Saturday, 31 December 2011

MFAHAMU BALOZI OMBENI SEFUE

Rais Jakaya Kikwete akimwapisha rasmi Balozi Ombeni Sefue kua Katibu Mkuu Kiongozi, Ikulu, Dar es Salaam leo. (PICHA YA IKULU)

KATIBU Mkuu Kiongozi mpya, Balozi Ombeni Yohana Sefue ni mwanataaluma ya diplomasia ambaye tokea Agosti 31, 2010 amekuwa Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa mjini New York, Marekani.

Kabla ya kuteuliwa kwenda Umoja wa Mataifa, Balozi Sefue alikuwa Balozi wa Tanzania katika Marekani mjini Washington DC tokea Juni 15, 2007. Na kabla ya hapo alikuwa Balozi wa Tanzania nchini Canada nafasi aliyoishikilia kati ya Oktoba 2005 hadi Juni 2007.

Balozi Sefue amekuwa mtumishi wa Serikali tokea 1977 alipoajiriwa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa akiwa Ofisa wa Mambo ya Nje.  Alipanda nafasi Serikalini na kati ya mwaka  1987 na 1992 Bw. Sefue alikuwa Ofisa Mwandamizi katika Ubalozi wa Tanzania nchini Sweden Mjini Stockholm.

Kati ya mwaka 1993 na 2005, Bwana Sefue alikuwa mwandishi wa hotuba na msaidizi binafsi wa marais wawili – Rais Ali Hassan Mwinyi (1993-1995) na Rais Benjamin William Mkapa (1995-2005).

Miongoni mwa mambo mengine, Balozi Sefue alimsaidia Rais Mkapa wakati Rais alipokuwa Kamishna wa Afrika (Kwenye Kamisheni ya Waziri Mkuu wa Uingereza wakati huo – Mhe. Tony Blair) ambayo ilitoa ripoti iitwayo, Our Common Interest: Report of the Commission for Africa mwezi Machi mwaka 2005, na alishiriki naye kwenye Mkutano wa Wakuu wa Nchi za G8 ambao ulijadili ripoti hiyo na uliofanyika Gleneagles, Scotland mwezi Julai mwaka 2005.

Balozi Sefue pia alifanya kazi na Rais Mkapa wakati Mheshimiwa Mkapa alipokuwa Mwenyekiti Mwenza wa Kamisheni ya Shirika la Kazi Duniani ya ILO World Commission iliyojadili Masuala ya Kijamii ya Utandawazi kati ya mwaka 2002 na 2004 ambako alishiriki katika maandalizi ya ripoti ya kamisheni hiyo iitwayo A Fair Globalisation: Creating Opportunities For All, iliyotolewa mwezi Februari mwaka 2004.

Balozi Sefue alipata elimu yake ya juu katika Chuo cha Mzumbe (ambacho kwa sasa ni Chuo Kikuu cha Mzumbe) katika masuala ya Utawala mwaka 1977.  Alipata Shahada ya Uzamili katika masuala ya Sera na Utawala kutoka Institute of Social Studies (ISS) mjini The Hague, Uholanzi mwaka 1981. Pia alipata diploma ya juu katika masuala ya Uhusiano wa Kimataifa na Diplomasia kutoka Chuo cha Diplomasia cha Dar es Salaam mwaka 1986.

Balozi Sefue amemwoa Mama Anita M. Sefue na wana watoto wawili.


JK ASHIRIKI KUTOA SALAM ZA MWISHO KWA HAYATI HALIMA MCHUKA WA TBC

Rais Jakaya Kikwete akipeana mkono na Mkurugenzi Mkuu wa TBC Bw Clement Mshana wakati wa kutoa heshima za mwisho kwa mtangazaji Halim Mchuka jana katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili, kabla ya kwenda kuzikwa makaburi ya Msasani baada ya Sala ya Ijumaa.


Rais Jakaya kikwete akiwapa pole wafiwa

Rais Jakaya Kikwete na waombolezaji wakiombea mwili wa Halima Mchuka (PICHA ZA IKULU)


LUHANJO NA JAIRO WAPATA WARITHI


JAIRO
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, David Jairo aliyekuwa anatuhumiwa kwa shutuma za kuchangisha fedha kwa ajili ya kupitisha bajeti ya wizara yake (2011/2012) amepata mridhi wa nafasi yake.

Wakati huohuo, Katibu Mkuu Kiongozi Philemoni Luhanjo naye amepata mrithi wa nafasi yake. Luhanjo naye alituhumiwa kumbeba Jairo na kulidharau Bunge pale alipojaribu kumrudisha kazini Bwana Jairo katika hali ya utata.

Hii inakuja muda mfupi baada ya Bunge kupitisha maadhimio kwamba, Jairo na Luhanjo walikuwa na makosa kwa kitendo hicho cha kuchangisha fedha kutoka kwenye idara na taasisi zote zilizopo chini ya wizara hiyo na wakamtaka Rais Jakaya Kikwete awawajibishe.

Taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu inasema kwamba nafasi ya Jairo inazibwa na Bwana Eliakim C. Maswi, ambaye kabla ya uteuzi huo alikua anakaimu nafasi hiyo.

“Kabla ya uteuzi wake, Bwana Maswi alikuwa Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa. Kwa sasa anakaimu nafasi ya Katibu Mkuu, Nishati na Madini” imesema taarifa hiyo.

LUHANJO
Taarifa hiyo ambayo inanukuu taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi, Philemoni Luhanjo (Muda Mfupi kabla hajamaliza muda wake)  inasema kwamba Rais Jakaya Kikwete pia amefanya uteuzi wa Makatibu Wakuu na Naibu Katibu Mkuu na pia amefanya uhamisho wa Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu kuanzia Alhamisi wiki hii.

Taarifa inasema kwamba Bwana Fanuel E. Mbonde, Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Ikulu, anahamishiwa Wizara ya Katiba na Sheria, na Bwana Alphayo Kidata, Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Ikulu, anahamishiwa Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).

Rais Kikwete pia amemteua Bwana Peter Ilomo, Mratibu Mkuu wa Sera na Mipango, Ofisi ya Rais, Ikulu, kuwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Ikulu.

Naye Bibi Susan Paul Mlawi ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Ikulu. Kabla ya uteuzi huu, Bibi Mlawi alikuwa Msaidizi wa Katibu wa Baraza la Mawaziri (Cabinet Under Secretary) Kamati ya Katiba na Bunge ya Baraza la Mawaziri.

Taarifa hiyo inamalizia kwa kusema kuwa mabwana Maswi na Ilomo pamoja na Bibi Mlawi wataapishwa Jumatatu, Januari 2, 2012, saa nne asubuhi, Ikulu, Dar es Salaam.

BALOZI SEFUE
KATIKA HATUA NYINGINE, Rais Jakaya Kikwete amemteua Balozi Ombeni Yohana Sefue kuwa Katibu Mkuu Kiongozi.      
Balozi Sefue anachukua nafasi inayoachwa wazi na Bwana Phillemon Luhanjo ambaye anahitimisha mkataba wake wa utumishi wa umma kesho, Jumamosi, Desemba 31, 2011.
Kabla ya uteuzi wake, Balozi Sefue alikuwa Balozi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, New York, Marekani.  Kabla ya hapo, Balozi Sefue alikuwa Balozi wa Tanzania nchini Marekani na kabla ya hapo alikuwa Balozi wa Tanzania nchini Canada tokea Oktoba 2005.
Balozi Sefue anatarajiwa kuapishwa leo saa nne asubuhi ( Desemba 31, 2011)  Ikulu, Dar es Salaam.


Friday, 30 December 2011

KITANZI CHA AHMAD RASHID MIKONONI MWA MAALIM SEIF LEO


KATIBU Mkuu CUF, Seif Shariff Hamad leo anaongoza Kikao cha Kamati ya Utendaji ya chama hicho kitakachopitia tuhuma za uvunjaji katiba zinazomkabili Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid Mohamed na wenzake 12.

