Thursday, 1 December 2011

RAIS MSTAAFU WA MAREKANI GEORGE BUSH YUPO TANZANIA

Bush

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete leo, Alhamisi, Desemba Mosi, 2011, amekutana na kufanya mazungumzo na Rais Mstaafu wa Marekani Mheshimiwa George W Bush ambaye yuko katika ziara ya siku sita nchini Tanzania.


Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika Ikulu, Dar es Salaam, viongozi hao wamezungumzia jinsi Taasisi ya Mheshimiwa Bush ya George W Bush Institute for Global Health inavyoweza kushirikiana na Tanzania katika kukabiliana na changamoto kubwa za sekta ya afya na hasa magonjwa ya saratani.


Mheshimiwa Bush ambaye anafuatana na mkewe Mama Laura Bush amemweleza Rais Kikwete mipango ya taasisi yake katika kupambana na ugonjwa wa kansa ikiwa ni pamoja na jitihada za kupima, kuzuia na chanjo.


Katika mkutano huo uliohudhuriwa pia na Mama Salma Kikwete, Rais Kikwete ametumia nafasi hiyo kumweleza Mheshimiwa Bush jitihada za serikali yake katika kupambana na magonjwa yanayoua watu wengi ikiwamo malaria, ukimwi na saratani, magonjwa ambayo mapambano yake Mheshimiwa Bush alichangia sana kifedha alipokuwa madarakani.


Rais Kikwete pia ametumia nafasi hiyo kumweleza Mheshimiwa Bush kuhusu mipango mingine ya maendeleo inayosaidiwa na Marekani ikiwa ni pamoja na mpango mkubwa wa ujenzi wa miundombinu chini ya Mpango wa MCC. 


Rais Bush na familia yake wako katika ziara ya Afrika na mbali ya Tanzania wanatembelea pia Ethiopia na Zambia.

Imetolewa na:

Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.

01 Desemba, 2011


No comments: