Mawaziri wawili wa zamani na mtangazaji mmoja waredio, ambaye kwa wakati huo alikuwa akimuunga mkono Waziri Mkuu wa sasa Raila Odinga, wanakabiliwa na mashitaka dhidi ya ubinaadam.
Wengine watatu waliokuwa wakimuunga mkono Rais Mwai Kibaki - akiwemo naibu Waziri Mkuu - watafikishwa mahakamani siku ya Ijumaa.
Zaidi ya watu 1,000 waliuawa katika ghasia za Kenya mwaka 2007 na 2008.
Watu wengine wapatao 500,000 walikimbia makazi yao.
Ghasia zilizuka baada ya wafuasi wa Rais Mwai Kibaki kutuhumiwa kujaribu kuvuruga uchaguzi wa urais.
Ghasia hizo zilimalizika wakati Bw Kibaki na hasimu wake Raila Odinga kukubaliana kugawana madaraka, huku Raila Odinga akiwa Waziri Mkuu.
Kenya iliiomba mahakama ya ICC kushughulikia kesi hiyo, lakini sasa inasema inaweza kuchunguza na kushitaki kesi hizo yenyewe.
Waziri wa zamani wa Elimu ya juu Wiliam Ruto, waziri wa zamani wa Viwanda Henry Kosgey na mtangazaji wa redio Joshua Arap Sang walifika mahakamani kwa ajili ya hatua ya awali za kusomewa mashitaka yanayojumuisha mauaji, kuhamisha watu na utesaji.
Wabunge wengi kutoka Kenya wanatarajiwa kuwepo mjini The Hague kuunga mkono wahsukiwa hao sita, anasema mwandishi wa BBC wa masuala ya dunia, Peter Biles.
ICC inadai kuwa njama za kihalifu zilipangwa katika eneo la Bonde la Ufa kwa wafuasi wa Rais Mwai Kibaki kushambuliwa baada ya uchaguzi.
Mwendesha mashitaka wa ICC Luis Moreno Ocampo anasema kwa kulipiza kisasi, polisi walipewa ruhusa kutumia nguvu kupita kiasi na pia kutumia magenge kushambulia raia.
Ghasia hizo nusura zisababishe mapigano ya wenyewe kwa wenyewe, huku mivutano ya muda mrefu ya kikabila na kiuchumi ikilipuka kutokana na mivutano ya kisiasa.
Tukio moja kubwa lilikuwa kuchomwa moto kwa kanisa ambalo watu wapatao 100 walikimbilia kujificha, na kusababisha vifo vingi.
Ghasia hizi zilimalizika baada ya katibu mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa Kofi Annan kufanikisha mazungumzo ya amani kati ya wagombea urais wa Kenya. Katika mpango huo wa amani, iliafikiwa kuwa waliochochea ghasia hizo wafikishwe mahakamani, ama Kenya, au katika mahakama ya ICC iliyopo The Hague.
Shirika la kutetea haki za binaadam, Human Right Watch limesema kufikishwa mahakamani kwa washukiwa hao sita, ni jambo muhimu kupima ushirikiano wa Kenya na mahakama ya ICC.
Chanzo: BBC
No comments:
Post a Comment