Na Faki Mjaka-Maelezo Zanzibar
Wananchi wa Zanzibar wameombwa kushiriki katika Dua maalum ya Mkesha wa kuliombea taifa la Zanzibar ilioandaliwa na Umoja wa Makanisa Zanzibar ambapo Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar Balozi Seif Ali Add anatarajiwa kuwa Mgeni.
Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Mkesha huo Mchungaji Simon Mputa alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika Ukumbi wa Habari Maelezo uliopo Raha leo Mjini Zanzibar .
Amesema dua hiyo ambayo inatarajiwa kufanyika kuanzia majira ya usiku wa kuamkia Mwaka 2012 katika Uwanja wa Mao tse Tung lengo lake kuu ni kuliombea taifa kuepukana na majanga mbali mbali ambayo yanaweza kulikumba Taifa hilo .
Mchungaji Simon amesema sambamba na kuliombea taifa pia kutafanyika maombi maalum ya shukrani kwa Mungu juu ya kupatikana kwa Serikali ya Umoja wa kitaifa Zanzibar pamoja na kuwaombea viongozi wake hekima na busara katika uongozi wao
Aidha ameongeza kuwa kuna haja ya wananchi kukaa kwa pamoja na kuweza kumuomba Mungu ili kuyaepusha majanga yaliyoikumba Tanzania mwaka 2011 yasiweze kutokea tena katika Mwaka mpya wa 2012
Ameyataja majanga hayo kuwa ni pamoja na ajali ya kuzama kwa Mv. Spice Islanders Zanzibar na Mafuriko yaliyoikumba mikoa ambali mbali ya Tanzania Bara ikiwemo Dar es Salaam na kusababisha vifo vya wananchi wengi.
Kwa upande wake Katibu wa Mkesha huo Mchungaji Edward Mashimba amesema maandalizi ya Mkesha huo yamekamilika na kuwataka wananchi wa Zanzibar kushiriki kwa wingi bila kujali itikadi za dini wala siasa zao.
Mchungaji Saimon amesema Maombi hayo ni maombi shirikishi ambayo hapo awali yalikuwa yakifanywa na watu wachache lakini kutokana na mwamko wa watanzania kumesababisha maombi hayo kufanyika katika viwanja ili kukidhi haja ya wageni wanaoshiriki
Naye Mraribu wa Tamasha hilo hapa Zanzibar Allen Mbaga amesema Mkesha wa Maombi wa kuliombea Taifa utafanyika katika mikoa mbali mbali ya Tanzania Bara na Visiwani ambapo washiriki wa Zanziabar watapata burudani mbali mbali kutoka kwa vikundi vya Kwaya huku huduma ya za vitafunwa na vinywaji vikiwa vinapatikana Uwanjani hapo.
No comments:
Post a Comment