Saturday, 9 April 2011

Dar es Salaam inapokua jiji la aibu

Watato wanaosadikiwa kuwa ni wa mtaani wakicheza kamari pembezoni mwa barabara ya Bibi Titi katikati ya jiji la Dar es Salaam. Mambo kama haya yanalitia aibu taifa.

Kamari inaendelea wananchi wanapita wanashuhudia, magari nayo yanapita na baadhi ni ya polisi lakini hakuna hatua inayochukuliwa. Hii inanikumbusha kauli aliyoitoa mbunge mmoja hivi karibuni ya kwamba Dar es Salaam ipo kwenye orodha ya 'world's cities of shame' (Majiji ya aibu Duniani).

Hivi mgambo wa jiji wanafanya nini kama watoto kama hawa wanaeweza kujenga kibanda kati ya jiji na wakacheza kamari bila wasiwasi wowote? Tunajenga jamii ya aina gani?

Kigwangala: Mswada wa katiba sio msaafu

Dk Hamis Kigwangala

Mbunge wa Nzega (CCM) Dk Hamis Kigwangala amesema wanasiasa wasiwapotoshe watu juu ya mswada wa serikali wa mabadiliko ya katiba kwa kuwa mswada huo wa serikali sio msaafu.

Akizungumza kwenye kipindi cha televisheni moja ya hapa nchini leo asubuhi kilichorushwa moja kwa moja kutoka Dodoma, Kigwangala amesema Bunge bado linauwezo mkubwa wa kujadili na kutoa maamuzi juu ya mswada huo.

"Inasikitisha kuona kwamba wanasiasa wanawapotosha watu, kwa kuwaambia wasikubaliane na mswada huu na kwamba ni hatari kama ukimwi na matokeo yake wananchi wameacha kutoa maoni na kuanza kupiga siasa," alisema.

Baadhi ya wanasiasa wamekua wakilalamikia mswada wa katiba mpya, wengine wakidai kwamba umekuja mapema sana na wengine wakidai kwamba muda uliotengwa wa siku nne hautoshi.

"Kamswada kenyewe ni kadogo sana, nadhani hata siku moja inatosha kujadili mswada huu," alisema Kigwangala.

Friday, 8 April 2011

Bundi Alia Chadema Mbeya


Mwenyekiti wa CCM Rais, Jakaya Mrisho Kikwete akimkabidhi kadi ya CCM Bw Sambwee Mwalyego Shitambala aliyekuwa Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Mbeya wakati wa hafla fupi ya kumkaribisha CCM baada ya kukihama rasmi CHADEMA katika makao makuu ya CCM mjini Dodoma leo mchana.
Anne Makinda

Spika wa Bunge, Anne Makinda ameelezea kusikitishwa na taarifa kwamba wapo wabunge na wanasiasa wanaotumia fursa ya wananchi kutoa maoni juu ya katiba mpya kuwashawishi vijana haswa wanafunzi kufanya vurugu.

Spika Makinda ameitoa kauli hiyo Bungeni, Dodoma leo ikiwa ni siku moja baada ya vurugu zilizojitokeza Dodoma na Dar es Salaam siku ya Alhamisi ambayo ilikua ni siku ya kwanza ya utoaji wa maoni zoezi ambalo pia limeendelea leo.

Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Bila kuisoma hii huwezi kutoa maoni ya katiba mpya.

                                        http://www.tanzania.go.tz/images/katibamuungano.pdf

Libya: Waasi na Raia Wakimbia Makazi Yao Ajdabiya

Waasi wa Libya wakijipanga kwa mashambulizi

Kikundi cha majeshi ya waasi na raia wa mji wa Mashariki mwa Libya wa Ajdabiya wamekimbia makazi yao. Tukio hilo limekuja muda mfupi baada ya kushambuliwa kwa bahati mbaya na majeshi ya NATO jambo lililoyafanya majeshi ya Muammar Gaddafi yapate nguvu zaidi ya kuwashambulia.

Familia kadhaa zilionekana siku ya Alhamisi zikifungasha mizigo yao na kuingia kwenye magari ya kijeshi ya waasi kuelekea mji mkuu wa wapinzani wa Benghazi umbali wa kilometa 160 Kaskazini Mashariki mwa Libya.

Hata hivyo wananchi wa Ajdabiya wamekanusha uvumi kwamba majeshi ya Gaddafi yemeshauteka mji huo.

CHANZO: Aljazeera

Maoni ya Katiba: Tuhamie viwanjani

                                             Waziri wa Katiba na Sheria, Celina Kombani.

Vurugu zilizojitokeza Dar es Salaam na Dodoma jana zianonyesha kua tunahitaji utaratibu mzuri zaidi wa kuwafanya wananchi waweze kutoa maoni yao juu ya mchakato wa kuandikwa kwa katiba mpya.

Ni ukweli usiopingika kwamba wananchi wengi wamehamasika na kwa hivyo tunahitaji kua na sehemu kubwa zenye nafasi kama pale Jangwani (Dar es Salaam) na Jamhuri Stadium (Dodoma).

Lakini pia tunahitaji kua na mwongozo wa namna ya kutoa maoni yetu. Hii inatokana na ukweli kwamba baadhi ya viongozi wa siasa wanakwenda kwenye midahalo hii kwa kofia za vyama vyao na wanatoa maoni kwa mtazamo wa kichama zaidi bila kujali maslahi ya umma.

Watuhumiwa wa Kenya wafikishwa ICC

Washukiwa watatu wa ghasia za baada ya uchaguzi nchini Kenya mwaka 2007 wamefikishwa mbele ya mahakama ya kimataifa mjini The Hague.
Ruto
William Ruto na Joshua Sang wakiwa The Hague


Mawaziri wawili wa zamani na mtangazaji mmoja waredio, ambaye kwa wakati huo alikuwa akimuunga mkono Waziri Mkuu wa sasa Raila Odinga, wanakabiliwa na mashitaka dhidi ya ubinaadam.
Wengine watatu waliokuwa wakimuunga mkono Rais Mwai Kibaki - akiwemo naibu Waziri Mkuu - watafikishwa mahakamani siku ya Ijumaa.

Zaidi ya watu 1,000 waliuawa katika ghasia za Kenya mwaka 2007 na 2008.
Kenya
Ghasia za Kenya


Watu wengine wapatao 500,000 walikimbia makazi yao.
Ghasia zilizuka baada ya wafuasi wa Rais Mwai Kibaki kutuhumiwa kujaribu kuvuruga uchaguzi wa urais.
Ghasia hizo zilimalizika wakati Bw Kibaki na hasimu wake Raila Odinga kukubaliana kugawana madaraka, huku Raila Odinga akiwa Waziri Mkuu.
Raila
Rais Kibaki na Waziri Mkuu Odinga


Kenya iliiomba mahakama ya ICC kushughulikia kesi hiyo, lakini sasa inasema inaweza kuchunguza na kushitaki kesi hizo yenyewe.

Waziri wa zamani wa Elimu ya juu Wiliam Ruto, waziri wa zamani wa Viwanda Henry Kosgey na mtangazaji wa redio Joshua Arap Sang walifika mahakamani kwa ajili ya hatua ya awali za kusomewa mashitaka yanayojumuisha mauaji, kuhamisha watu na utesaji.
Uhuru
Uhuru Kenyatta

Siku ya Ijumaa, Uhuru Kenyatta - ambaye ni naibu waziri mkuu na mtoto wa rais wa kwanza wa Kenya, Jomo Kenyatta - anatarajiwa kufika mbele ya mahakama hiyo, pamoja na Mkuu wa Utumishi wa Umma Francis Muthaura na mkuu wa zamani wa polisi Hussein Ali, kukabiliana na mashitaka ya mauaji, kuhamisha watu, utesaji na ubakaji. Washukiwa wote sita wamekanusha kuhusika na ghasia na wanasema wako tayari kukabiliana na mkono wa sheria.

Wabunge wengi kutoka Kenya wanatarajiwa kuwepo mjini The Hague kuunga mkono wahsukiwa hao sita, anasema mwandishi wa BBC wa masuala ya dunia, Peter Biles.

ICC inadai kuwa njama za kihalifu zilipangwa katika eneo la Bonde la Ufa kwa wafuasi wa Rais Mwai Kibaki kushambuliwa baada ya uchaguzi.

Mwendesha mashitaka wa ICC Luis Moreno Ocampo anasema kwa kulipiza kisasi, polisi walipewa ruhusa kutumia nguvu kupita kiasi na pia kutumia magenge kushambulia raia.
Ocampo
Luis Moreno Ocampo


Ghasia hizo nusura zisababishe mapigano ya wenyewe kwa wenyewe, huku mivutano ya muda mrefu ya kikabila na kiuchumi ikilipuka kutokana na mivutano ya kisiasa.

Tukio moja kubwa lilikuwa kuchomwa moto kwa kanisa ambalo watu wapatao 100 walikimbilia kujificha, na kusababisha vifo vingi.

Ghasia hizi zilimalizika baada ya katibu mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa Kofi Annan kufanikisha mazungumzo ya amani kati ya wagombea urais wa Kenya. Katika mpango huo wa amani, iliafikiwa kuwa waliochochea ghasia hizo wafikishwe mahakamani, ama Kenya, au katika mahakama ya ICC iliyopo The Hague.

Shirika la kutetea haki za binaadam, Human Right Watch limesema kufikishwa mahakamani kwa washukiwa hao sita, ni jambo muhimu kupima ushirikiano wa Kenya na mahakama ya ICC.

Chanzo: BBC

Thursday, 7 April 2011

Seneta Inhofe : Utawala wa Obama Umekosea Ivory Coast

Ivory Coast's incumbent President Laurent Gbagbo (file photo) 
Rais aliyegomea Ikulu, Laurent Gbagbo

Seneta wa Oklahoma (Republican) James Inhofe amesema utawala wa Obama umekosea kwa jinsi unavyolichukulia suala la Ivory Coast kufuatia mgogoro wa kugombea madaraka kati ya Rais wa sasa (Gbagbo) na mpinzani wake anayetambulika kimataifa kama mshindi wa urais (Alassane Ouattara).

Seneta huyo ameiambai VOA kwamba utawala wa Obama unaunga mkono upande ambao sio sahahihi na kwamba ni vigumu kimantiki kwa Outtara kushinda kwenye mgogoro huo uliosababishwa na uchaguzi wa Novemba mwaka jana ambao Gbagbo anadaiwa kua alishindwa.

"Nafahamu kwamba Ufaransa wamekua wakiendesha serikali ya Ivory Coast tangu zamani, na Gbagbo hakuwa chaguo lao na tangu aingie madarakani wamekua wakimpinga. Ukweli ni kwamba Outtara ndio chaguo la Ufaransa na ninauhakika kwamba waliiba kura," alisema Inhofe.


CHANZO: VOA

Siasa na Jamii

Kwa muda mrefu sasa nimekua nikifuatilia kwa karibu sana kazi za mabloga hapa nchini, imefikia mahali nimeonelea na mimi nijiunge na jamii hii ya wanahabari wenzangu ambao kwa kiasi kikubwa wamekua wakitoa mchango mkubwa kwa jamii kupitia taarifa zao ambazo zinatuelimisha na kutuburudisha.

Binafsi nimekusudia kutizama zaidi siasa na jinsi zinavyo iathiri jamii ya watanzania na kwa upande mwingine kuangalia namna jamii inavyoathiri siasa au maamuzi ya wanasiasa. Natumai katika hili nitakua na wigo mpana wa kuhabarisha jamii kwa kuwa kila tunachokiona katika mazingira yetu kwa namna moja au nyingine kinatokana na jamii au maamuzi ya wanasiasa.

Nimatumaini yangu kwamba lengo langu hili litatimia kadri siku zinavyosogea na nimatumaini yangu pia kwamba nitapata ushirikiano mzuri kutoka kwa bloggers ambao nilikua msomaji wao na sasa mwana blogger mwenzao.

Sivibaya nikawataja baadhi ya wanablogger wachache ambao tumefahamiana muda mrefu na ambao wamekua wakinishauri nianzishe blog: http://www.issamichuzi.blogspot.com/, http://www.mjengwa.blogspot.com/ na http://fullshangwe.blogspot.com/.

PAMOJA