Wakati Maalim Seif akitarajiwa kuongoza kikao hicho, tayari Hamad Rashid ametangaza kutokuwa na imani na mtendaji mkuu huyo wa CUF baada ya kunasa kile alichokiita, waraka wa siri wa kiongozi huyo, unaoeleza namna ya kumfukuza uanachama.

Wachunguzi wa mambo ya siasa wanatafsiri mkutano wa leo chini ya  Maalim Seif dhidi ya hasimu wake kisiasa Hamad Rashid, ni sawa na kwamba  ameshika kitanzi kitakachoamua hatma ya uhai au ukomo wa mwanasiasa huyo ndani ya CUF.

Hata hivyo, jana akizungumza jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Kamati ya Nidhamu na Maadili ya chama hicho, Abdul Kambaya, alisema watuhumiwa hao wakipatikana na hatia, kamati hiyo inaweza kutoa mapendekezo kwa Baraza Kuu la kutoa onyo, karipio ama kuwafukuza uanachama.
 
Kambaya, alisema kamati hiyo imemaliza kuwahoji watuhumiwa 12 na mmoja ambaye ni mjumbe wa Baraza Kuu kutoka Mbeya, hakufika kuhojiwa. “Kwa hiyo tumemaliza kuwahoji watuhumiwa wote na wametupa ushirikiano, tunachofanya sasa ni kuandaa taarifa kwenda katika kikao cha siku mbili cha Kamati ya Utendaji kitakachoanza kesho (leo) mjini Zanzibar,” alisema Kambaya.

Akizungumzia uhalali wa kamati yake, mwenyekiti huyo, alisema kamati hiyo imeundwa kutokana na maelekezo ya Baraza Kuu kupitia kifungu namba 63, kipengele namba 1 (e).

“ Katika kifungu hicho kinaruhusu Baraza Kuu kuanzisha kamati ama kurugenzi,” alisema na kuongeza kuwa  kikao cha Baraza kilichoanzisha kamati hiyo, kilikutana Novemba 3 hadi 4 mwaka huu, jijini Dar es Salaam.

Alisema baada ya Hamad Rashid  kuelezwa kuhusu uhalali wa kamati hiyo, ndipo akasema hana imani na wajumbe wa kamati hiyo. Kambaya alifafanua kwamba licha ya kusema hana imani na wajumbe hao, lakini pia aliomba apatiwe tuhuma 11 zinazomkabili ili azipitie.
“ Katiba ya chama inaruhusu mtuhumiwa kusomewa tuhuma zake na kuzijibu papo hapo siyo kwenda nazo nyumbani, hivyo Hamad amevunja tena katiba ya chama hicho kwa kutozijibu tuhuma zake,” alisisitiza Mwenyekiti huyo.   Hamad Rashid Akizungumza kwa simu jana, Hamad Rashid alisema hategemei haki kutendeka katika kikao hicho kitakachoongozwa na Maalim Seif.

“Mnafahamu kuwa kikao cha Kamati ya Utendaji kitaendeshwa na Maalim Seif ambaye ameshafanya uamuzi wa kutaka nifukuzwe uanachama,” alisema Hamad.Aliongeza kuwa, “Hivyo vikao watakavyovifanya ni mchakato ambao hatma yake wanaifahamu ila wanafanya ili kutimiza wajibu tu.”

Hata hivyo, Hamad alisema hajapata taarifa zozote za kuitwa kwenye kikao hicho.  Hivi karibuni Hamad amejikuta katika mgogoro na baadhi ya viongozi wakuu wa CUF, baada ya kutangaza rasmi nia yake ya kuwania nafasi ya Katibu Mkuu wa chama hicho.

Baada ya kuweka wazi nia yake hiyo, alianza kupita kwenye  baadhi ya matawi na kugawa misaada hatua iliyozua vurugu katika Tawi la Chechnya lililopo Manzese, Dar es Salaam na kusababisha umwagaji damu baada ya wanachama wanaomuunga mkono, kupambana na walinzi wa chama hicho, maarufu kama  Blue Guard.

