Monday, 5 December 2011

UJUMBE WA VIONGOZI ZANZIBAR KUTEMBELEA CHINA

Na Maelezo Zanzibar                         



Pandu Ameir Kificho

Ujumbe wa Viongozi Waandamizi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ukiongozwa na Spika wa Baraza la Wawakilishi Pandu Ameir Kificho unatarajiwa kuondoka Zanzibar hii leo kuelekea Beijing, China kwa ziara ya mafunzo ya wiki mbili.

Wakiwa nchini China viongozi hao wanatarajiwa kujifunza mambo mbali mbali ya kiutendaji pamoja na kutembelea maeneo muhimu ya uwekezaji yanayotegemewa kwa uchumi wa nchi hiyo.

Viongozi hao pia watapata fursa ya kutembelea Mji wa Shangai na Suzhuo ambapo pia wataweza kutembelea sehemu muhimu ikiwemo maeneo ya viwanda.

Mbali na Spika Kificho msafara huo utakuwa na Mawaziri nane na Naibu Waziri Mmoja wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Wengine ni wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, Maofisa na Watendaji waandamizi katika Wizara mbalimbali pamoja na waandishi wa habari

Akizungumza kwenye Mkutano Maalum wa kuagana na viongozi hao katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi,waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo Omar Yussuf Mzee amesema ziara hiyo ni muhimu kwa viongozi hao na Zanzibar kwa ujumla.

Amesema kwa kiasi kikubwa China imepiga hatua kubwa kiuchumi hivyo Zanzibar nayo kama inataka kuendelea ni jukumu la viongozi hao kujifunza na kuja kuitumia taaluma watakayoipata China kuja kuibadilisha Zanzibar.

Ujumbe wa viongozi hao unatarajiwa kurejea Nchini Desemba 20 mwaka huu.  

No comments: