Monday, 23 January 2012

SERIKALI IPO KAZINI

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kikagua ujenzi wa Chuo Kikuu cha Sayansi  na Tekinolojia cha Nelson Mandela kilichopo Arusha wakati alipokitembelea  Jana (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akifunua kitambaa ikiwa ni ishara ya kuweka jiwe la Msingi katika jengo jipya la Utawala la Shule ya Sekondari Mnolela, iliyopo kijiji cha Luhokwe, wakati akiwa katika ziara yake ya Mkoa wa Lindi jana. (Picha na Muhidin Sufiani-OMR)
Rais Jakaya Kikwete naye yupo bize Ikulu anapokea maoni ya wadau katika kuhakikisha kwamba mchakato mzima wa katiba mpya unabeba sura ya kitaifa na unakwenda kidemokrasia. Hapa alipokutana na Dr Slaa na viongozi wengine waandamizi wa CHADEMA.

Monday, 16 January 2012

NAPE: MAKUNDI KWENYE VYAMA NI KAWAIDA TU

NAPE
Siasa za Tanzania kwa siku za karibuni zinaonekana kukumbwa na zimwi la makundi ndani ya vyama, makundi ambayo wengi wamekua wakidhani kwamba ni tatizo kisiasa na kwamba pengine litapelekea kuvunjika kwa vyama husika.
Lakini leo nimepata kusikia toka kwa mwanasiasa mahiri na kijana wa Chama cha Mapinduzi, Nape Nnauye akilizungumzia suala hili tofauti kabisa na wengi wanavyofikiri.
Nape ambaye pia ni Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi, anasema kwamba ndani ya chama makundi ni muhimu yawepo na sio kitu kibaya.
Anasema kwamba ni pale tu ambapo makundi hayo yataonyesha kwamba yanachupa mipaka na kufikia hatua ya kutishia uhai wa chama, ndipo yatakua hayafai.
Ila kwa CCM, Nape anasema wazi kabisa na kwa kujiamini kwamba hakuna makundi ambayo yameshafikia hatua ya kutishia uhai wa chama.
Aidha, anasisitiza kwamba chama kama taasisi kina nguvu sana na nimaarufu kuliko mtu yeyote na kwamba endapo makundi yatafikia hatua ya kutishia uhai wa chama, basi hatua madhubuti zitachukuliwa na hakuna kitakachoharibika.

TANZANIA RED CROSS 'ACTION TEAM' WAENDELEA NA UJENZI MABWEPANDE

Vijana kazini
Ujenzi wa makazi ya muda huko Mabwepande unaendelea kwa takribani wiki ya pili sasa ambao unafanywa na kikosi maalum cha Maafa na Uokoaji mkoa wa Dar es Salaam (Action Team) cha Msalaba Mwekundu Tanzania (Tanzania Red Cross), ambapo muda wowote kuanzia sasa kaya 300 zitapelekwa huko  kwa ajili ya kuanza maisha mapya sambamba na kujenga nyumba zao za kudumu.
Viwanja hivyo kwa ajiri ya waathirika wa mafuriko jijini Dar es Salaam, vipo nje ya jiji la Dar Kilometa 6 kutoka njia panda ya Bunju B, mpaka kufika huko  Mabwepande huku usafiri wake mkubwa ukiwa ni pikipiki kwa nauli ya shilingi 1500/2000, huku kwa taxbubu nauli ikiwa ni bukubuku kwa abiria wanne.
Mpaka sasa tayari kikosi hicho maalufu kama 'TRC's Action Team', kimeweza kufikisha nyumba za muda zaidi ya 200 na tayari Rais Jakaya Kikwete ameweza kujitembelea na kujionea hali halisi ya utendaji wa kazi wa kikosi hicho ambacho pia kinashirikiana na jeshi la kujenga Taifa 'JKT'.
Katika ujenzi huo unaosimamiwa na mtaalamu maalum wa TRC's, Aidan David, alisema kua nyumba hizo ni imara na zinauwezo mkubwa wa kukaa familia tano kwa kila moja na zinadumu iwapo mtumiaji ataitumia kwa ukamilifu mkubwa sambamba na kuifanyia marekebisho kidogo.
Aidan alisema kua, watahakikisha wanajenga nyumba zaidi ya 300 katika viwanja hivyo  na zitakua faraja kwa wakazi watakaoletwa hapo na watazitumia huku wakiendelea na ujenzi wa nyumba zao za kudumu.
Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa habari hizi alibaini kasoro mbalimbali ikiwemo ufinyu wa upatikanaji huduma muhimu ikiwemo za maduka na vyakula huku vyakula vilivyopo vikiwa havikidhi mahitaji halisi ya walaji wanaofika kila kukicha katika maeneo ya viwanja hivyo kwa sasa.
Hivyo wafanyabiashara wa makampuni ikiwemo ya simu,vinywaji na chakula wanashahuriwa kufika eneo hilo la viwanja hivyo ilikurahisisha tatizo la ukosefu wa mahitaji muhimu ambapo kwa siku Mabwepande kwenye mradi huo wa viwanja inapokea watu zaidi ya 100 mbali ya wafanyakazi wa Msalaba Mwekundu,askari wa JKT, wataalamu wa barabara na Wakandarasi wanaofanya savei na kupima viwanja hivyo.
....Onyo  epuka matapeli tayari wameshavamia kwenye viwanja hivyo na namba za nyumba za watu wa jangwani wakidai kua viwanja hivyo wakipewa watawauzia watu hivyo uchunguzi umebaini watu wengi wanamiminika huko wakiangalia mianya ya kufanikisha hadhima hiyo ikiwemo kuwahadaa maafisa ardhi wa Kinondoni na kamati ya maafa ya waziri mkuu.
(Mwandishi ni Mjumbe wa kikosi cha maafa na uokoaji cha msalaba mwekundu Tanzania)


Sunday, 15 January 2012

ALIYEMPA MTEMA LESENI YA UDEREVA HAKUMTAKIA MEMA

Marehemu Mtema enzi za uhai wake.
Ni huzuni, majonzi na kwa wana familia ni pigo ambalo hawatalisahau milele. Ndio ameondoka, kwa sisi tunaoamini ‘kudra’ tunasema kwamba siku zimefika ama kwa imani ya marehemu tunaweza kusema ‘Bwana ametoa na Bwana ametwaa……”.
Naandika mistari hii ikiwa ni masaa kama 28 hivi yamepita tangu Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema) Regia Mtema afariki dunia jana pale karibu na Daraja la Ruvu barabara ya Morogoro, Mkoa wa Pwani kwa ajali ya gari.
Binafsi nimesikitika sana, nimesikitishwa na mambo mawili makubwa: 1. Mtema alikua bado kijana na alikua na matarajio mengi lakini Watanzania walikua na matarajio makubwa zaidi kutoka kwake. 2. Nimesikitishwa na taarifa kwamba marehemu alikua anaendesha gari mwenyewe.
Sote tunafahamu kwamba Mtema alikua mlemavu, hakua na mguu wa kulia ambao kwa magari ya auto ndio unaotumika kuendeshea.
Cha kushangaza ni kwamba pamoja na ulemavu huo bado Mtema alipewa leseni ya kuendesha gari na akawa anaendesha kwenye safari ndefu na kwenye barabara ambayo ina msongamano mkubwa kama hii ya Dar-Chalinze.
Nani kati yetu amewahi kujaribu kuendesha gari kwa mguu wa kushoto na akaona ugumu wake?, kwa kweli sio kitu rahisi hata kidogo.
Hata alipokua akitoa taarifa kwa waandishi wa habari jana, Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani mkoani Pwani, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Salehe Mbaga alieleza wazi kwamba kilichochangia kutokea kwa ajali ile ni ulimevu wa dereva akisema kwamba haikua rahisi kutumia mguu ule kufanya maamuzi ya haraka na sahihi.
Sasa tujiulize; nani alitoa leseni kwa marehemu? Taratibu gani za kisheria zilifuatwa mpaka akaonekana anastahiki? Bila shaka tumejifunza kitu kwa tukio hili la kusikitisha.
Kwahiyo wakati tunapita katika kipindi hiki cha majonzi na huzuni, tulitafakari na hili.

Thursday, 12 January 2012

HUDUMA ZAKIJAMII ZANZIBAR KUIMARIKA

Na FAKI MJAKA-Maelezo Zanzibar 12/01/2012

Dkt Shein akikagua gwaride.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Ali Mohamed Shein,amesema serikali yake imejidhatiti katika kuimarisha huduma za jamii kwa kasi zaidi ili ziweze kukidhi mahitaji ya wananchi wake.
Rais Shein ameyasema hayo leo alipokuwa akilihutubia taifa katika kilele cha maadhimisho ya Sherehe za miaka 48 ya Mapinduzi ya Zanzibar yaliyofanyika Uwanja wa Amani Zanzibar
Amesema mafanikio mbalimbali yaliyopatikana katika kipindi hicho cha miaka 48 ni pamoja na mfumo wa utawala bora ambapo alisema Zanzibar ya sasa imepiga hatua kubwa katika kuongoza kisheria kuliko ilivyokuwa kabla Mapinduzi hayo.
Alisema mikakati iliyopo sasa, ni kuhakikisha kilimo kinapewa kipaumbele ili kiendeshwe kitaalamu jambo litakalopelekea kuzalisha kwa wingi mazao ya chakula na biashara.
Dk Shein pia, alisema katika serikali yake inayoendeshwa kwa mfumo wa umoja wa kitaifa, kumekuwa na ushirikiano mzuri kwa watendaji, ambao unawapa imani wananchi hasa baada ya ujio wa serikali hiyo kuzika kabisa siasa za chuki na uhasama.
Alieleza kuridhishwa kwake na kasi ya maendeleo, na kuahidi kuwa serikali yake itaendelea na dhamira ya kuwapatia wananchi huduma muhimu na za uhakika kama vile elimu, afya, maji safi na salama pamoja na kuweka mazingira mazuri kwa wafanya biashara na wafanyakazi.
Katika hatua nyingine Dk. Shein amewataka Wananchi wa Zanzibar kuacha woga wa kutoa maoni yao wanayodhani yanafaa kwa Tume ya kukusanya maoni ya kupata Katiba mpya pale ambapo tume hiyo itaanza kazi zake.

Amesema Katiba inayokusudiwa kutungwa ni ya Wananchi wote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hivyo Wazanzibari ni haki yao kutoa maoni yao wala hakuna mtu atakayewabeza

Aidha amewaasa wale wote wenye tabia ya kudharau maoni ya wenzao waache kufanya hivyo kwani kila mmoja ana uhuru wake wa kutoa maoni kulingana na anavyoamini yatasaidia.
Mapema, Dk Shein alipokea saluti kutoka kwa askari wa vikosi vya ulinzi na usalama, pia kukagua Gwaride la vikosi vya Ulinzi na Usalama vya Tanzania pamoja na Maandamano ya Wananchi na Wafanyakazi wa Wizara mbalimbali za uma na sekta binafsi.
Sherehe hiyo ya kilele cha kuadhimisha miaka 48 ya Mapinduzi ya Zanzibar ilihudhuriwa na viongozi wa kitaifa akiwamo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Jakaya Mrisho Kikwete, Marais wastaafu Mabalozi mbalimbali wa Nchi za Nje waliopo Tanzania Viongozi mbalimbali wa Serikali pamoja na wananchi mbali mbali kutoka maeneo ya Tanzania Bara na Visiwani.

SHEREHE ZA MIAKA 48 YA MAPINDUZI KATIKA PICHA

Rais Jakaya Kikwete akifurahia jambo na Rais wa Zanzibar, Dr Ali Mohamed Shein
Rais wa Zanzibar, Dr Ali Mohamed Shein akikagua gwaride.

Rais Jakaya Kikwete akisalimiana na Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad

Rais Jakaya Kikwete akisalimiana na Rais wa Zanzibar, Dr Ali Mohamed Shein
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akisalimiana na Rais Mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa, wakati alipowasili kwenye Uwanja wa Aman mjini Zanzibar leo Januari 12, kwa ajili ya kuhudhuria sherehe za maadhimisho ya miaka 48 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akisalimiana na Rais Mstaafu wa Zanzibar, Aman Abeid Karume, wakati alipowasili kwenye Uwanja wa Aman mjini Zanzibar leo Januari 12, kwa ajili ya kuhudhuria sherehe za maadhimisho ya miaka 48 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Kutoka (kulia) Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, Mke wa Makamu wa Rais wa Jamhuri, Mama Asha Bilal,Rais Mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa, Jaji Mkuu, Othman Chande na Rais Mstaafu wa Zanzibar, Aman Abeid Karume, wakiwa katika sherehe hizo.

(PICHA ZOTE KWA HISANI YA: IKULU NA OFISI YA MAKAMU WA RAIS)


Thursday, 5 January 2012

JK ASHIRIKI MAZISHI YA ATHUMAN MHINA

Rais Jakaya Kikwete akiwa na Rais Mstaafu Mh Benjamin Mkapa, Waziri Mkuu Mstaafu Mh Frederick Sumaye, Makamu wa Mwenyekiti wa CCM Bara Mh Pius Msekwa na wao mbolezaji wengine kwenye mazishi ya Mwenyekitiwa Jumuiya ya Wazazi Taifa Balozi Athumani Mhina kijijini Mnyuzi, Korogwe, Mkoani Tanga jana.

Huzuni kubwa msibani

Wednesday, 4 January 2012

KIGAMBONI HAWALILII MIA

Wadau tunapoizungumzia issue ya Kigamboni tuitizame kwa ujumla wake. Issue sio mia ya abiria, tizameni bei za Maguta kutoka 200/- mpaka 1800, Bajaji kutoka 300/- mpaka 1500 n.k, bei zote zimepanda kwa  kati ya asilimia mia na miatano.

Sasa jamaa wa guta anafanya biashara gani kubwa kiasi hicho? Halafu kama haitoshi vile jamaa wa guta analipia mzigo aliobeba na kipimo hakuna wahusika wanakadiria tu kwa macho wanakuambia hii ni kilo mia, miambili au miatano na kadhalika.

Pamoja na ongezeko hilo kubwa Waziri wa Ujenzi, Dr Magufuli leo ametangaza ongezeko la mapato kwa asilimia mia tu, yani kutoka 9m/- mpaka 18m/-.
Pantoni huwa kwa kiasi kikubwa ni huduma sio biashara ndio maana huko Mombasa abiria wote wanavuka bureeeee, sasa hapa walikua wanachangia 100/- serikali inasema ni ndogo sana  haitoshi kujiendesha kibiashara.

Na iweje wakati wao wanapandishiana posho kwa asilimia miambili huko mjengoni msukuma mkokoteni na guta wamuongezee gharama za kuvuka Kigamboni kwa asilimia mia tano?

Kama maisha ni magumu kwa wabunge, basi ni magumu zaidi kwa wananchi wa kawaida na kwahiyo jitihada zozote za kumkaba mtanzania masikini lazima zipingwe kwa juhudi zote.

Serikali ni kama baba haipendezi baba anajua kabisa mtoto ana hali ngumu halafu anazidi kumwekea mazingira magumu ili ashindwe kabisa kuishi.

Tuesday, 3 January 2012

DKT JAMES MSEKELA ATEULIWA BALOZI ITALIA

Rais Jakaya Kikwete amewateua mabalozi wawili kuanzia Oktoba 12, mwaka jana, 2011, Katibu Mkuu Kiongozi, Bwana Ombeni Yohana Sefue ametangaza leo, Jumanne, Januari 3, 2012.
Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu jioni hii imesema kwamba katika taarifa yake, Katibu Mkuu Kiongozi Sefue amesema kuwa Rais Kikwete amemteua Dkt. James Alex Msekela kuwa Balozi wa Tanzania nchini Italia. Kabla ya hapo Mheshimiwa Msekela alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma.
Aidha, taarifa hiyo ya Bwana Sefue imesema kuwa Rais Kikwete amemteua Bwana Ramadhani Muombwa Mwinyi kuwa Naibu Balozi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, New York. Kabla ya hapo, Bwana Mwinyi alikuwa Katibu Mkuu Kiongozi, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
Katibu Mkuu kiongozi amesema katika taarifa yake kuwa wateuliwa hao wawili wataapishwa keshokutwa, Alhamisi, Januari 5, 2012.

TAASISI ZANZIBAR ZATAKIWA KUSAIDIA UMMA

Na Iddi Haji Issa, Maelezo Zanzibar

Wito umetolewa kwa taasisi zote zisizo za kiserikali kubadilika kwa kutekeleza shughuli zilizo na manufaa kwa umma kuliko kwa mwanachama mmoja mmoja.

Wito huo umetolewa na Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Asaa Rashid wakati wa ufunguzi wa mradi wa kuongeza uelewa juu ya sera ya jumuiya zisizo za kiserikali (NGOs) Zanzibar katika ukumbi wa chuo cha elimu mbadala Rahaleo

Alisema kuwa jumuiya zisizo za kiserikali zinalo jukumu kubwa katika kutekeleza wajibu wake hii inamaana kuwa iwapo Serikali itafanya kazi yake , sekta binafsi nazo zikafanya kazi yake bila shaka mafanikio yatakuwa makubwa.

Kwa upande wa Wizara katibu amesema wamedhamiria kukiimarisha kitengo cha jumuiya na hivi karibuni wanatarajia kufanya kazi muhimu za kupitia sheria ya jumuiya ( sheria Nam 6 ya 1995)  ili kukiwezesha kuwafikia zaidi walengwa  ambao ni jamii.

Aidha ameziomba taasisi zote kufahamu kuwa sera hiyo inatoa mwelekeo wa tunakotaka kuelekea lakini sheria imebainisha zaidi yale yaliotajwa katika sera.

Katibu huyo amesema Sheria inazitaka jumuiya zote kuelekeza kikamilifu suala zima la kuhakikisha ripoti za hesabu za jumuiya zinawasilishwa na kuangaliwa kwa usahihi wa hali ya juu.

Aidha akichangia mradi huo Mwenyekiti wa Umoja wa Wavuvi wa Kojani ( KOFDO) Omari Muhammed Ally ameiomba Serikali kutokuangalia upande wa ardhi tu ila na upande wa bahari utizamwe kwani hali inazidi kua mbaya sambamba na kuwashirikisha Wavuvi kikamilifu katika kuundwa sheria zinazo husu maswala ya bahari.

Mradi huo ambao umeanza hivi karibuni unategemewa  utaendeshwa kwa muda wa mwaka mmoja  chini ya Zanzibar Current Generation Forum ZCGF




  

DKT BILAL KATIKA MSIBA WA BALOZI ATHUMAN MHINA LEO


Makamu Wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akisalimiana na Mwenyekiti wa Wazazi wa CCM Zanzibar, Bi. Dogo Mabruk, wakati alipokuwa akiwasili nyumbani kwa aliyekuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM Taifa, marehemu Balozi Athuman Mhina, kwa ajili ya kuhudhuria shughuli za maziko, Madale jijini Dar es Salaam, leo Januari 3, 2012. Kulia ni Sophia Simba. Picha zote na Muhidin Sufiani-OMR

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akiweka saini katika kitabu cha maombolezo wakati alipofika nyumbani kwa  aliyekuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM Taifa, marehemu Balozi Athuman Mhina, kwa ajili ya kuhudhuria shughuli za maziko, Madale jijini Dar es Salaam, leo Januari 3, 2012.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akisalimiana na Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Pius Msekwa, wakati akiwasili  nyumbani kwa aliyekuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM Taifa, marehemu Balozi Athuman Mhina, kwa ajili ya kuhudhuria shughuli za maziko, Madale jijini Dar es Salaam, leo Januari 3, 2012.



Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akijumuika na baadhi ya Viongozi na wananchi kuomba dua maalum kwa  aliyekuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM Taifa, marehemu Balozi Athuman Mhina, wakati wa shughuli za maziko zilizofanyika nyumbani kwa marehemu Madale jijini Dar es Salaam leo, Januari 3, 2012.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akiagana na Mufti Mkuu wa Baraza la waislam Tanzania, Sheikh Shaaban Simba, wakati akiondoka nyumbani kwa aliyekuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM Taifa, marehemu Balozi Athuman Mhina.

MIRADI KIBAO KUZINDULIWA MIAKA 48 YA MAPINDUZI ZANZIBAR

Na Faki Mjaka, Maelezo Zanzibar


Dr Shein

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imetoa ratiba ya sherehe za kuadhimisha miaka 48 ya Mapinduzi ya Zanzibar ambazo zinaanza rasmi kesho katika majimbo yote 50 ya Unguja na Pemba

Katibu wa Kamati ya Sherehe hizo Dk. Khalid Mohamed amesema kuanzia kesho kutakuwa na kazi ya usafishaji mazingira katika majimbo yote 50 ya Zanzibar ambapo wasimamizi wa zoezi hilo ni Halimashauri za Wilaya, Baraza la Manispaa,Mabaraza ya Miji na Masheha.

Kwa mujibu wa Ratiba hiyo inaonesha kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohammed Shein atazindua Jengo la Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB) huko Mazizini Mkoa wa Mjini Magharibi

Aidha Rais Shein anatarajiwa pia kuzindua Barabara ya Dunga-Amani katika hafla itakayofanyika huko Dunga Mkoa wa Kusini Unguja ambapo Januari 9 atafungua barabara mbili (2) za Wilaya ya Chake Chake Pemba ambazo ni Chanjamjawiri-Tundaua na Chanjamjawiri-Pujini.

Katika hatua nyingine Rais Shein anatarajiwa kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa Nyumba ya Madaktari kutoka Norway katika Chuo cha Afya cha Mbweni Mkoa wa Mjini Magharibi

Halikakadhalika Rais Shein atafungua Barabara nne (4) za Wilaya ya Mkoani Kisiwani Pemba ikiwemo Mtambile-Kengeja, Mtambile-Kangani, Mizingani-Wambaa na Kenya-Chambani

Shughuli nyengine atakazofanya Dk.Shein ni Ufunguzi wa Jengo la Ofisi ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi huko Weni Mkoa wa Kaskazini Pemba na ataendesha zoezi la kuchangia Mfuko wa Fedha za Mikopo (Fund Rising) katika Hoteli ya Bwawani Mjini Zanzibar

Wakati huo huo Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim seif Sharif Hamad anatarajiwa kuzindua Jengo la Ofisi ya Makao Makuu ya Mfuko wa Barabara Zanzibar ambapo jioni yake atafungua Jengo la Idara ya Uvuvi liliopo Maruhubi katika Mkoa wa Mjini Magharibi

Aidha Maalim seif Sharif Hamad atafungua Tangi la Maji Gongoni Wilaya ya Micheweni Pemba ikiwa ni shamra sharma za kutimiza mika 48 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Naye Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Idd anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika hafla ya Ufunguzi wa Skuli ya Mkanyageni Mkoa wa Kusini Pemba ambapo pia atafungua Soko la Jumapili (Sunday Market) kwa wajasiriamali liliopo Michenzani Mkoa wa Mjini Magharibi

Viongozi wengine watakaofungua miradi mbalimbali ya maendeleo kwa nyakati tofauti ni pamoja na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Mohamed Gharib Bilal Mke wa Rais wa Jamhuri ya Muungano Tanzania Mama Salma Kikwete na Marais Wastaafu wa Zanzibar

Wengine ni pamoja na Mawaziri wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambao watahusika na ufunguzi wa miradi mbali mbali ya maedeleo

Shamra shamra za Sherehe za kutimiza miaka 48 ya Mapinduzi Zanzibar zimenza jana na ziaendelea katika mikoa yote ya Zanzibar ambapo kilele chake kitafikiwa Januari 12 katika kiwanja cha Aman Mjini Zanibar.

JK ATOA AGIZO LA KUMREJESHA MNYAMA

Rais Jakaya Kikwete ameiagiza taasisi ya utafiti wa wanyamapori (Tanzania Wildlife Research Institute - TAWIRI-) kutafiti sababu za kutoweka kwa mnyama aina ya Palahala (Roosevelt Sable Antelope) katika Hifadhi ya Taifa ya Saadani  mkoani Pwani na maeneo mengine  walikokuwa wakionekana kwa wingi hapo awali.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu leo, Rais Kikwete ametoa agizo hilo mwanzoni mwa wiki kwa Mkurugenzi Mkuu wa TAWIRI Dkt. Simon Mduma, baada ya kupokea maelezo ya  Mpango wa Kitaifa wa Kuhifadhi Tembo nchini  (Tanzania  Elephant   Management   Plan),  alipokutana na uongozi  wa taasisi hiyo katika hifadhi ya Taifa ya Serengeti mkoani Mara.
Mpango   huo  umeainisha   vipaumbele vinavyohitaji   kutiliwa   maanani   katika   kuhifadhi  na   kudhibiti  Tembo   katika   kipindi   cha miaka mitano ijayo.
Rais aliiagiza TAWIRI kwamba pamoja na kupata chanzo cha kutoweka kwa wanyama hao, pia itafutwe njia ya kuwarejesha tena, akisisitiza kwamba Palahala  ni mnyama anayevutia sana na  anaweza  akawa kivutio cha ziada katika Hifadhi ya Taifa ya Saadani,  hasa kwa utalii wa upigaji picha.
PALAHALA
Palahala ni mnyama anayevutia sana kutokana na umbo lake ambapo wawindaji hupendelea sana kumuwinda ili kupata pembe zake ndefu ambazo hutumika kama mapambo katika nyumba.  Pembe hizo pia hutumika kuchezea ngoma za kiasili.
 Rais Kikwete pia ameagiza kufanyike uchunguzi wa kina ili kujua sababu zilizosababisha kupungua kwa kasi kwa idadi ya tembo katika ukanda wa mbuga za wanyama za  Selous na Mikumi, baada ya kustushwa  na ripoti inayoonyesha kwamba zaidi ya tembo 30,000 wametoweka katika kipindi kifupi.
Rais alitoa agizo hilo baada ya Mkurugenzi Mkuu wa TAWIRI. Simon Mduma kutoa takwimu zilizoonyesha  kwamba  katika mbuga za Selous na Mikumi mwaka 2006 kulikuwa na tembo 74,900, na sensa iliyofanyika mwaka 2009 ilionyesha wamesalia 43,552.

Monday, 2 January 2012

JK AWAAPISHA MAKATIBU WAKUU WAPYA NA NAIBU KATIBU MKUU

Rais Jakaya Kikwete aklimwapisha Mh Eliakim C. Maswi kuwa Katibu Mkuu wizara ya Nishati na Madini

Rais Jakaya kikwete akimwapisha Mh Peter Ilomo kuwa Katibu Mkuu Ikulu

Rais Jakaya Kikwete akimwapisha Naibu Katibu Mkuu Ikulu Mh Suzana Mlawi