Mbali na Hamad, watuhumiwa wengine  waliohojiwa ni Mjumbe wa Baraza Kuu Unguja, Juma Said Saanan, Mjumbe wa Baraza Kuu kutoka Pemba, Shoka Hamis Shoka, Mjumbe wa Baraza Kuu kutoka Tanga, Doyo Hassan Doyon na Mwenyekiti wa Wilaya ya Ilala, Doni Waziri.
Wengine ni Katibu wa Wilaya ya Ilala, Mohamed Masaga, Mwenyekiti wa Wilaya ya Temeke Abdadawi na Amir Kiyungi.
Watuhumiwa wengine waliohojiwa ni Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi Wilaya ya Temeke, Yusufu Mbungilo, Mwenyekiti wa Wilaya ya Nachingwea Nanjase, Ahmed Issa na Tamim Omar----www.mwananchi.co.tz

MAKANISA ZANZIBAR YAANDAA MKESHA WA MWAKA MPYA


Mwenyekiti wa Kamati ya Mkesha wa Kuliombea Taifa Mchungaji Saimon Mputa (katikati) akizungumza na waandishi wa habari hawapo pichani kuhusu maandalizi ya Mkesha huo katika ukumbi wa Habari Maelezo Raha Leo,Mjini Zanziba kushoto kwake ni Katibu wa Kamati Mchungaji Edward Mashimba na kuliani kwake ni Mjumbe wa kamati hiyo Askofu Obeid Fabian

Mratibu wa Mkesha wa kuliombea Taifa, Allen Mbaga (kulia) akifafanua jambo mbele ya waandishi wa habari hawapo pichani kuhusu maandalizi ya Mkesha huo katika ukumbi wa Habari Maelezo Zanzibar, Raha Leo kuliani kwake ni viongozi mbali mbali wa Kamati ya Mkesha huo kutoka makanisa mbali mbali Zanzibar


Na Faki Mjaka-Maelezo Zanzibar

Wananchi wa Zanzibar wameombwa kushiriki katika Dua maalum ya Mkesha wa kuliombea taifa la Zanzibar ilioandaliwa na Umoja wa Makanisa Zanzibar ambapo Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar Balozi Seif Ali Add anatarajiwa kuwa Mgeni.

Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Mkesha huo Mchungaji Simon Mputa alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika Ukumbi wa Habari Maelezo uliopo Raha leo Mjini Zanzibar.

Amesema dua hiyo ambayo inatarajiwa kufanyika kuanzia majira ya usiku wa kuamkia Mwaka 2012 katika Uwanja wa Mao tse Tung lengo lake kuu ni kuliombea taifa kuepukana na majanga mbali mbali ambayo yanaweza kulikumba Taifa hilo.

Mchungaji Simon amesema sambamba na kuliombea taifa pia kutafanyika maombi maalum ya shukrani kwa Mungu juu ya kupatikana kwa Serikali ya Umoja wa kitaifa Zanzibar pamoja na kuwaombea viongozi wake hekima na busara katika uongozi wao

Aidha ameongeza kuwa kuna haja ya wananchi kukaa kwa pamoja na kuweza kumuomba Mungu ili kuyaepusha majanga yaliyoikumba Tanzania mwaka 2011 yasiweze kutokea tena katika Mwaka mpya wa 2012

Ameyataja majanga hayo kuwa ni pamoja na ajali ya kuzama kwa Mv. Spice Islanders Zanzibar na Mafuriko yaliyoikumba mikoa ambali mbali ya Tanzania Bara ikiwemo Dar es Salaam na kusababisha vifo vya wananchi wengi.

Kwa upande wake Katibu wa Mkesha huo Mchungaji Edward Mashimba amesema maandalizi ya Mkesha huo yamekamilika na kuwataka wananchi wa Zanzibar kushiriki kwa wingi bila kujali itikadi za dini wala siasa zao.

Mchungaji Saimon amesema Maombi hayo ni maombi shirikishi ambayo hapo awali yalikuwa yakifanywa na watu wachache lakini kutokana na mwamko wa watanzania kumesababisha maombi hayo kufanyika katika viwanja ili kukidhi haja ya wageni wanaoshiriki

Naye Mraribu wa Tamasha hilo hapa Zanzibar Allen Mbaga amesema Mkesha wa Maombi wa kuliombea Taifa utafanyika katika mikoa mbali mbali ya Tanzania Bara na Visiwani ambapo washiriki wa Zanziabar watapata burudani mbali mbali kutoka kwa vikundi vya Kwaya huku huduma ya za vitafunwa na vinywaji vikiwa vinapatikana Uwanjani hapo.



Monday, 19 December 2011

KAFULILA ASEMA YEYE BADO NI MBUNGE

Wakati mijadala ikiendelea juu ya kufukuzwa uanachama kwa Mbunge wa Kigoma Kusini, David  Kafulila (NCCR-Mageuzi), mbunge huyo ameibuka na kudai kwamba yeye bado ni mbunge na kwamba mwishoni mwa wiki anatarajia kutembelea jimbo lake.
Hata hivyo Mbunge huyo amekiambia kituo cha Televisheni ya Taifa (TBC 1)  kwamba hayupotayari kuzungumzia taratibu nyingine zinazoendelea ndani ya chama chake.
Wakati huohuo ripoti kutoka katika ofisi za Bunge zinasema hakuna taarifa rasmi zilizowasilishwa juu ya kuvuliwa uwanachama Kafulila.

RAIS JAKAYA KIKWETE ALIPOWAAPICHA MABALOZI WAPYA IKULU LEO

Mhe. Phillip MARMO, ameteuliwa kuwa Balozi nchini CHINA. Kabla ya hapo Mhe. Marmo alikuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge.


Dkt. Batilda S. BURIAN, ameteuliwa kuwa Balozi nchini KENYA. Kabla ya hapo Mhe. Dkt. Burian alikuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira).

Dkt. Deodorus B. KAMALA, ameteuliwa kuwa Balozi nchini BELGIUM. Kabla ya hapo Mhe. Kamala alikuwa Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki

Dkt. Ladislaus C. KOMBA, ameteuliwa kuwa Balozi nchini UGANDA. Kabla ya hapo Dkt. Komba alikuwa Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii

Bibi Shamim NYANDUGA, ameteuliwa kuwa Balozi nchini MSUMBIJI. Kabla ya hapo Bibi Nyanduga alikuwa Naibu Mkuu wa Itifaki, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa. 
Ndugu Ali A. SALEH, ameteuliwa kuwa Balozi nchini OMAN. Kabla ya hapo Bwana Saleh alikuwa Balozi Mdogo (Consul General) nchini Dubai


Bibi Grace J.E. MUJUMA, ameteuliwa kuwa Balozi nchini ZAMBIA. Kabla ya hapo Bibi Mujuma alikuwa Kaimu Mkurugenzi, Ushirikiano wa Kikanda (Regional Co-operation), Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa. (PICHA ZOTE NA IKULU)

Sunday, 11 December 2011

CCM WAKATAA ONGEZEKO LA POSHO KWA WABUNGE

NAPE
Hivi karibuni kumeibuka mjadala juu ya ongezeko la posho za wabunge kwa karibu ya asilimia mia mbili (200%) kutoka shilingi Elfu sabini mpaka shilingi Laki Mbili.

Malipo hayo yaliyoibua mjadala baina ya wadau mbalimbali, ni yale yanayohusisha posho ya kikao cha bunge kwa siku.

Chama Cha Mapinduzi kimefuatilia kwa ukaribu suala hilo la nyongeza ya posho hiyo ya wabunge kama lilivyoripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari na baadae kutolewa maelezo na Katibu wa Bunge Dokta Thomas Kashilila na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa ANNE MAKINDA.

Kwa namna suala lenyewe linavyopewa msukumo, CCM imeona si vema kuliacha bila kutoa msimamo wake kama ifuatavyo:-

i. Linapotekelezwa jambo lolote kwa kigezo cha ugumu wa maisha au kupanda kwa gharama za maisha, ni lazima jambo husika lilenge kutatua ugumu huo wa maisha kwa makundi yote katika jamii na si kwa makundi machache ndani ya jamii.

ii. Kwa kuongeza kiwango hicho cha posho kwa wabunge ni kuongeza pengo/tofauti ya mapato kati ya wenye nacho na wasionacho katika jamii yetu hasa kwa kuegemea baadhi ya makundi.

iii. Bunge ni chombo muhimu cha kutunga sheria, kinapoibuka na madai kama hayo yaliyoainishwa na Spika wa Bunge kuwa sababu za kuongezeka kwa posho hizo kunatokana na kupanda kwa gharama za maisha mjini Dodoma, ndiko kulikosababisha hofu na mashaka miongoni mwa watanzania. Na kwakweli swali kubwa hapa inakua je, maisha yanapanda Dodoma pekeake na kwa wabunge tu?

Hivyo  basi CCM inashauri kwa kuzingatia masilahi mapana ya nchi na jamii yetu kwa ujumla, waheshimiwa wabunge wetu na mamlaka zingine zinazohusika na swala hili, kulitafakari upya jambo hili. Tunaamini busara itatumika kuachana na jambo hili, kwani kuendelea nalo kunaweza kutafisiriwa ni kuwasaliti watendaji katika sekta nyingine wakiwemo Walimu, askari, Madaktari na wengineo.

Ni muhimu ifahamike kuwa kuongoza ni kuonesha njia, hivyo si sahihi kwa wabunge kuonesha njia kwa kujiongezea posho peke yao kwa kisingizio cha ugumu wa maisha huku wakiwaacha wananchi ambao ndiyo wanaowawakilisha bungeni wakikosa nafasi ya kupunguza ugumu wa maisha unaowakabili, jambo ambalo ni hatari.

Katika hatua nyingine Chama Cha Mapinduzi Kinawapongeza sana watanzania kwa ujumnla wao, bila kujali tofauti yao, kwa kushiriki kwa amani na utulivu, maadhimisho ya miaka hamsini ya Uhuru wa Tanzania Bara.

Ushiriki wao kwa pamoja, umeyafanya maadhimisho hayo yafane sana. CCM inaamini kuwa maadhimisho haya ya miaka hamsini yatatumika kuendelea kujenga uzalendo, umoja na mshikamano wan chi yetu katika kufikia maendeleo.


Imetolewa na:-
Nape M. Nnauye,
KATIBU WA HALMASHAURI KUU YA TAIFA
ITIKADI NA UENEZI
11/12/2011




Saturday, 10 December 2011

WAZIRI MKUU KUFUNGA WIKI YA MAONESHO JUMATATU

PINDA
WAZIRI MKUU Mizengo Pinda kesho kutwa (Jumatatu, Desemba 12, 2011) anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika shughuli maalum ya kufunga Wiki ya Maonesho ya Maadhimisho ya Miaka 50 ya Uhuru itakayofanyika kwenye Viwanja vya Mwalimu J. K. Nyerere, barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam.
Taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Bw. Peniel Lyimo imesema Waziri Mkuu anatarajiwa kuwasili katika viwanja hivyo saa 3.30 asubuhi na amewaomba washiriki wote kuwahi mabandani mwao mapema asubuhi.
Mara baada ya kuwasili katika viwanja hivyo, Waziri Mkuu Pinda atatembelea mabanda ya washiriki mbalimbali ili kujionea shughuli zilizozokuwa zikifanyika na baadaye atawahutubia washiriki wa maonesho hayo kabla ya kuyafunga rasmi.
Maonesho hayo yanayoshirikisha wizara, mikoa na taasisi mbalimbali, sekta binafsi na wafanyabiashara mbalimbali wa kimataifa na ndani ya nchi yalianza Desemba Mosi, 2011 katika viwanja hivyo na kufunguliwa rasmi Desemba 2, 2011 na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein. Maonesho hayo  yalikuwa ni ya bure kwa wananchi wote.
Viongozi wa kitaifa waliopo madarakani na wastaafu wametembelea maonesho hayo kwa nyakati mbalimbali.
Maadhimisho ya Miaka 50 ya Uhuru yalizinduliwa rasmi Juni Mosi, 2011 mjini Songea na Makamu wa Rais, Dk. Mohamed Gharib Bilal ambapo mambo mbalimbali yamefanyika hadi sasa. Miongoni mwa shughuli za maadhimisho hayo ni maonesho yaliyoshirikisha Wizara,  Mikoa na Sekta Binafsi ambayo yalikamilika Novemba 30, 2011.
Vilevile kulikuwa na taarifa za Miaka 50 ya Uhuru zilizoandaliwa na Wizara na Mikoa ambazo pia zimetumika pia katika kuandaa Taarifa Jumuishi ya Kitaifa iliyochapishwa kwa Kiswahili na Kiingereza. Taarifa hizo zimewekwa kwenye Tovuti ya Taifa, Tovuti ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Tovuti maalum iliyoanzishwa kwa ajili ya maadhimisho hayo.
Shughuli nyingine maalum iliyofanyika wakati wa maadhimisho hayo ni Mbio za Mwenge wa Uhuru ambazo zilitumika kuelezea mafanikio ya Serikali katika kipindi cha miaka 50.
Mwenge huo uliwashwa rasmi na Makamu wa Rais, Dkt. Bilal katika kijiji cha Butiama tarehe 14 Oktoba, 2011 na mbio hizo zilifikia kilele Desemba Mosi, 2011 jijini Dar es Salaam ambapo Rais Jakaya Kikwete alipokea mwenge huo katika Uwanja wa Uhuru na kuwakabidhi wanajeshi waliopewa jukumu la kuupandisha katika Mlima Kilimanjaro.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU

RAIS KIKWETE AKUTANA NA MAKAMO WA RAIS WA KENYA, KALONZO MUSYOKA

Rais Jakaya Kikwete akipokea ujumbe maalumu toka kwa Rais Mwai Kibaki wa Kenya uliowasilishwa na Makamu wa Rais wa nchi hiyo Mh Kalonzo Musyoka alipomtembelea leo Desemba 10, 2011 Ikulu jijini Dar es salaam. (PICHA NA IKULU)

Rais Jakaya Kikwete kulia akimsikiliza makamu wa Rais wa Kenya Kalonzo Musyoka.


Rais Jakaya Kikwete (kulia) akifanya maongezi na ujumbe wa kenya unaoongozwa na Makamu wa Rais wa nchi hiyo Mh Kalonzo Musyoka
Rais Jakaya kikwete akiulaki ujumbe wa Kenya
Rais Jakaya kikwete kulia akisalimiana na Makamu wa Rais wa Kenya Kalonzo Musyoka.


Rais Jakaya Kikwete akitambulishwa kwa Mfalme Peter Nabongo Mumia wa ukoo wa Wanga wa Magharibi mwa Kenya wakati Makamu wa Rais wa Kenya Mh. Kalonzo Musyoka alipomtembelea leo Desemba 10, 2011 Ikulu jijini Dar es salaam.






UHURU NI MIAKA 50: SHEREHE ZAFANA UWANJA WA UHURU

Rais Kikwete anakagua gwaride

Wanapendeza

Makomandooo

Makomandoooo

Mambo ya komandooo hayo

Kifaru



Hii ilikua inatoa heshima kwa kupinda bawa moja chini

Watoto wa halaiki

Hawa wamegonga 50, walizaliwa siku ya uhuru

Rais Kikwete anasema tumetoka mbali, tumefanya mengi lakini bado safari ni ndefu.

Monday, 5 December 2011

MWENGE WA UHURU HUOOOOO KUELEKEA KILELENI-MLIMA KILIMANJARO

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Mhe.Leonidas Gama akimpa mkono wa kumtakia heri mmoja wa vijana wanaopandisha Mwenge wa Uhuru kwenye kilele cha Mlima Kilimanjaro kwenye hifadhi ya Mlima Kilimanjaro zilizoko Marangu Mkoani Kilimanjaro leo tarehe 5.12.2011.

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Mhe. Leonidas Gama pamoja na Viongozi wa Mkaoa wa Kilimanjaro na wawakilishi wa Wizara ya Habari ,Vijana ,Utamaduni na Michezo wakiwasindikizaVijana wanaopandisha Mwenge wa Uhuru kwenye Kilele cha Mlima Kilimanjaro tayari kwa safari leo Marangu kwenye Hifadhi ya Mlima Kilimanjaro Mkoani Kilimanjaro.


Vijana wanaopandisha Mwenge wa Uhuru kwenye kilele cha Mlima Kilimanjaro wakiwa tayari kwa kuanzakupandisha mlima huo na Mwenge. Kwa picha zaidi; http://fullshangwe.blogspot.com/


KATIBU MKUU WA CCM ZIARANI UJERUMANI

Katibu Mkuu wa CCM,  Wilson Mukama akiwa katika mazungumzo rasmi na Karin Roth, Mbunge anaewakilisha Chama cha SPD na Katibu wa Mambo ya Nje wa SPD Belin, Ujerumani,jana. Katibu Mkuu yupo nchini ujerumani kwa ziara ya kikazi.


UJUMBE WA VIONGOZI ZANZIBAR KUTEMBELEA CHINA

Na Maelezo Zanzibar                         



Pandu Ameir Kificho

Ujumbe wa Viongozi Waandamizi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ukiongozwa na Spika wa Baraza la Wawakilishi Pandu Ameir Kificho unatarajiwa kuondoka Zanzibar hii leo kuelekea Beijing, China kwa ziara ya mafunzo ya wiki mbili.

Wakiwa nchini China viongozi hao wanatarajiwa kujifunza mambo mbali mbali ya kiutendaji pamoja na kutembelea maeneo muhimu ya uwekezaji yanayotegemewa kwa uchumi wa nchi hiyo.

Viongozi hao pia watapata fursa ya kutembelea Mji wa Shangai na Suzhuo ambapo pia wataweza kutembelea sehemu muhimu ikiwemo maeneo ya viwanda.

Mbali na Spika Kificho msafara huo utakuwa na Mawaziri nane na Naibu Waziri Mmoja wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Wengine ni wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, Maofisa na Watendaji waandamizi katika Wizara mbalimbali pamoja na waandishi wa habari

Akizungumza kwenye Mkutano Maalum wa kuagana na viongozi hao katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi,waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo Omar Yussuf Mzee amesema ziara hiyo ni muhimu kwa viongozi hao na Zanzibar kwa ujumla.

Amesema kwa kiasi kikubwa China imepiga hatua kubwa kiuchumi hivyo Zanzibar nayo kama inataka kuendelea ni jukumu la viongozi hao kujifunza na kuja kuitumia taaluma watakayoipata China kuja kuibadilisha Zanzibar.

Ujumbe wa viongozi hao unatarajiwa kurejea Nchini Desemba 20 mwaka huu.  

Sunday, 4 December 2011

CANADA SHOULD ARREST BUSH

OTTAWA — Amnesty International Canada says the federal government should arrest former U.S. president George W. Bush when he visits British Columbia next week.

The rights body says both Canadian and international law oblige Canada to detain Bush and investigate him for war crimes and torture.

Amnesty Canada's secretary general, Alex Neve, says Bush admits in his memoirs that he authorized the use of torture against terror suspects.

Neve says the Americans used a variety of torture methods, including waterboarding, beatings and sleep deprivation.

He says Amnesty has sent a lengthy document to the federal government, outlining its responsibilities under international law.

Bush and former president Bill Clinton are scheduled to attend an economic conference in Surrey, B.C., next week.