopitia tuhuma za uvunjaji katiba zinazomkabili Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid Mohamed na wenzake 12.

Wakati Maalim Seif akitarajiwa kuongoza kikao hicho, tayari Hamad Rashid ametangaza kutokuwa na imani na mtendaji mkuu huyo wa CUF baada ya kunasa kile alichokiita, waraka wa siri wa kiongozi huyo, unaoeleza namna ya kumfukuza uanachama.

Wachunguzi wa mambo ya siasa wanatafsiri mkutano wa leo chini ya  Maalim Seif dhidi ya hasimu wake kisiasa Hamad Rashid, ni sawa na kwamba  ameshika kitanzi kitakachoamua hatma ya uhai au ukomo wa mwanasiasa huyo ndani ya CUF.

Hata hivyo, jana akizungumza jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Kamati ya Nidhamu na Maadili ya chama hicho, Abdul Kambaya, alisema watuhumiwa hao wakipatikana na hatia, kamati hiyo inaweza kutoa mapendekezo kwa Baraza Kuu la kutoa onyo, karipio ama kuwafukuza uanachama.
 
Kambaya, alisema kamati hiyo imemaliza kuwahoji watuhumiwa 12 na mmoja ambaye ni mjumbe wa Baraza Kuu kutoka Mbeya, hakufika kuhojiwa. “Kwa hiyo tumemaliza kuwahoji watuhumiwa wote na wametupa ushirikiano, tunachofanya sasa ni kuandaa taarifa kwenda katika kikao cha siku mbili cha Kamati ya Utendaji kitakachoanza kesho (leo) mjini Zanzibar,” alisema Kambaya.

Akizungumzia uhalali wa kamati yake, mwenyekiti huyo, alisema kamati hiyo imeundwa kutokana na maelekezo ya Baraza Kuu kupitia kifungu namba 63, kipengele namba 1 (e).

“ Katika kifungu hicho kinaruhusu Baraza Kuu kuanzisha kamati ama kurugenzi,” alisema na kuongeza kuwa  kikao cha Baraza kilichoanzisha kamati hiyo, kilikutana Novemba 3 hadi 4 mwaka huu, jijini Dar es Salaam.

Alisema baada ya Hamad Rashid  kuelezwa kuhusu uhalali wa kamati hiyo, ndipo akasema hana imani na wajumbe wa kamati hiyo. Kambaya alifafanua kwamba licha ya kusema hana imani na wajumbe hao, lakini pia aliomba apatiwe tuhuma 11 zinazomkabili ili azipitie.
“ Katiba ya chama inaruhusu mtuhumiwa kusomewa tuhuma zake na kuzijibu papo hapo siyo kwenda nazo nyumbani, hivyo Hamad amevunja tena katiba ya chama hicho kwa kutozijibu tuhuma zake,” alisisitiza Mwenyekiti huyo.   Hamad Rashid Akizungumza kwa simu jana, Hamad Rashid alisema hategemei haki kutendeka katika kikao hicho kitakachoongozwa na Maalim Seif.

“Mnafahamu kuwa kikao cha Kamati ya Utendaji kitaendeshwa na Maalim Seif ambaye ameshafanya uamuzi wa kutaka nifukuzwe uanachama,” alisema Hamad.Aliongeza kuwa, “Hivyo vikao watakavyovifanya ni mchakato ambao hatma yake wanaifahamu ila wanafanya ili kutimiza wajibu tu.”

Hata hivyo, Hamad alisema hajapata taarifa zozote za kuitwa kwenye kikao hicho.  Hivi karibuni Hamad amejikuta katika mgogoro na baadhi ya viongozi wakuu wa CUF, baada ya kutangaza rasmi nia yake ya kuwania nafasi ya Katibu Mkuu wa chama hicho.

Baada ya kuweka wazi nia yake hiyo, alianza kupita kwenye  baadhi ya matawi na kugawa misaada hatua iliyozua vurugu katika Tawi la Chechnya lililopo Manzese, Dar es Salaam na kusababisha umwagaji damu baada ya wanachama wanaomuunga mkono, kupambana na walinzi wa chama hicho, maarufu kama  Blue Guard.

Mbali na Hamad, watuhumiwa wengine  waliohojiwa ni Mjumbe wa Baraza Kuu Unguja, Juma Said Saanan, Mjumbe wa Baraza Kuu kutoka Pemba, Shoka Hamis Shoka, Mjumbe wa Baraza Kuu kutoka Tanga, Doyo Hassan Doyon na Mwenyekiti wa Wilaya ya Ilala, Doni Waziri.
Wengine ni Katibu wa Wilaya ya Ilala, Mohamed Masaga, Mwenyekiti wa Wilaya ya Temeke Abdadawi na Amir Kiyungi.
Watuhumiwa wengine waliohojiwa ni Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi Wilaya ya Temeke, Yusufu Mbungilo, Mwenyekiti wa Wilaya ya Nachingwea Nanjase, Ahmed Issa na Tamim Omar----www.mwananchi.co.tz

No comments: